Rais wa Shirikisho la Soka nchini, Wallace Karia amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zitakazoandaa fainali za mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani CHAN itakayofanyika mwakani kwa kushirikiana na Kenya na Uganda.
Oktoba mwaka huu, Serikali ya Kenya ilipanga kuandaa michuano hiyo peke yao ingawa Karia ambaye pia ni rais wa Baraza la Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) alipendekeza nchi hizo kushirikiana katika fainali hizo.
"Mwaka ujao Septemba tumepewa haki kwa nchi za Tanzania, Kenya na Uganda kuandaa michuano ya CHAN kwa kila taifa, pamoja na Zanzibar ambayo itatoa kiwanja kimoja kitakachotumika kwa ajili ya mashindano hayo kwa wachezaji wa ndani," amesema.
Karia alitoa kauli hiyo wakati wa mkutano mkuu wa TFF uliofanyika Iringa, Jumamosi iliyopita mjini Iringa.
Nchi hizo tatu kwa ukanda huu wa Afrika Mashariki ni miongoni pia mwa mataifa yaliyotajwa na CAF kushirikiana katika Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) itakayofanyika 2027.
Algeria iliandaa michuano hiyo Januari hadi Februari 2023 ambapo ilipoteza mbele ya Senegal kwa mikwaju ya penalti 5-4, baada ya mchezo huo kuisha kwa suluhu.
Hii itakuwa ni mara ya tatu kwa Tanzania kushirikia michuano hiyo baada ya kufanya hivyo 2009 chini ya Mbrazili, Marcio Maximo na 2021 nchini Cameroon ikiongozwa na kocha, Etienne Ndayiragije.