Erik Ten Hag amecharuka kutokana na mwenendo na sera mbovu za Manchester United hasa kwenye usajili wa wachezaji.
Ten Hag pia ameponda usajili wa wachezaji waliosajiliwa miaka ya nyuma waliokuwa chini ya kiwango na kushauri kama Man United inataka mabadiliko, basi mabosi wa miamba hiyo wanatakiwa kufanya usajili wa wachezaji hatari ili washindane na timu nyingine wanapokuwa sokoni.
Man United ilimaliza nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu England msimu uliopita na kumpa wakati mgumu Ten Hag hadi kukijenga kikosi akitokea Ajax. Ten Hag aliweka wazi alitambua haraka ishu atakayokabiliana nayo alipotua Old Trafford, akasema hali haikuwa shwari ndani ya vyumba vya wachezaji vya kubadilishia nguo.
"Man United haikuwa katika hali nzuri msimu uliopita, nilipoangalia utamaduni wa klabu nilijiuliza ilikuwaje Man United ikawa hatari kipindi hicho, klabu ilisajili wachezaji wa kawaida sana miaka iliyopita, hata kiwango cha pesa kilichotumika, hakika jezi ya Man Unite ilibeba mzigo mzito," alisema Ten Hag.
Katika usajili wake wa kwanza Ten Hag alimleta Casemiro kutoka Real Madrid, Lisandro Martinez aliyetokea Ajax pamoja na Antony, sambamba na Tyrell Malacia aliyetokea Feyenooord, huku Christian Eriksen akajiunga na mashetani wekundi bure.
Hata hivyo, Ten Hag aliwahi kukiri kwenye usajili anaangalia wachezaji wanaojituma na walio tayari kupambana kwaajili ya timu.
"Tunahitaji wachezaji wapambanaji, mfano Casemiro na Raphael Varane, wachezaji hawa wana uzoefu mkubwa hasa kwenye mafanikio, Malacia, Martinez wanacheza kwa ajili ya timu, mchezaji yeyote atakayejiunga hapa anatakiwa acheze kwa kiwango cha hali ya juu," aliongeza Ten Hag.
Ten Hag ameleta mabadiliko makubwa ndani ya muda mfupi akiipandisha Man United hadi nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, vile vile wametinga robo fainali ya Kombe la Carabao. Aidha Mholanzi huyo bado anasaka wachezaji wengine ambao anaona watamletea manufaa kwenye timu.