Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tegete aibukia Mwadui FC, aanza na ushindi

John Tegete Kocha mkongwe nchini, John Tegete

Wed, 3 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kocha mkongwe nchini, John Tegete ameingia makubaliano ya kuifundisha timu ya Mwadui FC kwa muda hadi mwisho wa msimu huu, huku akianza kibarua chake kwa ushindi dhidi ya Alliance FC katika michuano ya First League.

Tegete ambaye aliwahi kuzifundisha timu za Alliance, Mbao na Toto Africans alianza kazi Mwadui FC yenye maskani yake mkoani Geita Desemba 30, mwaka huu na juzi (Jumapili) akaiongoza kupata ushindi wa mabao 2-1 mbele ya Alliance kwenye Uwanja wa Nyamagana, Mwanza.

Mabao ya Mwadui FC yalifungwa na Edison Ibrahim, huku Vincent Costa akiifungia Alliance kwa kichwa kupitia mpira wa kona ambapo mchezaji Amani Juma wa Alliance alionyeshwa kadi nyekundu. Kwa ushindi huo Mwadui imefikisha pointi 10 katika nafasi ya tano huku Alliance ikiwa na pointi nne kwenye nafasi ya saba.

Tegete anachukua nafasi ya Almasi Shaban aliyekuwa na timu hiyo tangu mwanzo wa msimu huu akiiongoza katika michezo sita akishinda miwili, sare moja na kufungwa tatu na kuvuna pointi saba.

Akizungumza na Mwanaspoti kuhusu kibarua chake kipya, Tegete alisema uongozi wa timu hiyo umemuomba awasaidie kuinoa kwa wakati huu ambao kocha mkuu ameondoka na kuamua kukubaliana nao kwakuwa amewahi kufanya nao kazi akiwa Toto Africans.

Alisema licha ya kukaa na wachezaji hao kwa siku mbili ameona wana kitu na ana imani kubwa atafanya vizuri na kupanda daraja kwenda Championship huku akiwaomba viongozi kutimiza wajibu wao kwa kuwasaidia wachezaji na kuwatimizia mahitaji yao.

“Namshukuru Gao (Waziri) ambaye ndiye mmiliki wa timu amejitahidi sana kupata wachezaji wazuri wenye uwezo mkubwa, bado ni wachezaji ambao wanachipukia na bahati nzuri kwa sababu mimi niko hapa basi alinikabidhi timu hii kwamba nimsaidie kufundisha.

“Kwa sababu nimekaa naye sana kwenye mpira nikasema siwezi kumkatalia lazima nimkubalie, kwanza alikuwa bosi wangu, nikasema sawa nitakuwa kwenye timu.”

Chanzo: Mwanaspoti