Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tembo yasaka rekodi tu kwa Mnyama ASFC

Tembo Ooo Tembo yasaka rekodi tu kwa Mnyama ASFC

Fri, 8 Dec 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati Tembo FC ikipangwa dhidi ya Simba, timu hiyo ya mkoani Tabora imesema inahitaji kuandika historia kwa kushinda mchezo huo wa Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na kufuzu hatua inayofuata.

Timu hiyo kwa sasa haishiriki mashindano yoyote zaidi ya michuano hiyo ya shirikisho, inahitaji kuweka historia kwa kuifunga Simba na kutinga 32 bora ya ligi hiyo.

HISTORIA YAO

Tembo FC yenye maskani yake wilayani Nzega mkoani Tabora siyo wageni kwenye soka la ushindani kwani waliwahi kushiriki Ligi Daraja la Pili (First League). Timu hii ilianzishwa mwaka 1987 ikiwa chini ya Halmashuri ya Wilaya ya Nzega na baada ya kushuka daraja mwaka 1996 halmshauri hiyo ilijitoa kuiendesha na kuchukuliwa na mashabiki.

Hata hivyo, kwa muda mrefu haikuwa kwenye mashindano yoyote kutokana na kukosa uongozi thabiti wa kuiendesha kwa madai ya ukata na kujikuta ikipotea muda mrefu.

Msimu wa 2016/17 ilifufuka tena chini ya baadhi ya wadau wakishirikiana kuanza kuiendesha na kuirudisha kwenye Ligi ya Wilaya kisha Daraja la Tatu Mkoa wa Tabora japokuwa haikutwaa ubingwa.

Kwa sasa timu hiyo ndio wawakilishi wa Mkoa wa Tabora kwa upande wa michuano ya ASFC baada ya kufanya vizuri hatua za awali kwa kushinda mechi mbili.

Mchezo wa kwanza dhidi ya Ziba FC ya wilayani Igunga na kushinda mabao 2-1 kisha kucheza na bingwa wa Ligi Daraja la Tatu, Mambali FC na kutakata kwa mabao 2-1 na sasa wanaenda kunyukana na Simba.

KOCHA KIROHO SAFI

Kocha mkuu wa timu hiyo, Ramadhan Kiroge anasema pamoja na kupangwa dhidi ya Simba, wao siyo jambo kubwa kwani walifuzu hatua hiyo wakitarajia kukutana na timu yoyote.

“Kukutana na Simba ni fursa ya kujitangaza kwani kwa sasa mpira ni ajira nawaomba vijana wapambane kuonesha uwezo wao.

Tunaenda kuandika historia matokeo yatajulikana ndani ya dakika 90 na hatutaingia kinyonge uwanjani.

“Hatuwezi kuiogpa Simba licha ya kuwa na wachezaji wakubwa wenye uzoefu kuliko sisi, ila dakika 90 zitaamua, tutapambana kwakuwa tupo kwenye maandalizi ya nguvu,” anasema Kiroge.

KIBU NA CHAMA

Kocha huyo bila kupepesa macho anakiri Simba ina mastaa wengi wenye ubora wakiwemo Kibu Denis na Clatous Chama ni miongoni mwa wachezaji wanaoweza kuamua mechi muda wowote.

Anasema kwakuwa Tembo FC haifuatiliwi na wapinzani hao, lakini wao wanaifuatilia Simba kwenye mechi zao, hivyo wataingia uwanjani kwa tahadhari na kujilinda zaidi.

“Tunaitamani sana hiyo mechi tushinde tuandike historia mpya kwenye soka hapa nchi, tunajua haitakuwa mchezo mwepesi ila tunaendelea na maandalizi kufikia malengo,” anasema kocha huyo.

STRAIKA ATAMBA

Nahodha wa timu hiyo, Rajabu Twaha ‘Chungu’ anasema wanatarajia kufanya maajabu kwa kuwafunga wapinzani hao akitambia uzoefu alionao na uwezo wa wachezaji kikosini.

Straika huyo aliyewahi kukipiga Rhino Rangers anasema licha ya kukutana na Wekundu hao msimu wa 2012/13 na kufungwa mabao 2-0, lakini hii ni mechi nyingine.

Anaeleza mechi itakuwa ngumu, lakini wanaendelea kujipanga akiwaomba wenzake kuhakikisha kila mmoja anatimiza majukumu yake.

“Tunawaheshimu ni timu kubwa, lakini kwenye mpira lolote linawezekana, wakifanya makosa tukayatumia vyema tutashinda, kimsingi wachezaji wote tutumie majukumu yetu vyema.

“Kwetu wachezaji ni nafasi nzuri kutumia mechi hiyo kujitangaza kuonesha ubora kwani hata dirisha dogo la usajili litakuwa limefunguliwa, matarajio ni kufuzu hatua inayofuata,” anasema.

UONGOZI MATUMAINI

Katibu mkuu wa timu hiyo, Rashid Msamaki anasema pamoja na ukongwe wao lakini kwa muda mrefu hawakuwa kwenye mashindano ila hawana hofu yoyote kucheza na Simba.

Anasema uongozi unapambana kuweka mipango bora kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri akitambia uwapo wa baadhi ya mastaa waliowahi kucheza Ligi Kuu kuongeza nguvu.

“Wachezaji wengi ni makinda hawana uzoefu sana wa ligi za ushindani, lakini wapo wawili kama Chungu na Mussa Digubike ambao walishacheza Ligi Kuu miaka ya nyuma wakiwa na Rhino Rangers.

“Tunajua mchezo huo utakuwa mgumu kwa sababu ya wapinzani ni timu kubwa yenye mafanikio kwenye soka ndani na nje hivyo tunaenda kwa nidhamu kupambana,” anasema Msamaki.

Kigogo huyo anasema kinachowapa hamasa zaidi ni baadhi ya wadau wanaoonesha nia na mapenzi ya kuwasapoti akiwamo Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Nzega na mbunge wa Jimbo hilo, Hussein Bashe.

“Mpaka sasa bado hatujatenga bajeti kwa sababu wadau wanaendelea kuahidi, hivyo hadi mechi ikikaribia tutakuwa tumejua la kufanya.

“Tunashukuru baadhi ya viongozi wanashirikiana na sisi akiwamo mkuu wa wilaya yetu, Naitapwaki Tukai na mbunge ambaye ni Waziri wa Kilimo, Bashe ambaye tuko naye pamoja kwenye hili,” anasema kiongozi huyo.

Chanzo: Mwanaspoti