Kocha Erik ten Hag anaripotiwa kuwa kwenye hatua za mwisho kabisa za kusaini mkataba mpya Manchester United.
Awali, kulikuwa na wasiwasi mkubwa wa kuhusu hatima ya ajira ya Mdachi huyo huko Old Trafford baada ya Man United kumaliza vibaya kwenye Ligi Kuu England msimu uliopita, ambapo ilishika nafasi ya nane.
Hata hivyo, ubingwa wa Kombe la FA iliobeba timu hiyo baada ya kuichapa Manchester City mwishoni mwa Mei umefanya Ten Hag akifikishe mataji mawili ya ndani tangu alipochukua mikoba ya kuinoa timu hiyo na hivyo Man United kukamatia tiketi ya kucheza Europa League msimu wa 2024-25.
Baada ya tathmini za msimu wa 2023-24, mabosi wa Man United, akiwamo mwekezaji mpya, bilionea Sir Jim Ratcliffe, aliamua kumbakiza Ten Hag.
Dili la sasa la Mdachi huyo lilikuwa linafika tamati mwishoni mwa msimu ujao, lakini sasa kocha huyo atasaini mkataba mpya kwa mujibu wa Fabrizio Romano, ambaye amedai kila kitu kipo kwenye hatua za mwisho kwa ajili ya kusaini dili hilo la kumfanya abaki Old Trafford.
Kunatarajiwa mabadiliko makubwa huko Man United, huku straika wa zamani wa miamba hiyo, Ruud van Nistelrooy akitarajia kutua kwenye timu hiyo kuongeza nguvu kwenye benchi la ufundi kama kocha msaidizi.
Man United ilihusishwa na makocha kibao akiwamo wa timu ya taifa ya England, Gareth Southgate, Thomas Tuchel na Mauricio Pochettino, pamoja na makocha Thomas Frank na Graham Potter.
Man United itaanza pre-season kwa kukipiga na Rosenborg, Julai 15, kabla ya kucheza na Rangers siku tano baadaye na baada ya hapo itatimkia Marekani, ambako itacheza na Arsenal, Real Betis na Liverpool kabla ya kurudi England kucheza na Man City kwenye Ngao ya Jamii.
Man United mechi yake ya kwanza kwenye Ligi Kuu England kwa msimu wa 2024-25 itakipiga na Fulham, Uwanjani Old Trafford, Agosti 16.