Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tchakei, Rupia sasa wameshindikana!

Rupia Mdk Tchakei, Rupia sasa wameshindikana!

Tue, 20 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Gari la Ihefu limewaka. Wakali hao wameendelea kutoa vichapo kwa wapinzani Ligi Kuu baada ya usajili mkubwa walioufanya kwenye dirisha dogo kwa kuwaleta mastaa kibao akiwemo mshambuliaji, Elvis Rupia na kiungo Marouf Tchakei ambao wameendelea kuibeba katika michezo ya Ligi Kuu.

Baada ya kuipa Ihefu ushindi 3-2 kwenye mchezo uliopita dhidi ya Mtibwa Sugar, nyota hao leo wameifungia mabao muhimu timu hiyo na kuiwezesha kuondoka na ushindi wa mabao 2-1 leo ugenini mbele ya Geita Gold kwenye Uwanja wa Nyankumbu, mjini Geita, ukiwa ni ushindi wa pili mfululizo.

Rupia aliitanguliza timu yake mapema katika dakika ya tano kwa kichwa akiunganisha krosi ya Marouf Tchakei, kabla ya Tchakei naye kuweka chuma cha pili katika dakika ya 12 akimalizia pasi ya Hernest Malonga na kwenda mapumziko wikiwa kifua mbele kwa mabao 2-0.

Baada ya kufunga leo katika mchezo huo ambao ulianza saa 8:00 mchana, Tchakei anafikisha bao lake la saba kwenye Ligi Kuu, huku Rupia akifikisha bao la tatu.

Geita Gold imekubali kichapo cha kwanza nyumbani kwenye Uwanja wa Nyankumbu tangu Septemba 30, 2023 ilipofungwa mabao 2-1 na KMC, ambapo baada ya hapo ilicheza mechi tano dimbani hapo bila kupoteza ikishinda tatu na sare mbili.

Ihefu imelipa kisasi cha kufungwa bao 1-0 katika mzunguko wa kwanza mchezo uliopigwa Agosti 15, 2023 kwenye Uwanja wa Highland Estates, Mbeya.

Beki wa Ihefu, Joash Onyango hakumaliza mchezo huo baada ya kufanyiwa mabadiliko katika dakika ya 17 akimpisha Lenny Kissu, huku Geita Gold nayo ikifanya mabadiliko ya mapema dakika ya 34 kwa kumtoa kiungo, Seleman Ibrahim na kuingia Jonathan Ulaya.

Kipindi cha pili Geita ilikuja juu ikisaka mabao ya kusawazisha, dakika ya 50 juhudi zao zililipa baada ya mshambuliaji wao, Tariq Seif Kiakala kuwafungia bao la kufutia machozi. Bao hilo ni la pili katika mechi mbili baada ya kuifungia bao pekee kwenye mchezo uliopita dhidi ya Azam wakipoteza kwa mabao 2-1.

Dakika 45 za kipindi cha pili, timu zote zilifanya mabadiliko, Ihefu wakiwapumzisha Emmanuel Lobota, Tchakei na Rupia na kuingia Morice Chukwu, Joseph Mahundi na Ismail Mgunda katika dakika ya 62 na 89, huku Geita Gold ikimpumzisha kiungo, Samwel Onditi na kuingia mshambuliaji, Ramadhan Kapera.

Kichapo cha leo ni cha tatu mfululizo kwa kocha wa Geita Gold, Denis Kitambi tangu aanze kuiongoza timu hiyo Desemba 20, mwaka jana, ambapo alifungwa 1-0 na Simba, 2-1 na Azam FC na leo kufungwa mabao 2-1 na Ihefu, huku akishinda 1-0 dhidi ya Singida Fountain Gate katika mchezo wake wa kwanza.

Ushindi wa leo ni wa tano kwa Ihefu msimu huu na unaifanya ifikishe pointi 19 na kupanda hadi nafasi ya 10 kwenye msimamo ikitoka nafasi ya 11. Baada ya kichapo cha leo ambacho ni cha nane msimu huu, Geita Gold imefikisha pointi 16 katika michezo 16 iliyocheza, ikishinda minne, sare nne na kufungwa minane.

Vikosi vilivyoanza:

Geita Gold: Sebusebu, Mwaita Gereza, Antony Mlingo, Geofrey Muha, Kelvin Yondani, Samuel Onditi, Seleman Ibrahim, Yusuph Dunia, Tariq Kiakala, Nasoro Saadun na Yusuph Mhilu.

Ihefu: Abubakar Khomeiny, Faria Odongo, Benson Mangolo, Joash Onyango, Benjamin Tanimu, Amande Momade, Hernest Malonga, Emmanuel Lobota, Elvis Rupia, Marouf Tchakei na Duke Abuya.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: