Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ten Hag afurahi Rashford kutemwa England

Marcus Rashford Marcus Rashford

Tue, 18 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kocha wa Manchester United, Erik ten Hag amesema Marcus Rashford amestahili kupigwa chini kwenye kikosi cha England kilichokwenda kwenye Euro 2024 huko Ujerumani.

Rashford alikuwa mmoja kati ya mastaa wenye majina makubwa ambao wamewekwa kando na kocha Gareth Southgate kwenye kikosi chake hicho cha Euro 2024, huku wengine waliotoswa ni Jordan Henderson, Jack Grealish na James Maddison.

Na kocha wa Man United, Ten Hag alisema wala hakushangazwa na kitendo cha Rashford kuachwa.

Akizungumza wakati anafanya uchambuzi huko Uholanzi kwenye chaneli ya NOS, akichambua mechi ya England ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Serbia kwenye mechi yao ya kwanza kwenye Euro 2024, Ten Hag alisema: “Grealish na Rashford wote walishindwa kufanya vyema msimu uliomalizika. Na unaposhindwa kufanya vizuri, basi huwezi kuchaguliwa na timu yako ya taifa.”

Rashford alishuka sana kiwango chake msimu uliopita, ambapo fowadi huyo alifunga mabao manane tu kwenye michuano yote, wakati mwaka mmoja kabla alitikisa nyavu mara 30. Na alipoulizwa kwanini kiwango cha staa huyo kimeshuka, Ten Hag alijibu hilo Aprili: “Ni mjadala unaovutia.

“Anajua, najua. Ni kitu anachopaswa kukifanyia kazi yeye binafsi, lakini na timu pia inatakiwa kumsaidia. Ni mjadala kwa sababu ni kitu kinachohusisha takwimu.”

Rashford alipigwa faini ya kukatwa mshahara wa wiki mbili baada ya kushindwa kuhudhuria mazoezi kufuatia kukesha akilewa huko Belfast. Fowadi huyo alisafiri kwenda Ireland Kaskazini wakati wa siku ya mapumziko mapema mwaka huu kwenda kumtembelea mchezaji mwenzake wa zamani, Ro-Shaun Williams, anayechezea Larne, na baadaye aliripotiwa kwamba aliugua akiwa kwenye treni.

Jambo hilo lilimfanya Rashford akose mechi ya Kombe la FA dhidi ya Newport, lakini baadaye alirudishwa kwenye timu na kuendelea kucheza, huku ikielezwa kwamba fowadi huyo na kocha wake Ten Hag bado hawana mazungumzo mazuri.

Kuhusu mchezo wa England na Serbia, Ten Hag aliponda mtindo wa kocha Gareth Southgate kwamba alifanya wapinzani wake wamshambulie sana na kucheza mechi kwa kuzingaria matukio. England itakipiga na Denmark, Alhamisi hii kisha itamaliza na Slovenia, Juni 25.

Chanzo: Mwanaspoti