Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ten Hag ramani ni hii...

Ten Hag Majeruhi.png Kocha wa Man United, Erik Ten Hag

Thu, 12 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ligi mbalimbali barani Ulaya zimesimama na wachezaji wa timu hizo wamerudi kwenye mataifa yao kwa ajili ya kutumikia timu zao za taifa.

Wakati ligi hizo zinasimama kuna baadhi ya timu zimeachwa kwenye hali mbaya kutokana na matokeo waliyoyapata.

Moja ya timu hizo ni Manchester United ambayo inashika nafasi ya 10 baada ya kucheza mechi nane huku mashabiki wakiwa wameshakata tamaa licha ya ligi ndio kwanza inaanza.

Wakati huu wa mapumziko huenda ikawa ni muda sahihi wa kocha wa Mashetani Wekundu kuangalia namna ya kupata suluhu ya baadhi ya matatizo yanayo onekana kuiweka timu hiyo kwenye hali mbaya. Haya hapa ni maeneo matano ambayo Erik Ten Hag anaweza kuyafanyia kazi katika kipindi hiki ili kuipa ahueni Man United wakati ligi itakaporejea tena.

5. Sakata la Sancho

Staa huyu wa kimataifa wa England aliingia Man United huku mashabik wakiwa na matumaini makubwa, lakini mambo yanazidi kuwa mabaya hadi kufikia sasa akiwa amegombana na kocha wake. Wawili hao ambao waliingia kwenye sintofahamu mwanzoni mwa Septemba baada ya Sancho kuachwa nje ya kikosi kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Arsenal hadi sasa hawapo sawa na Sancho amekataa kuomba msamaha kocha wake ili mambo yaishe.

Katika kipindi hiki unaweza kuwa wakati mzuri kwa wawili hawa kumaliza tofauti zao na kama ikishindikana basi upitishwe uamuzi wa kumuuza Januari.

4. Mpango wa kujihami

Kwenye mechi 10 za michuano yote msimu huu, Man United imemaliza mechi mbili tu bila ya kufungwa bao. Mchezo wa kwanza kutoka bila ya kuruhusu bao ni dhidi ya Burnley ambayo imekuwa na msimu huu ikipoteza mechi zote za nyumbani na nyingine ni dhidi ya Wolves ambapo mchezo ulipomalizika mashabiki walilalamika sana kwani waliona wamenyimwa penalti katika dakika za mwisho.

Kuruhusu sana mabao kunaweza kusiwe inshu sana ikiwa utafunga mabao mengi, lakini ni mechi iliyopita tu dhidi ya Brentford Man United ilifunga zaidi ya bao moja kwenye Ligi Kuu England kwa msimu huu, jambo ambalo ni tofauti na ilivyokuwa msimu uliopita.

Inawezekana sababu kubwa ikawa ni majeraha Lisandro Martinez yupo nje wakati Luke Shaw haijulikani atarudi lini.

Hivyo, Kocha Eric ten Hag lazima aje na mbinu mbadala itakayofanya eneo hilo lipunguze makosa.

3. Tatizo la Onana

Msimu uliopita David de Gea alimaliza akiwa na tuzo ya glovu ya dhahabu baada ya kucheza mechi nyingi bila ya kuruhusu bao lakini hiyo haikumshawishi Ten Hag kuendelea naye badala yake akamsajili Andre Onana.

Kipa huyu wa kimataifa wa Cameroon ana kipaji kikubwa na hilo lilionekana msimu uliopita alipokuwa na kikosi cha Inter Milan kwenye Ligi ya Mabingwa barani Ulaya ambapo alicheza hadi fainali dhidi ya Manchester City lakini tangu atue kwenye kikosi cha Man United amekuwa akifanya makosa mengi yanayoigharimu timu hiyo.

Moja ya sababu ambazo zilifanya Onana asajiliwe ilikuwa ni uwezo wake wa kuchezea mpira kwa miguu kitu ambacho pia ndio kimekuwa kikimgharimu sana. Katika mapumziko haya inaweza kuwa wakati sahihi kwa Ten Hag kuamua ikiwa anahitaji Onana achezee zaidi mpira ama awe langoni zaidi kama alivyokuwa akifanya David de Gea.

2. Mfumo kwa Hojlund

Licha ya kufunga mabao mawili Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Galatasaray, bado Ten Haga anahitaji kuja na mbinu zitakazomuwezesha Rasmus Hojlund kufunga zaidi.

Hojlund amesajiliwa na Man United katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi hadi sasa hajaonyesha kiwango bora kilichotarajiwa na mashabiki wa United.

Moja kati ya mambo ambayo yamekuwa yakitajwa kusababisha asifunge sana ni kutokuwepo kwa ulishaji wa kutosha kwenye eneo la mwisho.

Hivyo katika kuhakikisha jamaa anatoa kinachohitajika lazima Ten Hag anadae mfumo ambao utamuwezesha Hojlundu kuwa na matokeo yanayohitajika.

1. McTominay apewe nafasi

Scott McTominay alikuwa shujaa wa Man United wikiendi iliyopita alipofunga mabao mawili na kuipa pointi tatu United. Hata hivyo, swali ni jinsi gani ataweza kumtoa Casemiro kikosini ili kumpa nafasi Scott. Katika kipindi hiki cha mapumziko Ten Hag atatakiwa kuangalia namna ya kumchezesha McTominay peke yake ama pamoja na Casemiro.

Casemiro hatakuwepo kwenye Ligi ya Mabingwa dhidi ya FC Copenhagen, kwa sababu ya adhabu ya kadi nyekundu pia atasafiri na Brazil kwenda Venezuela na siku tano baadaye ataenda Uruguay, hivyo kwa kuzingatia uchovu ambao atakuwa nao Ten Hag anaweza kuitumia nafasi hiyo kumpa nafasi MacTominay.

Chanzo: Mwanaspoti