Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzania kubebwa na Soka la wenye Ulemavu

A0cc828a7dbeaeb4f7f47e8d551cfc7d.png Wachezaji wa Timu ya walemavu ya Tanzania

Sat, 20 Nov 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (CANAF) ya soka la watu wenye ulemavu yatayofanyika Dar es Salaam kuanzia Novemba 26 hadi Desemba 5, mwaka huu.

Mashindano hayo, ambayo yanatarajiwa kushirikisha nchi 15 za Afrika yatafanyika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Uhuru na JMK Park.

Katika mashindano haya timu nane zitafuzu Kombe la Dunia mwakani nchini Uturuki.

Tanzania itawakilishwa na timu ya taifa ya Tanzania, Tembo Warriors na ile ya Zanzibar ambayo jina la utani inaitwa Karafuu Empire.

Hii ni mara ya pili kwa Tanzania chini ya Shirikisho la Soka la Watu Wenye Ulemavu (TAFF) kuandaa mashindano makubwa, ambapo ya kwanza yalikuwa ni ya Afrika Mashariki na timu ya Rwanda ilitwaa ubingwa na Kenya washindi wa pili, huku nafasi ya tatu ikichukuliwa na Tanzania na nafasi ya nne ikienda kwa Zanzibar.

SOKA LA WALEMAVU

Mchezo huu ulianza kuchezwa kwenye chuo cha ufundi stadi Yombo miaka ya 70 na ikaenea hadi kwenye shule zingine kama vile Jeshi la Wokovu ‘Salvation Army’ miaka ya 1980.

Katika miaka ya 1989 hadi 1990 Tanzania imewahi kuwa na klabu nne na kufanikiwa kuwa na timu ya Taifa iliyokuwa ikiitwa Tanzania Stars.

Taifa Stars ilikuwa ikipata nafasi ya kusafiri kwenda kwenye mashindano ya Norway Cup na ilikuwa ikicheza wakati wa ufunguzi kama sehemu ya kutoa burudani ya pekee kwa mashabiki wa ligi hiyo ya Norway.

Pia mchezo uliendelea hadi shule ya sekondari Pugu, miaka ya 1990 lakini ulipotea ghafla hadi ulipokuja kuanza tena 2019 kwa nguvu na kushiriki mashindano ya kimataifa na kufanya vizuri.

Soka la watu wenye ulemavu linachezwa na wachezaji saba, mmojawapo akiwa golikipa ambaye anatakiwa kuwa na mkono mmoja.

Wachezaji wa ndani lazima wawe na mguu mmoja unaofanya kazi vizuri, lakini pia mtu mwenye mguu ambao mmoja ni mfupi kabisa wanaruhusiwa kuweasehemu ya timu, lakini hawazidi wawili.

Golikipa yeye lazima awe na mkono mmoja na endepo mkono wake umekatika usawa wa kiwiko analazimika kuufunga ndani ya mwili wake.

Mchezo huu unaweza kucheza ukapumzika baadaye ukaingia tena kuendelea kucheza ila hakuna kuotea.

TEMBO WARRIORS

Baada ya kuanzishwa kwa Shirikisho la Soka la Watu Wenye Ulemavu (TAFF), Juni 25, 2018 ulianza kuchezwa rasmi katika mashindano.

TAFF ilianzisha ligi ambayo kwa sasa inachezwa Dar es Salaam pekee na kupata wachezaji, ambao wanaunda timu ya Taifa ya Tembo Warriors.

Kwa kadri ligi ilivyoendelea ndivyo idadi ya wachezaji ilivyoongezeka na sasa kuna hazina ya wachezaji wenye vipaji.

MAANDALIZI Tembo Warriors ambayo iliingia kambini Septemba mwaka huu kujiandaa na Mashindano ya Afrika na kucheza michezo ya kirafiki.

