Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tatizo Simba sio Try Again, ni fedha tu!

Mo X Try Again Ll Tatizo Simba sio Try Again, ni fedha tu!

Mon, 10 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Nimeona mitandaoni taarifa za kujiuzulu kwa viongozi wa Simba upande wa mwekezaji, Mohamed Dewji.

Zipo taarifa Wajumbe wote akiwemo Mwenyekiti wa Bodi, Salim Abdallah Muhene ‘Try Again’ naye amejiuzulu. Sifahamu sana kuhusu ukweli wa hili, lakini ukweli ni kuna mabadiliko makubwa yanakuja ndani ya klabu hiyo kongwe nchini.

Ubaya ni Katiba ya Simba inatoa nafasi ya Mwekezaji kuteua Wajumbe na Mwenyekiti wake, lakini haimpi nafasi ya kuwatoa kama haridhishwi na ufanisi wao.

Hii ndiyo sababu Mo Dewji ameshindwa kuwatoa Wajumbe aliowateua mwenyewe licha ya kutoridhishwa na ufanisi wao kwa muda mrefu. Anawatoaje? Lilikuwa ni swali gumu kwake.

Sasa Simba imemaliza nafasi ya tatu katika Ligi Kuu Bara. Imefungwa mabao 5-1 na Yanga katika ligi hadi wakapika supu na kuinywa kwa chapati pale Jangwani. Pia imeng’oka mapema katika Kombe la Shirikisho. Ni fedheha kubwa. Kwa nini wamefika huko? Wanajua wenyewe.

Huu ulikuwa muda sahihi kwa Mo Dewji kuwawajibisha viongozi wake. Yeye ndiye mwekezaji. Ndiye bilionea wa klabu hiyo. Simba ikifanya vibaya anasemwa zaidi yeye kuliko mtu yeyote wa Msimbazi.

Malengo aliyosema ya Simba kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika hayaonekani. Utafika fainali na hawa kina Pa Omary Jobe? Sio kweli, ni utani.

Yanga imepindua meza kibabe. Inatawala soka la Tanzania sasa chini ya Rais Injinia Hersi Said. Kiongozi mwenye weledi na maono.

Simba wanafanya Nini? Wapo wapo tu. Unakubali wameshindwa kushindana na Yanga, ila pia wameshindwa na Azam FC.

Mwaka wa pili sasa Azam FC inacheza fainali ya Kombe la Shirikisho na Yanga. Iko =wapi Simba? Haijulikani. Mwaka jana ilitolewa na Azam FC na mwaka huu imetolewa na Mashujaa ya Kigoma. Timu iliyoshiriki Ligi Kuu kwa mara ya kwanza na iliyokuwa ikijitafuta katika ligi hadi kujiokoa kushuka daraja.

Yaani kwa kifupi ni jambo la aibu. Timu kama Simba inatolewaje na Mashujaa ambayo wakati huu ilikuwa inapambana kujinasua na janga la kushuka daraja? Ni kweli hii sio mara ya kwanza kwa Mashujaa kuitesa Simba. Ilishaitoa katika michuano hiyo ikiwa ipo Daraja la Kwanza, ila kwa levo za timu hizo inashangaza.

Hata hivyo, mambo haya ya kuudhi ndio yamemfanya Mo Dewji kurudi kwa kishindo na kutaka kuwatoa wawakilishi wote wa upande wake. Ana haki. Watu aliowateua wamemwangusha.

Ndio ipo hivyo duniani kote. Ukishindwa kufanya vyema, mwenye timu yake lazima akutoe.

Hata hivyo, kwa uchunguzi wa Mtu wa Mpira umebaini kuwa shida ya Simba ni zaidi ya hawa kina Try Again na wenzake. Shida ni kubwa zaidi! Shida ni pesa.

Kwa kipindi kirefu Simba imekuwa na vyanzo vizuri vya mapato kukidhi sehemu ya bajeti yake. Ni kweli fedha zipo ila hazitoshi kushindana na Yanga na Azam FC.

Hawa kina Jobe, Freddy Michael na Babacar Sarr hawajasajiliwa bahati mbaya. Ni uhaba wa fedha pale Msimbazi. Kuna fedha hazitoki kwa wakati.

Huyo Try Again watu wanamsema leo kwa msimu alikuwa anatumia zaidi ya Sh 1Bilioni kutoka katika mfuko wake kusaidia Simba. Kwa nini? Kwa sababu fedha hazitoshi. Soka bila ya fedha ni manjegeka.

Huwezi kupata wachezaji wa viwango vya kina Yao Kouassi, Pacome Zouzoua, Steophane Aziz KI au kipa Diarra Djigui. Unabisha? Waulize Yanga kipindi ikitembelea chaki, ndio utakuwa. Iliwaleta kina Kindoki Bongo!

Miaka mitatu nyuma wakati Simba inatawala soka la Tanzania gharama zilikuwa chini. Mchezaji mzuri angepatikana kwa Dola 100,000 (Laki Moja). Kwa sasa mchezaji mzuri si chini ya Dola 200,000 (Laki Mbili).

Kwa muktadha huo lazima Mwekezaji atoe fedha zaidi. Yawezekana aliona wanataka fedha nyingi na akapunguza imani kwao ila ukweli ni kwamba kila kitu sasa kimepanda.

Makocha wamepanda bei. Wachezaji wamepanda bei. Gharama za mechi zimepanda. Kila kitu kimepanda. Unawezaje kushindana? Ni kutoa fedha zaidi.

Yanga wanaweza kwa sababu wanatoka fedha. Msimu uliopita pale Yanga GSM alitoa karibu Bilioni 5. Mo alitoa kiasi gani? Anajua mwenyewe.

Ila ukweli ni kwamba hata kama Mo Dewji anabadili Bodi ya Wakurugenzi, Lazima akubali kuwa tatizo kubwa ni pesa. Atoe pesa timu itaweza kushindana.

Hivyo tu!

Chanzo: Mwanaspoti