Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Team Ronaldo, ukiwa mbele yao, usimseme vibaya CR7

Team Ronaldo Team Ronaldo, ukiwa mbele yao, usimseme vibaya CR7

Wed, 29 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Wikiendi iliyopita mshambuliaji wa Manchester United, Aljandro Garnacho alifunga bao kali la tik-taka kwenye mchezo dhidi ya Everton kisha akashangilia kwa staili ya Ronaldo maarufu kama ‘Siiiiu’.

Bao alilofunga linafanana kabisa na lile alilowahi kufunga Wayne Rooney akiwa na Mashetani Wekundu dhidi ya Manchester City, lakini stori kubwa mbali ya bao hilo ilikuwa ni jinsi alivyoshangilia.

Inadaiwa kuwa Garnacho ambaye ni raia wa Argentina ni shabiki mkubwa wa Ronaldo na sio nahodha wake wa timu ya taifa na shujaa wa Argentina katika Kombe la Dunia, Lionel Messi, ambaye wanatoka taifa moja. Garnacho aliwahi kuonekana amevaa ‘boxer’ ya CR7 ambayo aliiacha wazi watu waione na juzi akashangilia bao lake bora zaidi kwa staili ya supastaa huyo wa Ureno ya ‘Siiiiu’.

Lakini huyu sio mchezaji pekee ambaye amekuwa na mahaba makubwa na Ronaldo

ERLING HAALAND

Staa huyu wa Manchester United unaweza kumtaja kama mmoja kati ya washambuliaji bora duniani kwa sasa, lakini aliwahi kukiri kwamba asingewahi kuwa mchezaji bora na kufika hapo alipofika kama isingekuwa Ronaldo.

“Kila siku amekuwa ni kiigizo changu na ningependa kukutana naye na kumpa shukrani kwa vile nimekuwa mchezaji kwa sababu yake.’’

KYLIAN MBAPPE

Licha ya mara kadhaa nayeye kujumuishwa na Ronaldo kwenye vinyang’anyiro vya tuzo mbalimbali, Mbappe amekuwa shabiki wa Ronaldo tangu utotoni.

Kwenye chumba chake wakati huo kulikuwa na picha za Ronaldo na alishawahi hadi kupiga naye picha ikiwa katika kuonyesha mapenzi kwa staa huyo.

Hata hivyo, kwenye siku za hivi karibuni inaelezwa kwamba mapenzi yake yamepungua.

MARCUS RASHFORD

Muda mwingine unahitaji kuangalia mipira ya friikiki za Rashford ili kugundua kwamba jamaa anamfuata Ronaldo.

Mwaka 2018 alipofanya mahojiano na tovuti ya Man United, Rashford alisema: “Wachezaji wengi wadogo waliokuwa wanaitazama timu wakati yeye anacheza hapa walikuwa wakimuiga, ukimuangalia jamaa anakuwa mzuri kila siku, wachezaji wengi wameshindwa kufanya anavyofanya yeye katika umri wake lakini yeye ameweza, kawaida mastaa wengi kuanza kupunguza makali wakiwa na umri mkubwa lakini kila siku yeye amekuwa akienda juu.”

Mwaka huu huu, Ronaldo alimtumia jezi Rashford iliyoandika ‘kwako Murcus, endelea kufanya kazi nzuri.”

Matthijs de Ligt

Inaelezwa kuwa wakati akiwa mdogo Matthijs de Ligt alikuwa akijiita Ronaldo pale alipokuwa akicheza soka na wenzake, mitaani na mwaka 2019 baada ya kujiunga na Juventus akitokea Ajax ndoto yake ikatimia, akaenda kucheza na Ronaldo timu moja.

“Kila siku nilitamani kuwa Ronaldo, na alinivutia sana kipindi kile anacheza Manchester United, jezi ya kwanza ya mpira wa miguu kuwahi kuivaa ilikuwa ina jina lake.”

JOAO FELIX

“Ni mtu niliyekuwa namtazama sana wakati nikiwa mdogo, niliiga kila kitu kutoka kwake, bado nilikuwa na umri mdogo na yeye alikuwa tayari mchezaji bora duniani. Anaweka historia kwenye mpira wa miguu, watu huniuliza kila siku kama naweza kufikia alipofika Ronaldo, huwa nawaambia Cristiano ni wakipekee, kila siku napambana kuwa Joao Felix.”

JAMES MADDISON

Kiungo wa Tottenham alikuwa shabiki wa Manchester United alipokuwa mdogo na mchezaji aliyekuwa akimpenda zaidi ni Ronaldo na hadi sasa bado ipo hivyo.

