Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ten Hag analo kwa Haaland, Klopp na Arteta vita ni ugenini

Ten Hag X Pep Ten Hag analo kwa Haaland, Klopp na Arteta vita ni ugenini

Sun, 3 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Manchester United itakwenda Etihad kuwakabili mahasimu wao Manchester City kwenye kipute cha Manchester derby, huku Kocha Erik ten Hag akiwa na kazi ya kuirudisha timu yake kwenye hali ya ushindi Jumapili hii kwenye kipute hicho cha Ligi Kuu England. Ataweza?

Man United imekuwa kama ‘punching bag’ wanapokutana na mahasimu zao hao Man City kwa miaka ya karibuni na imepoteza mara tano katika mechi sita za mwisho za Manchester derby.

Baada ya kuwa na matumaini kiasi ya kurudi kwenye ubora, matatizo ya Man United yalirejea wikiendi iliyopita, wakati ilipokubali kichapo cha mabao 2-1 mbele ya Fulham tena uwanjani Old Trafford.

Baada ya bao la Alex Iwobi la dakika 97, gwiji Jamie Carragher alichambua mchezo huo wa Man United kutoa kasoro zilizowaponza na kupoteza mechi, washambuliaji waliongeza jitihada kwenye kutafuta bao la ushindi, lakini mabeki wao walikuwa nyuma zaidi na kuacha uwazi katikati ya uwanja, ambayo iliwafanya wapinzani kuitumia na kutengeneza bao lao la ushindi.

Kocha Ten Hag alijaribu kumjibu Carragher, lakini mashabiki wa Man United hawatakuwa na muda wa kusikilizia kisingizio kingine kutoka kwa kocha Ten Hag endapo watakumbana na kipigo kesho.

Ubora wao upoje?

Kabla ya kipigo cha wikiendi iliyopita, Man United ilishinda mechi nne mfululizo kwenye Ligi Kuu England. Jambo hilo liliwafanya mashabiki wa Man United kuamini timu yao imerudi kwenye ubora mkubwa wa kukamatia Top Four, lakini Fulham ikawakumbusha ugonjwa wao bado hawajapona.

Katikati ya wiki, ilicheza na Nottingham Forest kwenye Kombe la FA na kushinda bao 1-0, shukrani kwa bao pekee la kiungo Casemiro. Lakini, wenzao Man City katika mechi kama hiyo ya Kombe la FA, waliichapa Luton Town mabao 6-2 huko uwanjani Kenilworth Road na straika Erling Haaland alifunga mabao matano pekee yake. Man City imeshinda mechi 14 kati ya 15 za mwisho ilizocheza Etihad na mechi ambayo hawakushinda ilikuwa ya sare ya bao 1-1 dhidi ya Chelsea. Man United itachomoka?

Vikosi vipoje?

Kocha Ten Hag ataendelea kuwakosa mastaa kadhaa kwenye kikosi chake akiwamo Mason Mount, Anthony Martial, Tyrell Malacia na Lisandro Martinez. Straika, Rasmus Hojlund naye anasumbuliwa na maumivu ya misuli, wakati Luke Shaw atakosa baada ya kuwa na maumivu kwenye paja.

Aaron Wan-Bissaka aliumia mazoezini mapema mwezi uliopita, lakini Harry Maguire anaweza kurejea kikosini baada ya kukosa nmchezo dhidi ya Forest. Kwa upande wa Man City, yenyewe itamkosa Jack Grealish baada ya kuumia kwenye mechi ya Luton. Kikosi hicho cha Kocha Pep Guardiola kimepata mzuka baada ya kurejea kwa beki wao wa kati, Josko Gvardiol, ambaye alikuwa akisumbuliwa na maumivu ya enka.

Masteringi wa mchezo

Man United bila shaka watatawaliwa na wapinzani wao kwenye sehemu kubwa ya mchezo na kitu ambacho wanapaswa kukifanya ni kuwa makini zaidi kwenye safu yao ya ulinzi. Lakini, kama watahitaji kushinda, watapaswa kwenda mbele kushambulia kwa kutumia akili kubwa.

Marcus Rashford bado hajaonyesha ubora mkubwa na Hojlund hayupo, hivyo kiungo Bruno Fernandes atakuwa na majukumu makubwa ya kuonyesha ubora wake wa kumsaidia Ten Hag kupata matokeo kwenye mechi hiyo muhimu.

Kwa upande wa Man City, steringi wa mchezo bila ya shaka atakuwa Haaland. Kevin De Bruyne kazi yake itakuwa kumchezesha tu Haaland kuendeleza majanga huko Man United na wana kumbukumbu naye baada ya kuwafunga hat-trick msimu uliopita.

Rekodi zikoje?

Rekodi zinaonyesha Man City na Man United zimekutana mara 53 kwenye Ligi Kuu England na katika mechi hizo, sare ni tisa, huku Man United ikishinda 25, mara 12 nyumbani na 13 ugenini, huku Man City ikishinda 19, mara 10 nyumbani na tisa ugenini.

Mechi tano za mwisho walizokutana kwenye ligi hiyo, Man City imeshinda nne na Man United moja tu, jambo ambalo linatia mashaka makubwa kwa mwendo huo wa misimu ya karibuni kama Ten Hag na chama lake ataweza kutoboa ugenini.

Mambo ni moto

Mchakamchaka wa Ligi Kuu England utaendelea kwa mechi kibao katika wikiendi hii na mchezo mwingine wa kesho utakuwa Turf Moor, wakati wenyeji Burnley watakapokuwa na kibarua kizito Bournemouth.

