Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ten Hag asaka mrithi wa CR7

Cristiano Ronaldo Vs United Cristiano Ronaldo

Tue, 13 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Kocha wa Manchester United, Erik ten Hag amesema watafanya juu chini kusajili straika atakayeziba pengo la Cristiano Ronaldo katika dirisha dogo la usajili, Januari mwakani.

Inafahamika nyota anayekipiga PSV Eindhoven, Cody Gakpo ndiye chaguo la Ten Hag tangu dirisha la usajili la kiangazi, hata hivyo Man United iliachana naye baada ya kumsajili Antony akitokea Ajax. Wakati huohuo Ten Hag amevutiwa na straika anayekipiga Benfica, Goncalo Ramos aliyechukua mikoba ya Ronaldo kwenye mechi ya 16 bora ya Kombe la Dunia dhidi ya Uswisi na kufunga hat -trick.

Nafasi ya Ronaldo kwenye kikosi ipo wazi baada ya Man United kuvunja mkataba na staa huyo aliyekuwa akilipwa Pauni 500,000 kwa wiki.

Ten Hag amesisitiza watasajili straika mpya kama atapatikana kwenye dirisha dogo la usajili. Chanzo cha habari kimeripoti vilevile kuwa Man United itasajili straika kama bajeti itawaruhusu kusajili kwa mkwanja mrefu. Hata hivyo, haitasajili mchezaji wa kawaida.

“Tutapambana kwa nguvu zetu. Tunaendelea na msako wa straika na kama tukipata nafasi tutahakikisha anasajiliwa kwa gharama yoyote baada ya kuwasiliana naye,” alisema Ten Hag.

Mabosi wa Man United walianza mazungumzo na uongozi wa PSV kuhusu Gakpo tangu Agosti, mwaka huu, na kwa mujibu wa ripoti mabosi hao kutoka Old Trafford wapo tayari kuendelea na mazungumzo pale walipoishia.

Gakpo alionyesha kiwango bora kwenye fainali za Kombe la Dunia inayoendelea nchini Qatar, ambako aliifungia Uholanzi mabao matatu. Hata hivyo timu yake iliondolewa na Argentina.

Ten Hag amesajili wachezaji watatu wote kutoka Ligi Kuu ya Uholanzi huku tetesi zikidai kwamba huenda Gakpo akasajiliwa na kocha huyo kwani anamvutia kutokana na aina ya uchezaji wake.

Alipoulizwa kuhusu tetesi za Gakpo kuhusishwa na Man United, Ten Hag alisema:

“Huwa sipendi kuzungumzia wachezaji ambao wana mikataba na klabu zao, lakini tunapambana kuhakikisha tunapata wachezaji sahihi. Siwezi kujibu kuhusu mchezaji wa timu nyingine. Kamwe sitajibu kuhusu hili.”

Chanzo: Mwanaspoti