Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzia: Tshabalala afariki Dunia kwa majeruhi baada ya kupigwa risasi

Tshabalala Screamer Stanley 'Screamer' Tshabalala.

Fri, 12 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Klabu ya Orlando Pirates ya nchini Afrika Kusini wametangaza kifo cha ofisa wao mwandamizi Stanley 'Screamer' Tshabalala.

Kocha huyo wa zamani wa Timu ya Taifa ya Afrika Kusini maarufu kama Bafana Bafana alilazwa hospitali hivi karibuni baada ya kupigwa risasi wakati akiwa katika mapumziko kwenye makazi yake mwezi Machi mwaka huu.

Mzee huyo mwenye umri wa miaka 75 alikuwa akiendelea vizuri na matibabu madogo madogo nyumbani kwake lakini baadaye alizidiwa na kukimbizwa hospitali ambapo jana Alhamisi mchana aliaga dunia.

"Familia ya Tshabalala na Orlando Pirates kwa masikitiko makubwa inatangaza kifo cha mpendwa wetu Stanley Tshabalala mchana wa leo (jana) hospitalini," ilisema taarifa ya klabu hiyo.

"Bra Stan, kama alivyotajwa kwa upendo na kila mtu, alifariki kutokana na majeraha aliyoyapata alipopigwa risasi mwezi Machi mwaka huu.

“Familia ya Tshabalala na Orlando Pirates itatoa taratibu zingine za mazishi na maombolezo ya msiba huo. Tunawaomba umma uwe na subira, tutatoa maelekezo yote kadri mipango inavoendelea."

Tshabalala, aliyezaliwa mwaka 1949, alikuwa gwiji ndani na nje ya uwanja. Mwanachama na mwanzilishi wa Klabu ambayo ni wapinzani wa Orlando Pirates, Kaizer Chiefs. Pia, aliwahi kufanya kazi kama skauti mkuu wa Kaizer. Mchezaji huyo mzaliwa wa Orlando-Mashariki alipata jina lake la utani wakati akicheza soka.

Baada ya kustaafu kucheza, alijiunga na Mamelodi Sundowns kama kocha, baadaye aliitwa na kukabidhiwa timu ya taifa ya Afrika Kusini ilipokubaliwa tena na kurejeshwa katika soka ya kimataifa mwaka 1992.

Baadaye alirejea Orlando Pirates ambako amefanya kazi katika nyadhifa mbalimbali kwa miongo miwili.

Tshabalala anajulikana sana kwa kutengeneza mtindo maarufu wa "piano na shoe-shine" alipokuwa Mamelodi Sundowns miaka ya 1980. Wakati anaaga dunia, Tshabalala pia alikuwa sehemu ya timu ya ufundi ya Orlando Pirates.

Tshabalala kabla ya kucheza soka alipenda zaidi mchezo wa ngumi na ndiyo ilikuwa ndoto yake kubwa, alianza kupigana ngumi tangu akiwa shule lakini maisha hubadilika wakati wowote, miaka michache baadae aligeukia soka ambalo lilimpa pesa, umaarufu mkubwa na mafanikio.

POLE KWA MWANASOKA ALIYEONDOKA AFRIKA KUSINI

Klabu yake ya zamani, Mamelodi Sundowns, ilikuwa moja ya klabu za kwanza kutuma rambirambi zao.

“Mwenyekiti na Familia ya Motsepe, Bodi ya Wakurugenzi, Timu ya Ufundi, Wachezaji, Menejimenti, Wafanyakazi, Mashabiki wa Mamelodi Sundowns FC na Taifa zima la Abayellow wanatoa pole kwa familia na marafiki tunapoomboleza msiba wa Mchezaji wa zamani wa Mamelodi Sundowns na Kocha wa Bafana Bafana, Stanley “Screamer” Tshabalala,” inasoma taarifa hiyo kutoka kwa Sundowns.

"Kama mtu aliyeanzisha chapa ya kung'aa na piano ya mpira wa miguu, urithi wa Screamer, maisha na kumbukumbu yake vitaenziwa zaidi ya udugu wa kandanda.

"Mchango mkubwa uliotolewa na Screamer Tshabalala anayependwa na mcheshi katika mchezo utaadhimishwa milele. Tunaomba Mwenyezi Mungu awafariji na kuwatia nguvu familia ya Tshabalala, marafiki zake na wafanyakazi wenzake. Roho yake ipumzike kwa amani milele."

Chanzo: www.tanzaniaweb.live