Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tatizo kuwafungia waamuzi hakujatoa majibu

Ahmed Arajiga Ahmed Arajiga

Fri, 14 Apr 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Vilio kwa waamuzi vimekuwa vingi sana kwenye soka la Tanzania pindi wanapokuwa kwenye majukumu yao, huku wengi wakilalamikia maslahi.

Malalamiko kwa wadau wa soka ni namna waamuzi wanavyoingia matatani hasa wanapochezesha michezo inayozihusu Simba na Yanga.

Kwa miaka ya hivi karibuni waamuzi wengi walisimamishwa au kufungiwa ni kutokana na kuboronga katika mchezo mmoja wapo wa vigogo hawa wa soka nchini.

“Hakuna mtu anayependa kuona anafanya kazi yake vibaya na kulaumiwa kila wakati na ukiona hivyo, basi ujue kuna shida mahali kama sio mwamuzi basi mfumo mzima una matatizo.

“Kila mmoja anapenda kufanya kazi yake akiifurahia, mazingira rafiki na hata ikibidi kupongezwa unapofanya vizuri lakini kila kukicha ukiona huyu analalamika hivi yule vile hapo kunatakiwa kujitathimini,” anasema mmoja wa waamuzi wa Ligi Kuu.

Leo makala haya yanaangalia mambo yanayowakumba waamuzi kwa kushirikiana na waamuzi, viongozi wa kamati za waamuzi, wakufunzi na waamuzi walistaafu juu ya mustakabali wa tasnia hii.

VIWANGO VIPI

Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi, Nassor Amduni anasema: “Kwa sasa siwezi kufanya tathmini ya kiwango cha waamuzi kama kimeongezeka au kimepungua lakini msimu ukimalizika naweza kufanya hivyo kwa kuangalia ripoti mbalimbali.”

Shomari Lawi anasema kwa tathmni ya haraka viwango vya waamuzi vimeongezeka tofauti na mataifa mengine kwasababu wanatumia vifaa maalumu tofauti na Tanzania.

“Mfano waamuzi wa mataifa ya mbele wanavaa vifaa mkononi ili kurahisisha mawasiliano jambo ambalo kwetu hatuna, hivyo tunachezesha kwenye mazingira ya aina hiyo na bado tunafanya vyema, hivyo tukiwezeshwa vifaa tutakuwa bora zaidi.”

Abdallah Kambuzi anasema viwango vya waamuzi vipo wastani sababu hakuna mwamuzi ambaye amekuwa mfano kwa wengine katika kupiga hatua kwenye tasnia hiyo, hivyo bado tunatembea palepale kwa miaka yote.

Mkufunzi wa Waamuzi, Soud Abdi anasema hali ya waamuzi imebadilika sana japokuwa kuna wakati unapita upepo mbaya lakini kwa sasa kuna mabadiliko makubwa.

“Tukisimamia ukweli miaka ya nyuma na hali ilivyo sasa kuna mabadiliko makubwa nadhani kila mmoja anaweza akawa na jibu kama viwango vya waamuzi vipo kwenye levo gani.

“Sio kwamba makosa hakuna au yameisha hapana siwezi sema hivyo ila kuna unafuu fulani ambao tunauona hata kelele mtaani zimepungua,” anasema Abdi aliwahi kuwa mwenyekiti wa kamati ya waamuzi.

MADARAJA YA WAAMUZI

Mafunzo ya awali wale wanaotoka darasani 3P yaani Daraja la 3 ambao wengi ni kwaajili ya Ligi Daraja la Tatu ngazi za mikoa, Daraja la Pili kwaajili ya First League na Daraja la Kwanza. Hivyo waamuzi wote wa Ligi Kuu ni wale wa Daraja la Kwanza.

“Sasa hawa daraja la Kwanza kuna wale wanaochezesha Championship na wale wa Ligi Kuu ambao wanachanganywa na wale wa Fifa kwaajili ya Ligi Kuu, hivyo kutokana na uwingi wao utakuta wengine wapo hadi First League lakini anasifa sawa na yule wa Ligi Kuu,” anasema mmoja wa wakufunzi ambaye hakutaka kutajwa jina lake.

Vipi kuna mafunzo tofauti na wale waamuzi wa pembeni? ‘Line One na Line Two’. Jibu ni hapana kwani wote wanasoma masomo sawa lakini mwamuzi anajiangalia wapi anapamudu zaidi kama ilivyo kwa mwandishi wa habari mwingine anaandika habari za michezo mwingine habari za kijamii.

“Kozi ni moja lakini unapomaliza mtu anaamua kujikita sehemu moja ndio utaona utofauti wa mtu, hivyo hadi mtu anakuwa ‘promoted’ na wakufunzi kufikia levo ya Fifa lakini huwezi kufika Fifa bila kupita ‘Elite’ yaani ni ‘Clime’ ya daraja la Kwanza.