“Kiigizo changu ni Cristiano Ronaldo, tangu nakua nilikuwa namuangalia yeye kwa sababu pia nilikuwa shabiki wa Man United.”

HARRY KANE

Inawezekana watu wengi wakasema kwamba ilitosha awe kiigizo chake mwenyewe kutokana na kiwango chake, lakini ukweli ni kwamba staa huyu ana umri wa miaka minane pungufu kwenye umri wa Ronaldo.

Baada ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa kati ya Real Madrid na Tottenham mwaka 2017, Kane alisema: “Ni mtu ambaye ni kiigizo changu, nimekuwa namuangalia tangu nikiwa mdogo, nimebadilishana naye jezi kwa sababu jezi yake ni nzuri kuwa nayo, nimempa jezi yangu sijajua ataenda kufanya nayo nini.”

VINICIUS Jr

Jamaa hana kificho kwenye suala la kuwa shabiki mtiifu wa Ronaldo, hili lilianza kuonekana mwaka 2020, kwenye dimba Santiago Bernabeu alishangilia kama Ronaldo ile staili yake ya ‘Siiiiiu’, baada ya hapo alithibitisha kwenye ukurasa wake wa Instagram kwamba yeye ni shabiki wa Ronaldo.

GABRIEL MARTINELLI

Staa huyu Arsenal mwaka 2020 aliweka wazi kuwa kila siku alikuwa akimuangalia Ronaldo kama kiigizo chake.

“Kiigizo changu ni Cristiano Ronaldo, nampenda sana jinsi alivyo, jinsi anavyofanya kazi na kila kitu chake, kuanzia yeye mwenyewe na tuzo alizopata, ni mtu ambaye hajawahi kuridhirika, kila siku anataka zaidi, na hivi ndivyo ninavyohitaji hata mimi, yeye ni mfano mkubwa kwangu”

RAHEEM STERLING

Wakati anaichezea Liverpool, Raheem Sterling alithibitisha kwamba mchezaji Ronaldo ni mmoja ya watu anaowatazama kama kiigizo chake.

“Namuangalia sana Cristiano Ronaldo, kama mchezaji napenda kutazama wale waliofanikiwa duniani na kwa sababu nataka kuwa bora”

BRUNO FERNANDES

Inawezekana kwa sasa yeye ndo akawa mmoja kati ya wachezaji wanaokubalika ndani ya Man United lakini mwaka 2020, kapteni huyu wa sasa wa Mashetani Wekundu alisema sababu mojawapo iliyomfanya akubali kujiunga na Man United ilikuwa ni Ronaldo.

“Mimi ni shabiki mkubwa wa Cristiano Ronaldo ni mchezaji ambaye kila siku namfuatilia,” alisema Bruno wakati anahojiwa na Sky Sports.

JUSTIN KLUIVERT

Baba wa staa Justin Kluivert aitwaye Patrick Kluivert, alikuwa mmoja kati ya wachezaji bora kuwahi kutokea nchini Uholanzi. Lakini mtoto wake amekuwa ni shabiki wa kutupwa wa Ronaldo na sio mdingi wake.

“Kwa jinsi alivyo ndani na nje ya uwanja, mtu ninayemuangalia sana ni Cristiano Ronaldo, nimekuwa nikimpenda tangu nikiwa mdogo, daima namfuatilia ingawa hadi sasa sijawahi kupiga naye picha,” alisema Kluvert alipokuwa akihojiwa na DAZN.

MEMPHIS DEPAY

Baada ya kusajiliwa na Manchester United, Mei, 2015, Memphis Depay aliweka wazi kwamba mtu ambaye amekuwa akimvutia zaidi kwenye mpira wa miguu ni Ronaldo.

“Yeye ni mmoja kati ya wachezaji ninaowaangalia, na ni mchezaji mkubwa inawezekana pia akawa mchezaji mkubwa zaidi duniani, nilikuwa nikimuangalia sana jinsi anavyopiga mipira ya friikiki na jinsi anavyofanya mikimbio yake.”

BUKAYO SAKA

Staa huyu wa Arsenal hakufikiria mara mbili alipoulizwa ni mchezaji gani anayemuangalia kama kiigizo chake, alisema ni Criatiano Ronaldo.

“Napenda akili yake, kila siku anataka kuwa bora, daima anafanya anafanya kazi kwa nguvu.”

Chanzo: Mwanaspoti