‘Hakuna kukata tamaa’ ndivyo anavyoanza kusimulia maisha yake ya soka kiungo mshambuliaji wa Polisi Tanzania, Tariq Simba.
Mkasa mzima umejaa masikitiko kwa maana ya nyota huyo ambaye amepitia panda shuka nyingi kwenye soka, anadai kuna muda ilifikia akakata tamaa kabisa, lakini alipogundua maisha ni safari, aliamua kuamka tena na kuanza mwanzo huku akiitaja timu ya Tunduru Korosho kama mkombozi kwake.
Polisi Tanzania inakamata nafasi ya 16 (ya mwisho) kwenye msimamo wa Ligi Kuu na alama 19 baada ya michezo 25 hadi sasa, hata hivyo kwa Tariq ambaye alisaini nao mika miwili anasema bado hawajakata tamaa na wanapambana kuhakikisha haishiki daraja.
Mwanaspoti lilifanya naye mahojiano na kutiririka mengi ikiwamo alivyodhulumiwa pesa zake za usajili na mshahara wa mwaka mzima na bosi mmoja mkoani Kilimanjaro. Twende pamoja...
ALIKOANZIA SOKA, MPIGADEBE AMWIBUA
Anamtaja kwa jina moja Levocatus ndiye aliyegundua kipaji chake mkoani Songea na kujiunga na timu ya mtaani ya wapigadebe ya Daladala mwaka 2008-2009 akicheza soka la vijana kabla ya kupata timu za ushindani akianza na Ruvuma Town Small Boys mwaka 2014 na ilikuwa ikishiriki Ligi Daraja la Pili ‘First League’ sasa na alisajiliwa na timu hiyo baana ya kumwona akiwa na timu hiyo ya mtaani ‘Daladala’ iliyomilikiwa na matingo na madereva wa daladala mkoani humo.
Akiwa na Ruvuma Town Small Boyzs alishiriki ligi hiyo wakipangiwa kituo cha Mbozi pamoja na timu za Panone (Kilimanjaro), Njombe Mji (Njombe), Volcano (Katavi) na nyingine ameisahau jina ya Mbozi.
“Niliibuka mchezaji bora kwenye michuano hiyo na Panone walinifuata na kunisajili kwenda kucheza Ligi Daraja la Kwanza (sasa Championship) mwaka 2015,” anasema kiungo huyo.
ALIVYODHULIMIWA
Anasema moja ya mambo yaliyowahi kumkatisha tamaa ya kucheza soka ni kudhulumiwa pesa za usajili na mshahara wake wa mwaka zmima. Hiyo ilikuwa mwaka 2016 na baada ya hapo hakuona haja ya kuendelea na soka na kuamua kurudi mjini Songea kupumzika.
“Timu (anaitaja), walinifuata nyumbani Songea wakanisajili na kunipa Sh500,000 na kuniambia fedha nyingine ya usajili watanimalizia kama Sh3 milioni, pia watanipa mshahara wa Sh250,000,” anasema kwa uchungu na kuongeza;
“Nilikuwa napewa mshahara wa Sh100,000 kwa mwezi na sikujua sababu. Kumbe bosi alitoa hela zangu zote za usajili milioni 3 na mshahara wa 250,000 lakini hazikuwa zinafika zote kwangu, kuna mtu alikuwa anazila.
“Nilifuatilia kwa kuuliza viongozi lakini walinijibu nitalipwa tu. Sikujali kwani nilichotaka ni kutimiza ndoto yangu ya kufanikiwa kisoka kwa kuonekana,” anasema na kuongeza baada ya msimu bosi aliwauliza kama anadai chochote na ndipo alipofunguka kuhusu haki yake hiyo;
“Nilimwambia mimi nadai. Alishangaa sana na kuniambia sidai chochote na hela zako nilitoa zote, kabla ya kufungua kompyuta yake na kunionyesha kumbukumbu zote za malipo yalivyofanyika.”
AIBUKIA NJOMBE MJI, MAJIMAJI YAMWONA
Anasema baada ya sakata hilo, aliamua kukaa nje msimu mzima mwaka 2016 hadi 2017 aliamua kujiunga na Njombe Mji chini ya Kocha Aisack Migodela.
Hata hivyo, anasema baada ya mkataba kumalizika alirudi nyumbani Songea na kujiunga na Majimaji iliyokuwa ikishiriki Ligi Kuu Bara akijiunga na Iddi Kipwagwile, Peter Mapunda, Mpoki Mwakinyuki, Amani Simba na Fred Mbuna na mchezo wake wa kwanza ilikuwa dhidi ya Simba Jijini Dar es Salaam.
“Niliingia nikiwa mdogo kabisa ni mchezo ambao hauwezi kufutika katika kumbukumbu zangu kwani nilikuwa natamani sana kucheza ligi kuu,” anasema kiungo huyo.
KALLY ONGALA NOMA
Kati ya makocha waliopa nafasi ya kucheza ni Kalimangonga ‘Kally’ Ongala aliyekuwa akiifundisha Majimaji.