Abdi anasema kumwandaa mwamuzi hadi kuchezesha Ligi Kuu haipungui miaka mitano ili kuwa katika kiwango kinachotakiwa ndio maana hawapendi kuona wakishushwa daraja sababu kila mmoja wanaamini anafanya makosa

HUKO KIMATAIFA

Waamuzi kuchezesha mashindano ya kimataifa kama vile Afcon na Chan ni suala la mchakato ili kufika hapo lazima achezeshe michuano ya U-17, U-20 ndipo baadaye anaweza kuteuliwa kuchezesha michuano ya wakubwa. Kila ngazi ina miaka miwili ndio unakwenda ngazi nyingine, Frank Komba tayari ameshachezesha Chan.

Waamuzi wetu wamechezesha michezo mingi ya Caf na Fifa na michezo mingi ni ile ya kuwania kufuzu lakini kuchezesha fainali kubwa kama hiyo, marefa wetu wengi wanaonekana kupungua uwezo kwa kuzidiwa na wenzao.

Caf hufanya tathmini pia kwa mechi wanazochezesha waamuzi, ufuatiliaji wa sheria za uamuzi pamoja na maoni ya wadau mbalimbali baada ya mechi, lugha ya mawasiliano ni miongoni mwa changamoto ambapo Kiingereza na Kifaransa ndizo hutumika zaidi

Abdallah Kambuzi anasema tunashindwa kwenda mbele sababu ya maandalizi yetu kwa waamuzi sio mazuri lakini Tanzania bado hatujawekeza ili siku moja tupeperushe bendera kimataifa.

TUNAJIKONGOJA

Frank Komba msimu huu ameteuliwa katika orodha ya waamuzi kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Arfika kati ya Mamelodi Sundowns na Coton Sport na ndiye mwamuzi anayeipeperusha vyema bendera ya Tanzania.

Oktoba, 2022 waamuzi wanne wa Tanzania Elly Sasii, Frank Komba, Mohamed Mkono na Ramadhani Kayoko waliteuliwa na Caf kuchezesha mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika kati ya St. Michel (Shelisheli) na Motema Pembe (DR Congo).

Mwaka 2019 waamuzi hao pia waliteuliwa kusimamia mechi za Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho, Sasii alisimama katikati mchezo wa Ligi ya Mabingwa kati ya Aigle Noir ya Burundi na Gor Mahia ya Kenya uliochezwa Uwanja wa Prince Louis Rwagasore, Burundi Agosti 11,2019.

Sasii alisaidiana na mwamuzi msaidizi, Frank Komba, Ferdinand Chacha, huku mwamuzi wa Akiba alikuwa Emmanuel Mwandembwa wakati, Ahmed Mgoyi alikuwa kamishna wa mchezo wa marudiano kati ya timu hizo.

Mwamuzi Ahmed Aragija mwaka jana aliteuliwa na Caf kuchezesha michezo ya Cecafa U17 iliyofanyika Ethiopia na pia aliteuliwa katika mchezo kati ya ASAS Telcom ya Djibout na AS Kigali ya Rwanda kwenye kombe la Shirikisho.

Pia, Komba mwaka juzi alikuwa kwenye orodha ya waamuzi walioteuliwa kuchezesha Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 20, (Afcon U20) zilizofanyika nchini Mauritania.

Arajiga tayari ameteuliwa na Caf katika orodha ya awali ya waamuzi watakaochezesha Afcon U17 mwaka huu yatakayofanyika huko nchini Algeria.

SHERIA YA 11 MAJANGA

Sheria hii inaelezea mambo mengi kuhusiana na mchezaji kuotea ‘offside’. Mchezaji atahesabika kuwa amezidi kama atalikaribia goli la timu pinzani zaidi ya mpira na beki wa mwisho lakini ni pale tu atakapokuwa kwenye nafasi hiyo akiwa upande wa nusu ya timu pinzani uwanjani. Sheria inasema kama mchezaji amezidi na mpira ukapelekwa kwake na ukaguswa na mchezaji wa timu yake, anaweza kuamua kuuacha kana kwamba hayupo mchezoni ili mwenzake aendelee kuucheza.

Lakini inaeleza sio kosa endapo mchezaji atapokea mpira moja kwa moja kutokana na pigo la goli, pigo la kona au mpira wa kurusha.

Mkufunzi, Soud Abdi anasema anaweza akakubali Sheria ya 11 ndio ngumu kwa sababu inahitaji umakini sana katika utekerezaji wake.

Shomari Lawi anasema hili ni janga kubwa sio Tanzania pekee bali ulimwenguni kote sababu ya mazingira ya mchezo unavyokuwa lakini sio kwamba ni sheria ngumu bali kuitekeleza.

“Mchezo ambao ulikuwa mgumu kwangu ulikuwa kati ya Mbeya City na Yanga Uwanja wa Sokoine, Mbeya msimu wa mwaka 2018/19 ambapo mchezaji alitolewa lakini akarudi tena uwanjani.

Kambuzi anasema sheria ya ‘off side’ inatakiwa kuisoma kila wakati na kufanya kwa vitendo sababu inatazamwa tofauti na watu wa soka. Abdi anasema mataifa mengine waamuzi wananufaika kwa sababu wanakuwa wamepiga hatua katika teknolojia na kuwa na vifaa vingi vinavyowasaidi kugundua jambo tofauti na mataifa kama yetu

Chanzo: Mwanaspoti