Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tchakei ashtukia jambo Ligi Kuu Bara

Marouf Tchakei Tchakei ashtukia jambo Ligi Kuu Bara

Thu, 5 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kiungo mshambuliaji wa Singida Big Stars, Marouf Tchakei ameshtukia kitu akisema msimu huu unaweza kuwa mgumu kama hawataongeza juhudi.

Tchakei ambaye ameanza kuitumikia timu hiyo msimu huu akitokea AS Vita ameonekana kuwa na kiwango bora baada ya kukifungia kikosi hicho mabao manne katika mechi mbili za Kombe la Shirikisho Afrika.

Nyota huyo amefunga mabao mawili katika mchezo wa raundi ya kwanza ya mtoano dhidi ya JKU ya Zanzibar wa Kombe la Shirikisho Afrika walioshinda 4-1 kisha akafunga mabao kama hayo dhidi ya Future ya Misri ambayo hata hivyo hayakutosha kuwavusha wakitolewa na Waarabu hao kwa jumla ya mabao 4-2.

Akizungumza Tchakei alisema ameumizwa timu hiyo kushindwa kuingia makundi kwani huo ulikuwa mpango wao.

Alisema baada ya Singida kutolewa sasa akili zao wanazihamishia kwenye Ligi Kuu Bara ambako nako mapema ushindani mkubwa umeanza.

“Imetuumiza kutolewa mapema kwenye Shirikisho, tuliona kama tulikuwa na nafasi kubwa ya kwenda angalau hatua ya makundi. Haikuwa hivyo, tunahitaji kubadilika haraka wakati tunarudi kwenye ligi ya ndani,” alisema Tchakei, raia wa Togo.

“Kwenye ligi nako ni ngumu. Hatujafanya vizuri kwenye mechi zetu za kwanza, ligi ni ngumu, lakini ni lazima tukabiliane na ugumu huo kuweza kuinusuru timu. Tuliikuta ikiwa na heshima kubwa ya kumaliza ndani ya nne bora.

“Huu msimu unaweza kuwa mgumu zaidi kama tusipoweka juhudi kwani hatuna kingine cha kupandisha thamani timu zaidi ya mechi za Ligi Kuu, ushindi unatakiwa sasa.”

Chanzo: Mwanaspoti