“Sikuwa nikipata nafasi ya kucheza na viongozi walitaka kuniacha baada ya mzunguko wa kwanza mimi na Kipagwile, hata hivyo, Kally alikuwa akitupa nafasi ya kucheza kwa dakika 10 au 5 za mwisho kuonyesha uwezo wetu.
“Tulienda kucheza na Stand United, Mpoki aliumia na hivyo Kally akanipanga namba tatu. Nakumbuka nilicheza vizuri sana ingawa wakati huo nilikuwa nacheza nafasi ya ushambuliaji,” anasema na kuongeza anavutiwa na uchezaji wa marehemu Jabba (Ibrahim Rajabu) huku akimtaja Mzamiru Yassin mavitu anayofanya uwanjani ni kama anawajibu wengi wanaomsema.
AIPANDISHA NAMUNGO, AUMIA
Panda shuka za maisha yake ay soka zinatua Namungo FC na anasema alikuwa mmoja wa wachezaji walioipandisha Ligi Daraja la Kwanza mwaka 2018 chini ya Kocha Furgence Novatus.
Hata hivyo, mwaka 2019 alipata changamoto ya kufiwa na Mama yake na kuumia wakati akiitumikia timu hiyo pamoja na majeraha yaliyomweka nje kwa muda.
“Namshukuru Mwenyekiti wa Namungo Hassan Zidadu amenitoa mbali sana alikuwa anaamini sana katika kipaji changu na nilipoumia alinitibu kwa asilimia 100 na kunishauri nitafute timu ya kuchezea na yeye atanipa fedha ya usajili.
“Alinipa Sh3.5 milioni nikajiunga na JKT Mlale ya kule kwetu Songea iliyokuwa chini ya Kocha Maka Mwalwisi ambaye nilikuwa naye Panoni.
MAJERAHA YAMTIBULIA
Anasema akiwa na JKT Mlale aliumia kwenye mchezo wa Play Off Daraja la Kwanza dhidi ya Geita Gold jeraha ambalo lilikuwa baya sana.
“Dakika ya 25 ya mchezo beki wa Geita Antony Matogolo aliniumiza vibaya. Nilikata tamaa ya kupona na kuendelea kucheza lakini Iddi Kipagwile ambaye alikuwa Azam FC kipindi hicho, aliniambia nisikate tamaa.”
“Nilimwambia naacha soka, hakupenda, akaniambia niende Dar es salaam kwa ajili ya matibabu na kuna daktari anamjua atanisaidia. Daktari anaitwa Gilbet alikuwa pia daktari wa timu ya Taifa, ofisi zake zipo Mikocheni.
“Alinisaidia nikatibiwa goti na nikapona vizuri, wakati narudi Songea nilikuwa na Iddi, tukiwa Tunduru, tukakutana na washkaji zetu fulani wakasema wana timu yao inaitwa Tunduru Korosho,” anasema na kuongeza, hakufikiria mara mbili, aliamua kujiunga nao huku akiendelea kutafuta timu ya Ligi Kuu na timu hiyo ilipangwa kituo cha Kigoma Ligi Daraja la Pili na aliibuka mchezaji bora wa mashindano mwaka 2020 na ikawa njia ya kurudi Ligi Kuu Bara.
COASTAL YAMKATAA, ATUA BIASHARA
Baada ya michuano hiyo Kigoma, anasema alirudi Songea na akiwa huko alipigiwa simu na Mwenyekiti wa Coastal Union, Steven Mguto.
“Nilienda lakini hawakunikubali, nikapokea simu ya Mwenyekiti wa Biashara United, Seleman Mataso ambaye tulimalizana nae Jijini Dar es salaam na rasmi nikajiunga na Biashara msimu 2020-2021.”
BARAZA AMBADILISHA NAMBA
Anasema akiwa Biashara United alicheza nafasi ya mshambuliaji lakini kutokana na majeruhi waliokuwapo kwenye mafasi ya kiungo, alihamishiwa nafasi hiyo na akaanza kucheza kwenye mchezo dhidi ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga;
“Ally Kombo na Omary Banda wote hawa walikuwa wakicheza nafasi ya kiungo. Waliumia. Tukiwa tunaenda Arusha kucheza na Polisi Tanzania, Kocha Francis Baraza akaniambia nitacheza nafasi ya kiungo, nikacheza pamoja na Ramadhan Chombo na Benard Kauswa.”
“Baada ya mechi hiyo kocha aliniamini akaniambia nitaenda kuanza katika mechi dhidi ya Yanga nilicheza vizuri na ndio mwanzo wa mimi kucheza nafasi ya kiungo,” anasema kiungo huyo ambaye ni mtoto wa nyota wa zamani wa CDA ya Dodoma, Mukhtari Simba na anasema waliomwona baba yake akicheza enzi zake, yeye hamfikii hata robo.
Anasema Biashara ilipata nafasi ya kushiriki mashindano ya kimataifa lakini Baraza aliondoka na ndio ukawa mwisho wake kuichezea Biashara United na sasa anapambana kuhakikisha Polisi Tanzania inasalia Ligi Kuu msimu ujao.