Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tatizo sio Guede, ni Yanga yenyewe!

Joseph Guede Yanga Joseph Guede

Mon, 19 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kelele zimeanza kuwa nyingi huko. Jina la Joseph Guede, straika mpya wa Yanga, likijadiliwa kila kona. Wapo wanaomponda wakisema 'Pale hakuna mchezaji'. Wengine wakisema 'Yanga imepigwa'. Kisa ni kushindwa kufunga bao lolote tangu aanze kuitumikia timu hiyo iliyomsajili kupitia dirisha dogo.

Yanga imeshacheza mechi tano hadi sasa za Ligi Kuu Bara tangu lilipofungwa dirisha dogo la usajili mnamo Januari 15. Ilianza kucheza na Kagera Sugar kule mjini Bukoba, Guede hakufunga, licha ya kuingia kipindi cha pili na kutumika kwa dakika 35 tu na mechi kuisha kwa suluhu.

Yanga ikarejea jijini Dar es Salaam kuialika Dodoma Jiji. Guede alianza kwenye mechi hiyo, ambayo Yanga ilishinda 1-0, lakini straika huyo kutoka Ivory Coast hakufunga bao lolote. Watu wakamvumilia na kumsubiri kumuona katika mechi dhidi ya Mashujaa iliyopigwa jijini Dar na timu hiyo kushinda tena mabao 2-1.

Katika mechi hii mwamba alianza tena kikosi cha kwanza, japo alitolewa kipindi cha pili, pia hakufunga, licha ya Yanga kushinda pia 2-1.

Mechi ya nne ya Yanga ilikuwa ugenini dhidi ya Tanzania Prisons ambapo aliingia kipindi cha pili na bado hakatoka kapa kabla ya juzi tena kwenye Uwanja wa Jamhuri, mjini Morogoro dhidi ya KMC, aliingia kipindi cha pili wakati timu hiyo ikishinda mabao 3-0.

Baadhi ya wadau hasa wale wa mitandaoni wameanza kumnyooshea kidole, wakimponda hana tofauti na Mghana Hafiz Konkoni aliyetemwa dirisha dogo baada ya kuchemsha kuvaa viatu vya Fiston Mayele aliyepo Pyramids ya Misri.

Wapo wanaosema Guede ni Gnamien Gislain Yikpe aliyechangamka. Lakini wapo wanaomkingia kifua kwamba, Guede ni bonge la mchezaji ila bado hajazoea mazingira na siku akianza kutupia wale wanaomponda ndio watakaompigia makofi kupongeza.

KOSA WALA SIO LAKE

Ni kweli Guede amebeba matumaini ya wanayanga kwenye eneo la ufungaji, lakini ukweli ni kwamba kosa sio lake kwani hata washambuliaji aliowakuta kikosini nao pia hawafungi.

Utabisha nini? Kennedy Musonda aliyekuwa akitumianiwa zaidi na Yanga baada ya Mayele kuondoka, hadi sasa katika Ligi Kuu Bara amefunga mabao matatu. Alianza kufunga dhidi ya JKT Tanzania, kisha akafunga Novemba 5 wakati Yanga iliifunga Simba mabao 5-1 na bao la mwisho kwa Mzambia huyo kufunga lilikuwa la Desemba 16 mwaka jana dhidi ya Mtibwa Sugar.

Hii ikiwa na maana huwezi kumtofautisha Guede na Musonda kwani tangu Januari imeanza Mzambia hajafunga kama ilivyo kwa Ivory Coast huyo.

Achana na Musonda, rejea kwa Clement Mzize straika mwingine wa Yanga aliyetabiriwa kuvaa viatu vya Mayele, licha ya kuanza msimu akiwa na kikosi hicho, amefunga mabao mawili tu hadi sasa.

Mzize alifunga bao la kwanza dhidi ya Coastal Union, mechi iliyopigwa Novemba 8 mwaka jana kabla ya wiki iliyopita kufunga bao la pili wakati Yanga ikishinda mabao 2-1 mbele ya Tanzania Prisons.

Hivyo, wale wanaomponda Guede bado wanapaswa kuangalia washambuliaji wengine wa timu hiyo wanavyosuasua katika ufungaji, licha ya kuizoea Ligi Kuu kwani wapo na timu hiyo tangu msimu uliopita.

TATIZO LIPO HAPA

Linapokuja dirisha dogo ni mara chache kumpata mchezaji wa kiwango cha juu wa kuanza kazi na moto, hivyo hata mabosi wa Kamati ya Usajili ya Yanga, ilichemsha kumleta Guede kipindi hiki.

Kushindwa kuwika kwa sasa kwa Guede, lawama zinapaswa kwenda kwa mtu aliyeamua kumtoa Hafiz Konkoni na kumleta Guede katika dirisha hili.

