Tayari timu ya taifa ya wanawake 'Tanzanite' chini ya miaka 20 (U20). imeanza vyema kufuzu Kombe la Dunia mwakani kwa kuichapa Djibouti mabao 5-0 Uwanja wa Azam Complex Chamazi.
Mabao yote matano yalifungwa na Jamila Rajabu aliyepachika mawili, Noela Luhala, Winifrida Gerald na Yasinta Joseph yalitosha kuipa timu hiyo nafasi kubwa ya kufuzu kwa hatua inayofuata .
Baada ya matokeo hayo ya mechi ya kwanza marudio itakuwa Oktoba 11, mwaka huu Uwanja wa Azam Complex ambapo Tanzanite ikifanikiwa kuvuka hatua ya kwanza itakutana na Nigeria iliyoitoa Mauritous.
Kocha wa kikosi hicho, Ester Chabruma amesema baada ya kufanya vizuri kwenye mechi ya kwanza na kupata ushindi mnono kilichobaki ni mechi ya marudiano na kufanya vizuri kwenye michuano kwa ujumla.
Alisema tayari ameona kikosi chake na kila mechi ina matokeo yake hivyo wana siku mbili za kujiandaa ili kuvuka hatua hiyo.
"Kikubwa tutaangalia mapungufu ya timu yetu licha ya kupata magoli mengi haya ni mashindano kila mmoja anajiandaa kivyake na kila mechi ina matatizo yake." Alisema Chabruma.