Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tatizo ni hii kamati

Chamaa Penatai Kiungo fundi wa Simba Clatous Chama

Fri, 11 Nov 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Kukosa msimamo endelevu na utaratibu unaoeleweka katika ufuatiliaji wa matukio pamoja na utoaji wa adhabu, zimetajwa kama sababu mbili zinazoitia doa Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB).

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwanaspoti jana, wadau wa soka nchini wameitaka kamati hiyo kujenga utamaduni wa kushughulikia kwa haraka matukio na makosa yanayofanyika kwenye ligi ili kuepuka kuumiza baadhi ya timu na wachezaji na kunufaisha wengine.

Mmoja wa viongozi wa klabu ya Simba ambaye hakupenda jina lake litajwe kwa kuhofia kukutana na kifungo, alisema uamuzi ambao umekuwa ukitolewa na kamati hiyo, umekuwa hautengenezi taswira nzuri kwa taasisi zinazosimamia mchezo wa mpira wa miguu nchini.

“Hatusikitiki mchezaji au wachezaji wetu kuadhibiwa pindi wanapofanya makosa lakini kinachotupa wasiwasi ni namna kamati inavyoshughulikia inaonekana kama inafanya kwa lengo la kuzikomoa timu fulani na kuzinufaisha timu fulani. Hii sio sawa na lazima waliangalie hilo.”

“Mfano, sisi tumepata taarifa za mchezaji wetu Clatous Chama kufungiwa wakati tayari timu imeshafika Singida tena siku mbili kabla ya mechi. Maana yake tunashindwa kumtumia, kocha anakuwa hajajiandaa kutafuta mbadala wake na wakati huo tumeshapata hasara ya kumsafirisha.

Lakini hao Singida Big Stars tunaocheza nao, kipa wao alimpiga mchezaji mwenzake na akakaa wiki karibia mbili bila kupewa adhabu na alicheza baadhi ya mechi jambo ambalo sio sawa,” alisema kiongozi huyo.

Wakili Norbert Mwaifwani alisema kuwa kamati inapaswa kushughulikia mashauri yake kwa wakati ili kuepuka kujichafua.

“Kuna ukakasi na mtu anaweza kwenda mbali zaidi na kuhisi kuna lengo la kukomoa watu. Inawezekana kuna ukiukwaji wa makusudi wa sheria unaofanywa na hiyo kamati au sheria yenyewe inayoongoza hiyo kamati ina mianya ambayo inawapa watu fursa ya kufanya hayo. Hii sio sawa na ikumbukwe kuwa haki inayocheleweshwa ni haki inayonyimwa,” alisema Wakili Mwaifwani.

Mchambuzi wa soka, Geoffrey Lea alisema; “Haki inayochelewa ni haki inayonyimwa.Mpira ni kiwanda kinachokua kuliko kitu chochote,kama nchi tunatakiwa kuendana na kasi ya maendeleo ya mchezo huu na sio kubaki nyuma,mamlaka zetu pia zinapaswa kutazama ugawaji wa adhabu kuendana na muda ambao hautatoa mwanya wa klabu kulalamikia uonevu.”

“Haiwezekani timu inajiandaa na mchezo halafu inakutana na taarifa kuwa mchezaji fulani hataweza kucheza kwa sababu ya adhabu kama ilivyokuwa kwa Simba wakiwa wanalalamika kuchelewa kwa adhabu ya Chama,” alisema Lea

Mwenyekiti wa zamani wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wakili Aloyce Komba alisema kuwa kamati inajitengenezea mazingira ya kulaumiwa na haitendi haki.

“Ninachoshauri, mtu akifanya kosa, adhabu itolewe kabla ya mchezo mwingine. Timu na wachezaji wasiviziwe. Taarifa itolewe mapema kwa timu kuwa kuna mchezaji mwenye adhabu. Lakini pia kosa likihusu mchezaji adhabu iende kwa mchezaji na sio lisubiriwe liathiri timu.”

“Mfano hao Chama (Clatous) na Aziz Ki wana mechi muhimu halafu unatoa ghafla taarifa za kufungiwa kwao maana yake unawaathiri kisaikolojia kwa mechi zilizo mbele yao,” alisema Wakili Komba.

Komba aliongeza,” Kanuni nyingi hazitendi haki. Mfano kanuni hiyo ya kulazimisha watu kusalimiana, inaingilia uhuru binafsi wa mchezaji. La msingi ni kwamba masuala ya msingi yanaenda na mpira unachezwa na ndio maana hata Fifa kwenye sheria 17 za soka hakuna sheria inayolazimisha watu wasalimiane. Sisi kwenye sheria tunasema haki inayotolewa kwa wakati ndio haki kamili. Toeni maamuzi ndani ya muda,” alisema Wakili Komba.

Mjumbe wa zamani wa kamati hiyo ya uendeshaji na usimamizi wa ligi, Jemedari Said alitaja mambo mawili ambayo yanaweza kuchangia kamati kuchelewa kutoa uamuzi.

‘Kamati hii ilipoanzishwa maana yake ilikuwa inatakiwa kutoa kukutana na kutoa uamuzi, ndani ya saa 72 baada ya mechi za mwisho za raundi husika na ndio maana ilipewa jina la Kamati ya Saa 72 sasa kamati inakumbana na changamoto ambazo zinasababisha ichelewe kukutana.”

Chanzo: Mwanaspoti