Kwa vile Yanga ilikuwa inafunga mabao kupitia kwa viungo washambuliaji iliyonayo kama Maxi Nzengeli, Pacome Zouzoua na Stephane Aziz Ki, huku ikiwa na kina Mzize, mabosi wa Yanga wangeamua kulikaushia tu dirisha dogo na kusubiri dirisha kubwa kusaka straika wa maana wa kuibeba timu kama ilivyofanya kwa kumbeba Mayele toka AS Vita.

Guede hata kama ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa wa kucheka na nyavu kama ilivyokuwa ikielezwa, ni ngumu kwa sasa kuonyesha makali kwa haraka kwa vile anacheza kwa presha kubwa, huku akiwa hajazoeana na wenzake, kwani ndio kwanza amejiunga na timu hiyo katikati ya mwezi uliopita baada ya kusajiliwa toka Ivory Coast.

Ni mara chache kwa wachezaji wanaotua katika klabu na kuanza na moto, mfano mdogo ni Donaldo Ngoma aliyesajiliwa misimu kadhaa iliyopita. Ni kama alivyoanza Jean Baleke aliyetua Msimbazi msimu uliopita kupitia dirisha dogo na kufanya mambo, japo safari hii katika dirisha kama hilo ametemwa na Simba.

Rekodi zinaonyesha kuwa, Guede na hata Konkoni sio mchezaji wa kwanza kusajiliwa Yanga na kushindwa kujipata mapema.

Hata Obrey Chirwa aliposajiliwa na Yanga June, 2016 kutoka FC Platinum ya Zimbabwe na kuanza kuicheza Ligi Kuu Agosti 20 mwaka hu, alikuja kufunga bao la kwanza baada ya kupita karibu miezi muiwili, kwani alitupia kwenye mechi dhidi ya Mtibwa Sugar, iliyopigwa Oktoba 12 mwaka huo wakati Yanga ikishinda mabao 3-1.

MFUMO WA GAMONDI

Mbali na hilo, pia huenda mfumo anaoutumia kocha Miguel Gamondi ya kutopenda kuwatumia mawinga ni jambo jingine linalokwamisha washambuliaji wa Yanga kufunga mabao na kazi yote kufanywa na viungo washambuliaji.

Gamondi, hategemei kabisa mawinga asilia wa kusaidia timu 'kumwaga maji' ndio maana kwenye dirisha dogo amemtema Jesus Moloko, pia amewakaushia kina Denis Nkane na hata Skudu Makudubela na badala yake kutegemea krosi za timu hiyo kupigwa na mabeki wa pembeni wanaotumika kwa sasa kama mawinga.

Yao Kouassi au Kibwana Shomary kwa upande wa kulia ama Nickson Kibabage na Joyce Lomalisa wa upande wa kushoto ndio wenye kazi ya kumimina krosi, ambao mara nyingi hupiga pasi za kurudisha mipira ndani (v-pass) zikiwa ni nyuma ya mastraika, lakini kwa kawaida huwa wanaingia kwenye sita wakisubiri mipira ili watupie nyavuni.

Ndio maana Aziz Ki ana mabao mengi kuliko Musonda. Pia haishangazi sana kuona Pacome na Mudathir Yahya wana mabao mengi kuliko Mzize, kwani wanakutana na pasi kwenye eneo sahihi na kupata nafasi ya kutupia na ndio maana Maxi, hata yeye ana mabao mengine kuliko Guede.

APEWE MUDA

Kwa vile Yanga yenyewe ilibugi kuleta mchezaji wa kutaka kuibeba kwenye dirisha dogo wakati ni nadra kutokea mchezaji akawaka haraka, ni vyema ikampa muda Guede ili kujipata kama ilivyowahi kufanya kwa Chirwa ambaye licha ya kukaa kwa miezi karibu miwili bila kufunga licha ya kuanzishwa kikosi cha kwanza, gari lilipowaka alimaliza na mabao 12, yakiwa ni mawili pungufu na walioibuka Wafungaji Bora wa msimu huo, Simon Msuva wa Yanga na Abdulrahman Mussa wa Ruvu Shooting waliofunga 14 kila mmoja kupitia mechi 30 za msimu nzima.

Huenda Guede siku atakapopatia pasiwedi ya kutupia nyavuni, mashabiki wanaomponda watasahau kila kitu, kama ambavyo walisahau kwa Chirwa na hata Musonda ambaye naye alipambana msimu uliopita hadi kufunga bao lake la kwanza kwenye ligi na kuwapa furaha wanayanga kwa mabao muhimu aliyofunga katika michuano ya kimataifa.

Lakini hata kama ataishia kuendelea kuwa 'bwana shamba' uwanjani kwa kuzurura bila mabao kama ilivyokuwa kwa Yikpe au Konkoni, bado lawama hazistahili kuwa kwake, bali kwa waliolazimisha kusajiliwa na kuletwa kipindi hiki, Yanga ikiwa na presha ya mechi za mashindano inayoshiriki ikiwamo Ligi ya Mabingwa Afrika, Ligi Kuu na ASFC.

Chanzo: Mwanaspoti