Mkurugenzi Mtendaji wa SportPesa ambao ni wadhamini wa Klabu ya Yanga, Tarimba Gulam Abbas amesema kuwa mafanikio ya Yanga wametengeneza chuki kwa baadhi ya watu ambao wanaitakia mabaya klabu yao hiyo.
Tarimba ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi ya wadhamini ya Yanga, amesema hayo wakati akitoa hundi kwa klabu ya Yanga kama bonasi kutokana na klabu hiyo kumaliza ligi wakiwa mabingwa na kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa.
“Kwa kuwa tumefikia malengo yetu na Yanga imefanikiwa kuleta ushindani mkubwa, ninaona mwakani mpira wa Tanzania utakuwa mgumu sana. Mafanikio ya Yanga yanaweza kuwa yameleta furaha sana kwa Wanayanga lakini yameleta chuki kwa wadau wengine.
“Chuki hizo zinaweza kuanzia kwa watru kujaribu kutengeneza timu zao kuzifanya nazo ziwe kali, watajaribu sana. Lakini wapo ambao watatafuta wadau wengine kutafuta njia ya kuisumbua Yanga kwa namna moja ama nyingine, ninaomba tuendelee kusimama tukiwa thabiti sana wala tusishituke na kelele za watu ambao wanajaribu kuvuruga uongozi na wachezaji wetu.
“Sasa hivi kwenye mitandao kila mtu amekuwa msemaji wa Yanga, wanazungumzia mchezaji huyu anaondoka, wanasajili huyu mara yule, ningeomba Wanayanga wasikilize viongozi wao wala si watu wengine. Yanga tungependa kutawala soka la Tanzania, Afrika Mshariki na Afrika nzima,” amesema Tarimba.