Na mwishoni mwa wiki iliyopita ilicheza michezo ya kirafiki na timu ya taifa ya Zanzibar ‘Karafuu Empire’ ambapo mchezo wa kwanza ilishinda 4-0 na mchezo wa pili ikaifunga tena 2-0.

Kocha wa timu hiyo, Salvatory Edward ‘Dokta’ alisema amefurahi kupata mechi hizo kwani zimempa nafasi ya kuwasoma zaidi wachezaji wakicheza na wenzao wenye ulemavu.

Alisema tangu waingie kambini walicheza mechi za kirafiki na timu za wanawake na za wachezaji ambao sio walemavu, hivyo hizo mechi za Zanzibar zimekuwa za manufaa kwake.

“Nimefurahi kupata mechi hizi mbili na tumecheza na wachezaji wenye ulemavu kama sisi, hivyo nimewasoma vizuri wachezaji wangu na mchezo ulikuwa wa ushindani,” alisema Salvatory.

UZOEFU KIMATAIFA

Mashindano ya Afrika Mashariki ambayo yalifanyika nchini 2019 Tanzania ilishika nafasi ya tatu, huku bingwa akiwa Rwanda, Kenya washindi wa pili na nafasi ya nne ikienda kwa Zanzibar.

Tembo Warriors iliwakilisha Tanzania katika Michuano ya Kombe la Mataifa Afrika yaliyofanyika Angola, Septemba 30 hadi Oktoba 14, mwaka 2019 kushika nafasi ya nne.

Bingwa alikuwa ni Angola, Nigeria mshindi wa pili na Liberia washindi wa tatu.

Pia Angola ni nchi ya kwanza Afrika kuchukua Kombe la Dunia, nchi nyingine zilizowahi kutwaa ubingwa huo ni Urusi ikichukua mara nne mwaka 1998, 2002, 2003 na 2014.

Nyingine ni Brazil ilichukua mwaka 2000, 2001 na 2005, Jamhuri ya Uzbekistan, ilitwaa kombe hilo mara tatu mfululizo mwaka 2007,2010 na 2012.

MAKUNDI

Tembo Warriors ipo Kundi A pamoja na nchi za Sierra Lionne, Uganda na Morocco, Kundi B na nchi za Angola, Kenya, Rwanda na Zanzibar, Kundi C lina timu za Liberia, Cameroon, Gambia na Ethiopia na Kundi D ni Nigeria, Ghana na Misri.

Kocha wa Tembo Warriors Salvatory Edward anasema hana anachohofia kwa sababu amefanya maandalizi ya mashindano siyo ya kucheza na timu fulani.

Alisema katika timu nane zitakazofuzu Kombe la Dunia, Tembo Warriors itakuwa mojawapo hivyo watanzania waje kwa wingi kuwashangilia.

SERIKALI YAJITOSA

Serikali imetenga Sh Milioni 135 kwa ajili ya mashindano kwa mujibu wa Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Hassan Abbasi.

Anasema kupewa uenyeji wa mashindano hayo makubwa inaonesha wazi kuwa Tanzania ni kitovu cha michezo Afrika.

Alisema fedha hizo zitatumika kugharamia mashindano, timu ya taifa ya soka kwa wenye ulemavu, Tembo Worriors na kuzigharamia timu nyingine 15 kwa malazi, chakula na usafiri wa kwenda na kurudi kwenye mazoezi.

Rais wa TAFF pamoja na kuishukuru serikali kwa kuyabeba mashindano ansema bado wana upungufu wa magongo ya kuchezea na kuomba wadhamini kujitokeza kuwasaidia.

Pia alisema wadau wengine wa kusaidia kwenye maji na vimiminika vingine wanakaribishwa kwa sababu mashindano yatachezwa wakati huu ambao kuna joto kali na mamlaka ya hali ya hewa imetahadharisha watu kunywa maji mengi kutokana na joto kali.

Chanzo: www.habarileo.co.tz