Mwenyekiti wa zamani wa Yanga, Tarimba Abbas amezitaka Simba na Yanga kusahau matokeo yaliyopita na kuwekeza nguvu kwenye mechi za wikiendi hii dhidi ya Raja Casablanca na TP Mazembe ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kutoboa kwenye hatua ya makundi.
Tarimba ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya SportPesa, alisema kwa aina ya vikosi ilivyonavyo wawakilisho wa wa nchi katika Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika anaziona zikitoboa kwenda robo fainali kwa msimu huu.
Simba ipo Kundi C ya Ligi ya Mabingwa itaialika Raja ya Morocco Jumamosi hii, wakati Yanga inayoshiriki Kombe la Shirikisho ikiwa Kundi D, itashuka uwanjani Jumapili dhidi ya Mazembe kutoka DR Congo, mechi zote zikipigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Akizungumza Tarimba alisema matokeo mabaya waliyoyapata katika mechi za kwanza ugenini yasiziondoe timu hizo kwenye mstari, kwani bado zina nafasi ya kufanya vizuri na zinatakiwa kutumia vyema mechi hizo za nyumbani.
“Simba inacheza dhidi ya Raja Casablanca, ni timu nzuri, lakini hata wao ni wazuri na ina rekodi nzuri Kwa Mkapa, hasa mashindano ya kimataifa kwa miaka ya karibuni. Pia ina kikosi kizuri cha wachezaji wazoefu," alisema Tarimba na kuongeza;
"Inatakiwa kusahau matokeo yaliyopita na kuwekeza nguvu kwa mchezo huo na kutumia vyema motisha ya Rais Samia Suluhu kwa kufunga mabao mengi.”
Kwa upande wa Yanga, Tarimba alisema ina nafasi ya kufanya vizuri dhidi ya Mazembe kwenye uwanja wao wa nyumbani, akisisitiza hata wao wana kikosi kilichokamilika kuanzia benchi la ufundi, hivyo jitihada na kuamini katika kupambania pointi tatu ndio iwe silaha kubwa kwao.
“Yanga nayo ilipoteza ugenini kwa kufungwa 2-0, hii haina maana kwamba haiwezi tena, ijiamini na kuingia uwanjani ikijua kuna watu nyuma yao wanaotaka kuona wanafanya vizuri," alisema Tarimba na kuongeza;
“Kubwa kwao ni kuhakikisha kila mmoja inashinda mechi za nyumbani na ikitokea wakapata nafasi ugenini pia wasiache kufanya vizuri lakini matumizi ya uwanja wa nyumbani kufanya vizuri wayape kipaumbele.”
Tarimba alisema anazitakia kila la kheri timu zote mbili akizitaka kujiandaa vizuri na kutumia nafasi waliyoipata kuiwakilisha nchi vizuri kwa kutinga hatua inayofuata kwenye mashindano hayo.