Wakati dunia ikiendelea na shangwe za siku kuu ya krismasi na mwaka mpya, wadau na mashabiki wa soka jijini Mbeya wamesherekea kwa maumivu kufuatia matokeo waliyopata timu za Tanzania Prisons na Mbeya City juzi na jana.
Prisons na City zikicheza ugenini jijini Dar es Salaam zilijikuta zikiaga na kukaribisha mwaka kwa aibu baada ya kukubali vipigo vizito.
Wajelajela ndio walianza kukumbana na pigo la mwaka kwa kubanjuliwa mabao 7-1 dhidi ya Simba ikiwa ni matokeo ya rekodi kwa timu hiyo tangu ipande ligi kuu.
Ilishuhudiwa Maafande hao licha ya kwenda mapumziko wakiwa sare ya bao 1-1 kipindi cha pili kilikuwa cha dhahma kwao kwa kuruhusu mengine sita, huku mstaa wa Wekundu, John Bocco na Saido Ntibazonkiza wakifunga mabao matatu kila mmoja 'hatitriki'.
Kabla ya Mbeya City hawajamaliza kuwacheka ndugu zao hao, nao waliingia kwenye kibano cha kukung'utwa mabao 6-1 dhidi ya Azam FC usiku wa kuamkia leo.
Matokeo hayo yanaifanya City kufikisha mechi 12 mfululizo wakicheza bila ushindi na kushuka nafasi ya 10 kwa pointi 21 baada ya kushuka uwanjani mara 19.
Kipa wa Prisons, Husein Abel amesema kipigo hicho ni cha kwanza kwake katika maisha yake ya mpira na kwamba hakutarajia kukutana na mvua hiyo kubwa ya mabao.
Amesema hata wakati wa mechi zake za kirafiki huko mitaani 'Ndondo' hajawahi kuruhusu wavu wake wa mabao hayo na kwamba hii imekuwa rekodi mbaya kwake katika kazi ya soka.
"Ni kipigo cha mwaka na rekodi mbaya kwangu, mapungufu yaliyoonekana hatuna jinsi mpira uliisha salama lakini itabaki historia, Simba walituzidi tunakubali matokeo" amesema Hussein ambaye amekuwa Kipa na chaguo la kwanza kikosini.
Naye mdau wa soka jijini Mbeya, Haki Mwafumbo amesema mwaka umekuwa wa taabu kwao kwani matokeo hayo ni aibu kwa Jiji kubwa lenye kusifika kwa vipaji.
"Ni aibu ya mwaka hii tumefunga na kufungua kwa maumivu sana, lazima timu zetu zijitathmini benchi la ufundi waje na mkakati katika dirisha hili dogo kuna kitu hakipo sawa" amesema Mwafumbo.