Kama sheria za masumbwi zingekuwa zinatumika kwenye soka, Yanga kwa sasa asingetakiwa kucheza na timu yoyote hapa nchini. Angetakiwa kupunguza kwanza uzito au wapinzani kuongeza uzito.
Najua msimu huu wamefungwa na Ihefu kule jijini Mbeya lakini sote tunajua moja ya sababu za kupoteza mechi ile ni kufanya mabadiliko makubwa kikosini.
Bado wanaweza kupoteza tena mechi nyingine lakini, hawa watu wako levo nyingine sana kwenye soka letu.
Ukitazama mechi yao dhidi ya Simba, unaona namna walivyo wakatili uwanjani. Hawa Yanga wana unyama mwingi sana. Moja ya maeneo waliyoimarika sana ni idara ya ulinzi.
Yule Joyce Lomalisa na Yao Kouassi wanafanya kazi nyingi sana za kijeshi pale nyuma.
Yanga walikuwa wanajichelewesha sana msimu uliopita kutomtumia sana Lomalisa. Huyu jamaa ana kitu pale nyuma. Ana uwezo mkubwa wa kukaba, kushambulia na kontroo za kutosha.
Yanga wako salama sana kule kushoto, kulia ndiyo balaa na nusu! Yao Kouassi kafanya watu wamsahau kabisa Djuma Shaban. Ni mtu na Nusu.
Ukifika uwanjani na haujui uwezo wake, unaweza ukahisi jamaa ni winga wa kulia.
Ana mwaga sana maji huyu kiumbe. Anaubonda mwingi kweli kweli.
Yule Ibrahimu Bacca, Bakari Mwamnyeto na Dickson Job ni kama wamezaliwa upya.
Hawa jamaa wana timu imara sana pale nyuma. Ni kama wamezaliwa upya. Kupitia mechi hii, nimegundua kuna matatizo mawili makubwa pale Simba na ambayo yasipoangaliwa kwa macho mawili yatazidi kuwafunua.
Moja ni katika eneo ambalo Jonas Mkude alicheza kwa muda mrefu sana. Kiungo wa chini changamoto bado ipo pale pale.
Unaweza usione tatizo wanapocheza na timu hizi za katikati lakini wakikutana na wakubwa mara nyingi sana wanatikisika. Yanga silaha yao kubwa siku hizi sio mawinga. Ni viungo watatu washambuliaji, Maxi Nzengeli, Pacome na Aziz KI. Huwezi kuwazuia kama huna viungo wawili mahiri pale chini.
Huwezi kuwazuia kama namba 10 wako hana uwezo wa kurudi chini kusaidia kukaba wakati timu yako imepoteza mpira. Hapa ndipo Simba anateseka sana na hasa kwenye mechi kubwa. Kanoute, Ngoma na Mzamiru ni wachezaji wazuri sana lakini sio kwa viungo wale wa Yanga.
Walau Mzamiru amekuwa kwenye ubora kwa muda mrefu sana. Kwa bahati mbaya hata ile mechi nayo Mzamiru hakuanza.
Simba wataenda mbele na kurudi nyuma, lakini wanahitaji viungo wawili wagumu pale katikati kuweza kuhimili ubora kama wa wale Yanga wa juzi. Kwa mianya waliokuwa wanaiacha, Simba angeweza kufungwa bao nyingi sana. Juzi ingeweza kuwa aibu ya karne. Kama zingeongezwa dakika 15 mbele, zingeweza kufika saba. Baada ya bao la tatu ni kama Simba walipoteza netiweki kabisa!
Sina tatizo na idara ya ushambuliaji ya Simba. Jean Baleke, Mosses Phiri, Saido Ntibanzonkiza na Clatous Chota Chama bado ni watu wa uhakika sana. Yule Kibu Dennis ni kama anazaliwa upya. Sioni shida yoyote kama kocha ataamua kuwatumia vizuri Phiri na Baleke vizuri. Pale kwenye kiungo na ulinzi nadhani kunahitajika mabadiliko makubwa.
Pili, pale kwenye ulinzi nako kuna shida. Tena kubwa. Kimtazamo ni kama Che Malone na Henock Inonga wanafanana kila kitu. Wote wanataka kuchezea mpira. Wote walinzi bishoo. Simuoni mgumu hata mmoja.
Hakuna anayemlinda mwenzie. Kwenye mechi za katikati unaweza usilione hilo lakini kwenye mechi kubwa, naona shida sana namna wanavyocheza. Kwa mechi kama ile ya juzi, labda alitakiwa kuanza mmoja na Kennedy Juma. Sidhani kama walitakiwa kuanza wote pamoja. Simba wangeweza hata kuanza na Inonga kwenye eneo la kiungo. Ngoma, Inonga na Mzamiru wangeweza kuanza wote kwenye kiungo huku Kennedy Juma na Che Malone wakianza kwenye ulinzi. Ingeweza kusaidia kuwadhibiti Aziz KI, Pacome na Nzengeli. Sio rahisi lakini ulihitajika mkakati mpya kuwazuia Yanga.
Simba wakicheza dhidi ya Al Ahly huwa wanaandaa mpango maalumu wa kucheza nao kwa kuwaheshimu lakini nadhani dhidi ya Yanga waliwachukulia poa. Ni kweli hata Manchester United, Arsenal nao hufungwa mabao mengi lakini Simba angeweza kuepuka aibu ya mabao mengi kama angewaheshimu wapinzani muda wote. Dakika 45 za kwanza, Simba alikuwa na nidhamu ya hali ya Juu. Ni kama kipindi cha pili Simba waliichukulia poa Yanga. Waliona ni kama wanawamudu na hapo ndipo maafa yalipoanzia.
Kipindi cha pili ni kama Fabrice Ngoma, Mohammed Hussein na Shomari Kapombe wote walianza kupanda juu. Taratibu wakawa wanakwenda juu ya mstari wa katikati na ndiyo maana mabao mengi wamefungwa baada tu ya wao kupoteza mpira walipokuwa wanashambulia. Kwa sasa kwenye ukanda wetu wa CECAFA, Yanga ndiyo timu bora. Unapocheza nao unapaswa kuheshimu sana ubora wao. Unapaswa kuwa na mpango maalumu kabisa kama ambavyo unacheza na Al Ahly au Mamelod Sundowns.
Tukubali tukatae, Yanga wako kwenye dunia yao kwa sasa. Ni muda wa Simba kupata funzo kutokana na mechi hiyo lakini ni lazima waisahau ili wasitoke mchezoni mapema. Kipigo kikubwa kikiwasumbua kwa muda mrefu, watajikuta wanapoteza mechi nyingine. Bado naamini Simba wanaweza kufungwa tena na Yanga lakini wakashinda ubingwa mwisho wa msimu. Ubingwa hauji kwa kuwafunga Yanga tu. Hongereni sana Wananchi, naona mmeshajipata.