Kocha wa Manchester United Erik ten Hag amewataka wachezaji wa timu kuweka akili zao kwenye mechi zijazo na kuachana na kufikiria hali ya kesi ya mshambuliaji wa timu hiyo Mason Greenwood.
Ten Hag amesema hayo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari juu ya maandalizi ya timu kuelekea mchezo wa Ligi dhidi ya Crystal Palace siku ya Jumamosi ambapo ameeleza kuwa siku zote akili lazima iwaze mchezo ujao.
Kauli hiyo inakuja baada ya kesi zote zilizokuwa zinamkabili Mason Greenwood, 21, kutupiliwa mbali na mahakama baada ya mashahidi kujiondoa kutoa ushahidi na hivyo mahakama kuachana na kesi na Greenwood kubakia huru.
“Tunapaswa kufikiria kuhusu mechi yetu siyo kitu chochote”, alisema ten Hag.
Greenwood alikamatwa Januari 2022 akituhumiwa kuhusika kwenye matumizi ya nguvu na jaribio la kubaka kwa mpenzi wake hiyo ni baada ya picha jongeo kuvuja.
Alipoulizwa kama anazungumziaje kuachiwa huru kwa mshambuliaji wake, kocha huyo alisema hana neno la kusema kwa hivi sasa akirejea taarifa ya klabu.