Kocha wa Man United, Erik ten Hag na Mkongwe Sir Alex Ferguson wakiwa katika picha ya pamoja walishikilia Kombe la Carabao 2022/23 baada ya Mholanzi huyo kumkaribisha Ferguson kusherehekea ushindi wa kombe hilo.
Manchester United ilitwaa kombe la Carabao 2022/23 kufuatia ushindi wa 2-0 dhidi ya Newcastle United katika pambano lililopigwa kwenye Uwanja wa Wembley.
Mabao yote mawili ya Manchester United yalifungwa kipindi cha kwanza. Mpira wa kichwa wa Carlos Casemiro uliipatia Manchester United bao la uongozi mnamo dakika ya 33.
Dakika sita baadaye shuti kali la Marcus Rashford lilielekezwa wavuni na mlinzi wa Newcastle United Sven Botman na kuipatia Manchester United bao la ushindi.
Erik ten Hag alishinda taji lake la kwanza kama meneja wa United ikiwa pia ni taji la kwanza kwa Mashetani hao Wekundu tangu Jose Mourinho alipoiongoza kutwaa kombe la Europa League mnamo 2017.
Awali Erik ten Hag alionekana kutokuwa na ukaribu na Sir Alex Ferguson lakini uhusiano kati yao ulionekana wa karibu sana wiki iliyopita. Kabla ya fainali ya Kombe la Carabao kuchezwa wawili hao walikula chakula cha jioni pamoja.
"Alichofanya [Ferguson] kwa Manchester United kilikuwa cha ajabu, kilitutia moyo sisi sote," alisema Ten Hag.
Mbali na kumwalika Ferguson, Ten Hag pia alimwalika Avram Glazer kwenye chumba cha kubadilishia nguo cha United. Avram ni mwanachama wa familia ya Glazer inayomiliki klabu hiyo kwa sasa.