Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ten Hag bado anawataka

Man Utd 'moja Ya Timu Zinazoburudisha' Ligi Ya Premia   Ten Hag Kocha wa Man United, Erik Ten Hag

Sun, 28 Jul 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kocha wa Manchester United, Erik ten Hag amesema kikosi chake kinahitaji kusajili zaidi ili kuwa na mbadala katika kila eneo kuhakikisha hakiwatokei kile kilichowatokea msimu uliopita.

Kati ya mambo yaliyochangia kuiangusha Man United kwa msimu uliopita ilikuwa ni idadi kubwa ya mastaa wake wa kikosi cha kwanza kupata majeraha ya mara kwa mara.

Katika dirisha hili tayari imeshawasajili wachezaji ambao ni beki wa kati Leny Yoro iliyemnunua kwa Pauni 59 milioni sambamba na straika wa Bologna, Joshua Zirkzee aliyetua kwa Pauni 36.6 milioni.

Alipoulizwa anataka wachezaji wangapi wapya, Ten Hag alisema: “Nahitaji kuwa na kikosi kikubwa kadri inavyowezekana, tayari tumefanya usajili wa wachezaji wawili wazuri sana, kwa hivyo kila mtu anapokuwa fiti tunakuwa na timu ambayo inaweza kushinda mechi yoyote, lakini jambo kubwa zaidi ni kuwa na kikosi kipana, tunatakiwa kuwa na wachezaji wengi kwa sababu tuna mashindano magumu mbele yetu hivyo inabidi tuwe na kikosi kitakachokuwa na uwezo wa kucheza hata pale tunapokuwa na majeruhi.”

Man United inataka kujiimarisha katika eneo la beki wa pembeni na kusajili kiungo mkabaji baada ya kuibuka kwa taarida kwamba Casemiro au Scott McTominay mmoja wao anaweza kuondoka.

Vilevile, wanahitaji kumsajili beki mwingine wa kati baada ya kumpata Yoro na imewaweka katika rada Jarrad Branthwaite wa Everton na Matthijs de Ligt kutoka Bayern Munich.

“Tunataka kusajili katika maeneo muhimu ikiwezekana yote na kuwa na mpango madhubuti ili kujihakikishia kuwa tunafanya vizuri msimu ujao,” alisema Ten Hag, ambaye timu yake ilimaliza ya 8 EPL.

Chanzo: Mwanaspoti