Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ten Hag aitumia Man City kama motisha

Erik Ten Hag City Motisha Kocha wa Man United, Erik Ten Hag

Sun, 11 Aug 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kocha wa Manchester United, Erik Ten Hag amewataka wachezaji wake kusikia maumivu na kuutumia mchezo wao wa Ngao ya Jamii dhidi ya majirani zao Man City kama motisha ya kufanya vizuri kwenye msimu ujao lakini pia amesifia kiwango cha timu yake.

Man United ilipoteza mchezo huo wa Ngao ya Jamii kwa penalti 7-6 baada ya kutoka sare ya bao 1-1 katika dakika za kawaida.

Matumaini ya mashetani wekundu kushinda ngao yalizimwa na Jadon Sancho na Jonny Evans ambao walikosa penalti zilizoipa Man City ushindi.

Ten Hag amesema licha ya kufungwa amefurahishwa na kiwango ambacho wachezaji wake wameonyesha katika mechi hiyo.

"Tumeumizwa na matokeo na itabidi tuhisi maumivu na kila mchezaji ameonyesha hilo jambo ambalo kwangu lina ishara nzuri, lakini pia nimeona baadhi ya mambo chanya niliyoyaona, tulionyesha kiwango bora sana na tulikuwa na uwezo wa kushinda mechi, tulikuwa tunaongoza kuanzia katika mechi na hata kwenye mipigo ya penalti, lakini mwisho wa yote tumepoteza na tumeumia sana lakini tunatakiwa kuchukua mazuri ambayo yametokea katika mechi hii."

Katika mchezo huo, Marcus Rashford ambaye alifanya vibaya msimu uliopita akifunga mabao manane tofauti na ilivyokuwa katika msimu wa kwanza chini ya Ten Hag alipofunga mabao 30, katika mechi hiyo alikosa nafasi mbili za wazi lakini Ten Hag anasema hilo sio tatizo na anaamini atafunga sana msimu ujao.

"Nafikiri alikuwa katika nafasi nzuri muda mwingi, nafurahishwa sana na namna anavyokuwa katika nafasi kwa sababu kama Rasmus Hojlund akirudi na yeye akaendelea kucheza vile anavyocheza na timu kwa ujumla, mabao mengi yatafungwa."

Kocha wa City, Pep Guardiola alisema hajafurahishwa na kiwango cha timu yake licha ya ushindi huo.

Guardiola alionekana akifoka na kulaumu wachezaji wake muda mwingi wa mchezo na hata wakati wa mapumziko alionekana akipiga chupa ya maji kutokana na hasira zilizompata kutokana na kiwango cha timu yake.

Alipoulizwa ikiwa ushindi huo unatoa ishara ya kwamba anaweza kwenda kushinda taji la Ligi Kuu England kwa mara ya tano mfululizo alisema: "Ningependa kujibu ndio lakini sijui, hatukuwa katika ubora wetu leo, kiwango tulichoonyesha kilikuwa ni cha chini sana, tungeweza kupoteza hata mechi leo, zilisalia dakika chache kabla ya hilo kutokea. Ni kawaida lakini jambo zuri ni kwamba tumeanza ligi kwa kushinda kombe. Utofauti ni kwamba tumeshinda tu taji lakini hakuna kilichobadilika juu ya ukweli kwamba tulicheza vibaya."

Chanzo: Mwanaspoti