Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tembo Warriors wakabidhiwa zawadi na Serikali

20221011 180633 Tembo Warriors wakabidhiwa zawadi na Serikali

Tue, 11 Oct 2022 Chanzo: eatv.tv

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa ametimiza ahadi ya Serikali ya kuwazawadia donge nono Timu ya Soka ya Taifa ya Tembo Warriors iliyoshiriki mashindano ya Kombe la Dunia kwa watu wenye ulemavu nchini Uturuki na kushika nafasi ya saba kidunia.

Akiongea leo, Oktoba 11, 2022 jijini Dar es Salaam kwenye hafla ya kuikaribisha nyumbani na kuipongeza timu hiyo, amesema mafanikio ya ushindi huo unatokana na utashi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan katika kuwekeza kwenye michezo na hamasa ya watanzania kwenye michezo kwa ujumla.

Aidha, amefafanua kwamba ushiriki wa Tembo Warriors katika mashindano haya umesaidia kuitangaza Tanzania duniani na amewataka wanamichezo wengine wanaoshiriki mashindano ya kimataifa kuiga mfano wa Tembo Warriors kuweka uzalendo mbele na kupigania nchi yao.

Amewaagiza watendaji wa mashirikisho ya michezo nchini kushirikiana na Serikali kuvisaidia vilabu vinavyocheza mashindano ya kimataifa huku akiwataka watendaji wa Serikali kusimamia kikamilifu mashindano yote ya kimataifa ili kupata matokeo tarajiwa.

Amesisitiza kuwa kama vilabu vyote vya michezo vitaweka maslahi ya taifa mbele na kuacha kufikiria maslahi binafsi michezo itafika mbali.

Ametumia nafasi hiyo kuipongeza Timu ya Simba kwa kuishinda 3-1 timu ya C.D Primeiro de Agosto ya Angola katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kuwatakia kila la kheri Timu ya Soka ya Taifa ya Serengeti Girls inayocheza kesho na Timu ya Taifa ya Japan katika mashindano ya Dunia chini ya umri wa miaka 17 yanayoanza kesho nchini India.

Amewataka Watendaji wa Wizara kuwakumbusha vilabu vyote kukamilisha mpango kazi wa kujenga miundombinu ya michezo kama walivyokubalina katika kikao cha hivi karibuni baina ya wizara na vilabu vyote vya michezo huku akisisitiza kuwa hiyo ni kulingana na matakwa ya sera ya michezo inayoelekeza kila klabu kuwa na miundombinu.

Chanzo: eatv.tv