Rekodi zao zinaonyesha miamba hiyo imekutana mara tisa kwenye mechi za Ligi Kuu England na Burnley imeshinda sita, tatu nyumbani na tatu ugenini, huku Bournemouth yenyewe imeshinda tatu, mbili nyumbani na moja ugenini. Kinachovutia ni hawajawahi kutoka sare.

Liverpool kampeni yao ya kuendelea kubaki kileleni kwenye msimamo wa ligi hiyo itakuwa ugenini The City Ground, watakapokwenda kukipiga na Nottingham Forest. Jurgen Klopp na kikosi chake cha Liverpool ameshanyakua taji la Kombe la Ligi msimu huu na sasa mchakato upo kwenye kunasa ubingwa wa ligi.

Kikosi hicho kwa sasa kinaongoza ligi kwa tofauti ya pointi moja, hivyo kwenye mchezo wa Nottingham Forest kitahitaji ushindi ili kuweka pengo la pointi kufikia nne.

Rekodi zinaonyesha Liverpool na Forest zimekutana mara 13, Forest imeshinda tatu, zote kwenye uwanja wa nyumbani na Liverpool imeshinda sita, zote uwanjani Anfield.

Sare ni nne. Kwa maana hiyo, Liverpool itajaribu kusaka ushindi wa kwanza ugenini mbele ya Forest, ambao wamekuwa vizuri wanapokuwa nyumbani.

Chelsea wanaojikongoja mdogomdogo watakuwa Gtech Community kukipiga na Brentford. Namba si nzuri sana kwa Chelsea wanapocheza na Brentford na kwenye mechi tano walizokutana kwenye Ligi Kuu England, sare moja, Brentford imeshinda tatu na Chelsea moja tu.

Kinachovutia kuhusu mechi hiyo ni Brentford haijawahi kushinda nyumbani dhidi ya Chelsea, huku The Blues ushindi wao mmoja waliopata kwenye mechi ya ligi dhidi ya wapinzani wake hao, ulikuwa ugenini. Kipute kingine matata kitakuwa huko Goodison Park na Everton itakuwa na kibarua kizito mbele ya West Ham United. Kinachovutia kuhusu mchezo huo ni utamkutanisha David Moyes na timu yake ya zamani.

Everton na West Ham zimekutana mara 55 kwenye mchezo wa Ligi Kuu England na mechi 13 zilizomalizika kwa sare, huku Everton ikishinda 29, mara 16 nyumbani na 13 ugenini, huku West Ham yenyewe imeshinda mara 13, saba nyumbani na sita ugenini.

Wababe Fulham watashuka uwanjani kwao Craven Cottage kucheza na Brighton katika mechi inayotazamiwa kuwa na upinzani mkubwa. Namba zinaonyesha kwenye mechi saba ambazo timu hizo zilikutana kwenye michezo wa Ligi Kuu England, Brighton haijawahi kushinda hata moja, huku sare zikiwa nne na Fulham imeshinda tatu, mbili nyumbani na moja ugenini.

Newcastle United itajimwaga uwanjani kwao St. James’ Park kucheza na Wolves. Mambo ni moto kwelikweli. Takwimu zao zinaonyesha timu hizo zimekutana mara 17 katika mechi za Ligi Kuu England na sare ni 11, huku Newcastle ikishinda nne, tatu nyumbani na moja ugenini, wakati Wolves yenyewe imeshinda mbili tu, moja nyumbani na nyingine ugenini. Kutakuwa na kipute cha London derby, wakati Tottenham Hotspur itakapokuwa nyumbani kucheza na Crystal Palace.

Miamba hiyo kwenye Ligi Kuu England imekutana mara 29 na mechi saba zilimalizika kwa sare, huku Spurs ambao watakuwa wenyeji wameshinda 18, tisa nyumbani na tisa nyingine ugenini, huku Palace wao wakishinda nne tu, mechi tatu nyumbani na moja ugenini.

Luton Town itakuwa Kenilworth Road kukipiga na Aston Villa katika moja ya mechi zinazotazamiwa kuwa na upinzani mkali.

Aston Villa ipo kwenye mbio za kuwamo ndani ya Top Four ili kukamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, watakwenda kugenini kusaka pointi tatu muhimu. Luton na Aston Villa zimekutana mara moja tu kwenye Ligi Kuu England na mechi hiyo, Villa ilishinda ilipocheza kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Villa Park.

Arsenal inangoja Jumatatu

Wakati wapinzani wao kwenye mbio za ubingwa, Liverpool wakiwasha moto leo, huku wapinzani wengine Man City zamu yao ikiwa kesho, kocha Mikel Arteta na chama lake la Arsenal litakuwa na kibarua Jumatatu, kujaribu kusaka pointi za kuendelea kwenda jino kwa jino kwenye kilele cha msimamo wa ligi hiyo.

Mechi hiyo itafanyika Bramall Lane, takwimu zinaonyesha kwamba kwenye mechi tatu zilizofanyika katika uwanja huo baina ya Sheffield United na Arsenal, wenyeji walishinda mara mbili na Arsenal moja.

Kwa jumla wake, timu hizo zimekutana mara 11 kwenye Ligi Kuu England, ambapo mechi nne zilimalizika kwa sare, huku Arsenal ikishinda nne, tatu nyumbani na moja ugenini, wakati Sheffield United imeshinda mbili, zote kwenye uwanja wake wa nyumbani. Je, Arsenal itatoboa? Ngoja tuone.

Chanzo: Mwanaspoti