Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ten Hag anahitaji wawili tu, mmoja ni Ugarte

Erik Ten Hag City Motisha Kocha wa Man United, Erik Ten Hag

Sat, 24 Aug 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kana ulikuwa hujui, Erik ten Hag mambo yake si rahisi Manchester United.

Alihitaji subira ya wiki kadhaa kabla ya kuambiwa kwamba ataendelea kubaki huko Old Trafford na sasa Mdachi huyo anakabiliwa na msimu mgumu zaidi wa kupata au kukosa wakati akiendelea kufahamiana na mabosi wake wapya.

Sir Jim Ratcliffe, Sir Dave Brailsford, Jean-Claude Blanc, Dan Ashworth na Jason Wilcox wapo wanamsikilizia tu kocha Ten Hag na hawatasita kumfuta kazi endapo atashindwa kufanya jambo la maana katika msimu wake wa tatu kwenye kikosi hicho cha Old Trafford.

Bilionea Ratcliffe na washirika wake wamempa sapoti kocha Ten Hag kwa kutumia karibu Pauni 150 milioni kwenye usajili wa mastaa wapya hadi sasa, lakini bado kuna wachezaji wengine inaendelea kuwasaka. Hivyo Ten Hag ana siku sita tu kabla ya dirisha la usajili kufungwa ili kutambua hatima ya kikosi chake kamili ambacho atatamba nacho kwenye Ligi Kuu England na michuano mingine kwa msimu huu wa 2024-25.

Je, Man United bado inahitaji kufanya kitu kwenye usajili huu wa majira ya kiangazi kabla ya dirisha hilo kufungwa, Agosti 30.

Kipa na mabeki

Bado hakuna ushawishi kama Andre Onana ni kipa wa kumtumaini zaidi katika kumaliza shida za timu hiyo, lakini shida iliyopo ni kwamba hakuna kipa mwingine wa kumtishia nafasi kutokana na Altay Bayindir kuwa na kiwango cha kawaida tu kinachomfanya aendelee kuwa chaguo la pili.

Man United iliweka kipaumbele kikubwa kwenye safu yake ya mabeki kwenye dirisha hili na ndio maana imesajili mabeki wa kati wawili pamoja na kiraka wa kucheza beki za pembeni pande zote kulia na kushoto. Man United inaweza kufanya usajili wa beki zaidi baada ya sasa kuhusishwa na mkali wa RB Leipzig, Castello Lukeba. Kinda huyo ni beki wa kati anayetumia mguu wa kushoto, eneo ambalo linadaiwa kuwa shida kwa Man United kwa kukosa beki wa maana wa kati anayetumia mguu wa kushoto. Uzuri ni kwamba anaweza kupatikana kwa Pauni 29 milioni tu.

Lukeba anaweza kwenda kujifunza zaidi kwa Lisandro Martinez na huenda akatumika pia kwenye beki ya kushoto kutokana na Luke Shaw na Tyrell Malacia kuwa na majeraha ya mara kwa mara. Ujio wake unaweza kufungua milango ya Victor Lindelof kuondoka kikosini, huku pia akija kupunguza pengo la beki Leny Yoro, aliyeamia na kulazimika kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu. Usajili huo ukifanyika basi Man United itakuwa na wachezaji wanne wenye uwezo wa kucheza beki ya pembeni huku itakuwa na mabeki sita wa kali, watakaoondoa presha kabisa.

Kiungo

Eneo hili linajieleza. Manuel Ugarte ni chaguo muhimu kwenye rada ya Man United, ambapo kiungo huyo wa Uruguay anatazamwa kama mrithi wa kudumu wa Mbrazili Casemiro. Paris Saint-Germain inahitaji ilipwe Pauni 51 milioni ili imwaachie kiungo huyo kwenye Old Trafford na sasa Man United inaonekana kuwa tayari kutoa pesa ili kunasa saini yake kabla ya dirisha halijafungwa, Agosti 30.

Ni wazi, Ugarte atakapotua tu Old Trafford jambo hilo litamfanya Casemiro kutambua hatima ya nafasi yake kwenye kikosi cha miamba hiyo kwa msimu huu. Casemiro, 32, alicheza vizuri kwenye mechi ya kwanza ya Ligi Kuu England dhidi ya Fulham, lakini umri wake unatia shaka kama ataendelea kubaki kwenye kiwango bora kwa msimu wote. Kutokana na hilo, Man United inahitaji saini ya kiungo kama Ugarte ili kumfanya aje kucheza na kinda anayeibukia kwa kasi kwenye eneo hilo, Kobbie Mainoo. Scott McTominay anaweza kuendelea kubaki kwenye timu, lakini Christian Eriksen umri umeshaanza kumtupa mkono, huku Mason Mount, yeye ni bora zaidi akacheza kwenye Namba 10 kuliko kiungo ya kati.

Washambuliaji

Jadon Sancho inawezekana ameshamaliza tofauti zake na kocha Ten Hag, lakini bado uchezaji wake una mashaka mengi, haonekani kuitumikia Man United kwa mapenzi. Winga huyo aliyesajiliwa kwa ada ya Pauni 73 milioni huu ni msimu wake wa tatu, lakini bado haonekani kuwa msaada zaidi ya kupa matatizo tu Man United kuliko kuwa suluhisho. Man United inaweza kuchagua kumuuza tu, baada ya Chelsea kuhitaji saini yake.

Sancho bado ana umri wa miaka 24, anaweza kwenda kuwa mchezaji wa kiwango cha dunia kwe nye nchi nyingine, lakini kwenye Ligi Kuu England pameonekana kuwa mahali pagumu kwa upande wake. Kitu kama hicho pia kinamhusu Mbrazili, Antony, hana kitu cha maana ambacho amefanya kwenye kikosi cha Man United tangu aliposajiliwa kwa pesa nyingi kutoka

Ajax.

Licha ya kwamba kumekuwa na maelezo ya Man United kusajili straika mwingine kwenye dirisha hili, hayo yatakuwa matumizi mabaya ya pesa. Rasmus Hojlund na Joshua Zirkzee wanatosha kufanya safu ya ushambuliaji ya timu hiyo kuwa tishio sambamba na Bruno Fernandes, wakati mwingine kutumika kama Namba 9 bandia, huku kwenye timu yupo Marcus Rashford mwenye uwezo wa kucheza nafasi ya ushambuliaji wa kati, pamoja na kinda Ethan Wheatley. Hivyo, katika siku chache zilizobaki kabla ya dirisha la usajili kufungwa, eneo la ushambuliaji kwa Man United kwa sasa hawapaswi kusumbuka nalo, wasubiri kuona kitakachotokea msimu huu na kufanya tathmini mwakani.

Hitimisho

Kwa maana hiyo, kwa tathmini ya kikosi cha Man United kilivyo, maeneo ambayo wanapaswa kufanya usajili kwa siku sita zilizobaki kabla ya dirisha hilo kufungwa ni kuweka mkazo kwenye usajili wa kiungo wa kati, hasa Ugarte ambaye tayari amekushakubali kutua Old Trafford, pamoja na beki wa kati anayetumikia mguu wa kushoto, eneo ambalo wakimpata Lukeba watakuwa wamefanya usajili wa maana katika dirisha hili. Jarrad Branthwaite, linaweza kuwa chaguo sahihi pia endapo kama watafanikiwa kunasa huduma ya beki huyo wa kati kabla dirisha hili kufungwa.

Chanzo: Mwanaspoti