Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ten Hag ampiga mkwara Onana

Ten Hag X Onana Ten Hag ampiga mkwara Onana

Sun, 22 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kocha wa Manchester United, Erik ten Hag amemtaka kipa wake Andre Onana kupandisha kiwango chache kutokana na mwanzo mbaya aliokuwa nao ndani ya timu hiyo aliyojiunga nayo katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka huu kutokea Inter Milan.

Onana ameruhusu mabao 19 katika mechi 11 za Man United aliyojiunga nayo kwa dau la Pauni 47.2 milioni kama mrithi wa David de Gea ambaye hakuongezewa mkataba mpya na timu hiyo bada ya ule wa awali kumalizika.

Idadi kubwa ya mabao ambayo Onana ameruhusu, yameonekana kutokana na makosa yake binafsi jambo ambalo limekuwa likiwakwaza mashabiki wa klabu hiyo ambao baadhi yao wamekuwa wakishinikiza kipa huyo wa Cameroon awekwe benchi.

Hilo limemuibua Ten Hag ambaye licha ya kusifu ubora wa kipa huyo wa zamani wa Ajax Amsterdam amemtaka kufanya kazi ya ziada ili aweze kuwa na kiwango bora zaidi ili aweze kuisaidia timu yake.

Ten Hag anaamini kwamba 0nana atakuja kuwa staa mkubwa na tegemeo la Man United siku za usoni kwani hata makipa wawili walioacha alama kubwa klabuni hapo, Peter Schmeichel na David de Gea hawakuwa na mwanzo mzuri.

"Anajua na sisi tunajua atafanya vizuri sana. Kila mchezaji anayekuja katika Ligi Kuu ya England anahitaji kipindi cha mpito lakini anahitajika kupandisha zaidi kiwango. Makipa wakubwa wa United kama Peter Schmeichel na David de Gea hawakuanza vizuri na Onana hii ni vizuri akajua kidogo kutoka kwenye historia.

Kocha huyo alisema kuwa uamuzi unabaki kwa Onana mwenyewe kujituma ili aonyeshe kiwango kizuri katika mechi zijazo.

"Lakini tunaishi sasa, tunaishi kesho na anatakiwa atengeneze wakati wake ujao kwa kutoa kiwango kizuri. Nina uhakika ataweza," alisema Ten Hag.

kocha huyo Mholanzi alisema kuwa kitendo cha Onana kutocheza na safu ya ulinzi ambayo imekuwa ikibadilika mara kwa mara kutokana na majereha, kumemfanya kipa huyo kuathirika.

"Sitotumia majeraha kama utetezi na Andre hawezi kufanya hivyo lakinikila wakati unapokuwa na mstari tofauti wa ulinzi mbele yako haisaidii. Haisaidia mpito wake kiukweli," alisema Ten hag.

Katika msimu wa 2022/2023, Onana aliichezea Inter Milan idadi ya mechi 41 za mashindano tofauti na katika mechi hizo alifungwa mabao 36 huku akicheza mechi 13 bila kuruhusu bao.

Chanzo: Mwanaspoti