Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ten Hag anavyotembelea kamba nyembamba ya Mourinho

Ten Hag Mourinhos (1).jpeg Ten Hag anavyotembelea kamba nyembamba ya Mourinho

Sat, 16 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Nyimbo zile zile za Jim Reeves. Nyakati ngumu kama hizi. Mechi ile ile. Miaka tofauti. Lakini huenda historia ikajirudia. Desemba 18, 2018 Jose Mourinho aliingia katika ofisi yake ya Carrington pale Manchester kwa ajili ya kukusanya vitu vyake vichache na kuondoka Manchester.

Si ajabu alikusanya hadi picha ya familia yake yenye mkewe Matilde Faria na watoto wake Jose Mario Jr na Maltide. Ulikuwa mwisho wa enzi. Maisha hayakwenda sawa kwa Jose Mourinho Manchester United ingawa anabakia kuwa kocha wa mwisho kuipa taji la maana United.

Walikuwa wamepokea kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa Liverpool Anfield Desemba 16. Akafukuzwa Desemba 18. United ilikuwa imegawanyika vipande vipande huku ikiwa haitoi matumaini ya kwamba Jose anaweza kubadilisha mambo na kuirudisha katika makali yake.

Umegundua kitu? Erik Ten Hag yanaweza kumkumba maswahibu ya Jose Mourinho katika tarehe kama zile. Kuna mfanano ambao haukwepeki kuelekea katika pambano hili ambalo linaamsha hisia kali kwa mashabiki wa pande zote mbili.

Jumapili jioni ataingiza timu yake kwenye Uwanja wa Anfield. Haijalishi kwamba ana majeruhi wengi na Bruno Fernandes hatakuwapo. Mara ya mwisho kwenye uwanja huo majeruhi hao walikuwapo, Bruno alikuwapo lakini Manchester United walichezea kichapo cha mabao saba.

Pambano litachezwa Jumapili Desemba 17. Kama United wakifungwa na mabosi wakaamua jambo lao Desemba 18 basi historia itajirudia. Na kuna kila sababu ya historia kujirudia. Ten Hag amekalia kuti kavu kuliko muda wowote ule Old Trafford.

Baada ya kumalizika kwa pambano ambalo lilimfukuzisha Mourinho, United walikuwa wanashika nafasi ya sita katika msimamo huku kila jambo likienda ovyo. Ni nafasi hiyo hiyo ambayo Manchester United wanaishikilia kwa sasa pale katika Ligi Kuu ya England.

Lakini katikati ya wiki walitupwa nje katika michuano ya Ligi ya Mabingwa wakiwa wanashika mkia katika kundi ambalo eti FC Copenhagen imeshika nafasi ya pili nyuma ya Bayern Munich. United imeweka kila rekodi mbovu katika kundi lake ikiwamo kufungwa mabao mengi zaidi katika hatua ya makundi miongoni mwa timu za Ligi Kuu ya England ambazo zimewahi kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Aibu iliyoje.

Katika mechi sita za kundi lake Manchester United imeondoka na pointi nne tu. timu dhaifu kama Galatasaray na FC Copenhagen zimeondoka na pointi nyingi zaidi kuliko wao. Anguko kubwa linaendelea tangu kuondoka kwa Sir Alex Ferguson.

Ten Hag anaweza kuondoka akifungwa na Jurgen Klopp. Ukiona tetesi za makocha wanaoweza kumrithi basi ujue kibarua kipo njiani kuota nyasi. Waandishi wa Kiingereza sio wajinga. Wanajua kinachoendelea nyuma ya pazia.

Lakini itashangaza kitu gani kama United watamfukuza Ten Hag? Hakuna ambacho kitashangaza. Ni kweli kwamba wazungu ni wavumilivu na wanaweza kumpa kocha muda kuweza kuijenga timu na kubadili mambo. Tatizo ndani ya uwanja United haina mwelekeo.

United haijulikani ilikotoka, ilipo wala inapokwenda. Kuanzia kwa timu kwa ujumla hadi mchezaji mmoja mmoja. United ya leo hauwezi kujua kama wanaunda timu ya muda mrefu ujao au timu ya sasa. Wamenunuliwa wachezaji wazoefu halafu wakachanganywa na vijana.

Wamenunuliwa wachezaji ambao pia wanacheza aina tofauti ya soka. United ya leo haujui wana ubora katika sehemu gani kati ya kukaa na mpira, kushambulia au kujihami. Hawafanyi kitu chochote kwa ufasaha. Kwa msimu wa kwanza matajiri na mashabiki huwa wanavumilia hili huku wakiamini kwamba timu itabadilika.

Ninachohisi kwamba Ten Hag atafukuzwa sio kwa sababu ya matokeo mabaya, hapana, bali hawana mwelekeo wa kwamba wanaweza kufika nchi ya ahadi hivi karibuni. Makocha wote watatu ambao wanaonekana kutamba England kwa sasa hawakuwa na mwanzo mzuri walipoingia katika timu zao.

Pep Guardiola, Jurgen Klopp na sasa tunaye Mikel Arteta wala hawakuwa na mwanzo mzuri katika klabu zao. Hata hivyo walihakikisha kwamba mwelekeo unaonekana. Kuna mabadiliko walikuwa wanayafanya lakini mwelekeo ulikuwa unaonekana.

Kwa mfano, baada ya Arteta kuachana na Mesut Ozil na Pierre Emerick Aubamayeng, Arsenal walisonga mbele zaidi kwa kucheza kitimu na kushika nafasi za juu katika msimamo ambazo hawakushika wakati mastaa hawa walipokuwapo.

Ten Hag naye amechukua uamuzi mgumu kama vile kuachana na kina Cristiano Ronaldo lakini kila siku timu yake inadidimia. Mwanzoni ilionekana ni suala la muda tu kwa sababu watu walikuwa na imani naye kutokana na kile alichokifanya Ajax lakini kila siku amepunguza idadi ya wafuasi wake kiasi kwamba ukiwaambia mashabiki wa United wapige kura abaki au aondoke basi anaweza kuondoka hata kabla ya pambano la Jumapili.

Muda unaonekana kumtupa mkono kwa sababu ameshindwa kutengeneza walau picha ya kufirika na namna ambavyo timu yake inaweza kuwa siku za usoni. Zaidi ya kila kitu ni kwamba ameshatumia pesa nyingi za uhamisho kwa wachezaji ambao hawajaleta matunda makubwa United.

Timu kubwa hazivumilii zaidi kwa sababu kadri zinavyofanya vibaya ndivyo ambavyo zinapoteza pesa katika soko la hisa na mikataba yake. jose Mourinho alifukuzwa huku akiwa ametoka kuipa United taji la Europa sembuse kwa Ten Hag ambaye hajaipatia taji lolote kubwa.

Tusubiri kuona kama keshokutwa Ten Hag ataweza kununua muda kwa walau kushinda au kupata sare pale Anfield. Jambo hilo halionekani sana. Hauwezi kutabiri kwamba United watapokea kichapo kikubwa Anfield kama ilivyokuwa mara ya mwisho. Hata hivyo ni wazi kwamba wanasafiri kwenda Anfield kwa mara nyingine tena wakiwa katika hali mbaya pengine kuliko walivyokuwa wakati waliposafiri mara ya mwisho na kwenda kukumbana na kipigo kikali.

Kama ataweza kubadilisha mambo Anfield au kama ataweza kubadilisha mambo kwa ujumla pale Manchester basi Ten Hag atakuwa amefanya miujiza mikubwa katika maisha yake ya soka. United ipo vipande vipande.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live