Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tamu na chungu ya kamari michezoni

Ivan Toney Tamu na chungu ya kamari michezoni

Fri, 24 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kamari, upatu, michezo ya kubahatisha, bahati nasibu, kubeti na majina mengine mengi ambayo mwisho wa siku yanarudi kwenye maana moja kuwa ni michezo ya kubahatisha kwa njia ya kubashiri matokeo na matukio.

Kumbukumbu za maandishi zinaonyesha kamari ikichezwa katika China ya zamani karibu miaka 4,000 iliyopita. Kutokana na utandawazi uliochagizwa na kubadilika kwa teknolojia, kamari inachezwa kisasa ikiwa pia imefanikiwa kuvuka mipaka ya ardhi, anga na bahari.

Sasa kamari yaweza kuchezwa na mtu bila kwenda kwenye majumba ya kamari maarufu kama Cassino ambazo waitaliana walizianzisha miaka 400 iliyopita.Wanaocheza hawahitaji kufahamiana tena. Kila mtu anacheza kwa wakati wake kutoka kwenye kompyuta yake au kwenye simu kiganjani mwake.

Kamari ya asili ilitabiri mambo mengi ya kiroho na asili mfano matendo ya miungu kama kunyesha kwa mvua, kuchomoza kwa jua, magonjwa, vifo, kuandama kwa mwezi, kuonekana kwa nyota na mengine mengi, ubashiri wa matokeo na matukio ya michezo umechukua umaarufu kuliko ubashiri wa matukio mengine kwa sasa. Kampuni kubwa na watu binafsi wamewekeza pesa nyingi katika kutangaza masoko na kuibua teknolojia mpya za kuendesha biashara za ubashiri hasa kuhusu matokeo na matukio katika michezo.

Kama ilivyo kamari kwa ujumla wake, ubashiri katika michezo umeanza miaka mingi iliyopita,mfano katika dola ya kirumi huko Roma ambako inasemekana ubashiri ulifanyika katika mashindano ya farasi. Inasemekana ubashiri kwenye michezo ulifanyika pia kwenye michezo ya asili ya Olimpiki ya wayunani au wagiriki.

Ni vigumu kwa miaka hii kwenda kwenye tukio la michezo usikutane na bango la kampuni ya michezo ya kubahatishalikiwa limebandikwa mahali au kifuani kwa mwanamichezo. Mchezo pendwa wa mpira wa miguu naweza kusema ndio umevamiwa zaidi.

Pesa za makampuni ya michezo ya kubashiri ndizo zinaendesha mpira wa miguu kwa sasa. KAMPUNI za kamari zimekuwa wadhamini wakubwa sana wa klabu, mashindano na hata kumiliki haki za majina ya viwanja vya mpira. Kwa ujumla katika Ligi Kuu ya England, hakuna klabu inayoweza kudai kutofaidika na fedha za kampuni za michezo ya kubahatisha.

Shirika la IMARC linalojihusisha na utafiti wa masoko na biashara linaeleza kuwa thamani halisi ya uwekezaji katika sekta hii kwenye mpira wa miguu duniani ni takribani dola za Kimarekani 3.2 bilioni na inategemewa kufikia hadi dola 4 bilioni ifikapo mwaka 2028. Katika michezo, bado kamari imekuwa ni rafiki wa mashaka kwa wanamichezo na michezo.

Pamoja na uwekezaji mkubwa unaofanywa na kampuni hizi za kubeti, kamari haijawahi kuwa rafiki wa kuaminika wa michezo na wanamichezo. Tangu nyuma ambako michezo ya farasi ilikuwa maarufu zaidi katika kamari, tulisikia kashfa za waendesha farasi au wamiliki wa farasi kushiriki katika kupanga matokeo kutokana na ushawishi wa wacheza kamari.

Matokeo ya michezo huwa hatarini kuvurugwa pale wahusika wa michezo kama wachezaji, waamuzi, makocha na wadau wengine wakijihusisha katika michezo ya kubashiri bila kufuata maadili.

Michezo hii ya kubashiri ina taswira tofauti kwa wanamichezo. Vyama mbalimbali vya michezo ikiwemo Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) linapinga vikali wanamichezo wakiwamo makocha, waamuzi na benchi la ufundi kujihusisha katika michezo hiyo.

Hii inatokana na uwezo wa wahusika hao kuamua dira ya mchezo au matokeo ya mwisho ya mchezo. Hivyo basi, FIFA imeunda sheria kali endapo itachunguzwa na kubainika kwamba mhusika kati ya hao waliotajwa amejihusisha na michezo ya kamari moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja.

Njia ya moja kwa moja inahusisha mchezaji au muamuzi kuweka pesa mwenyewe kwenye mchezo wa ubashiri. Njia isiyo ya moja kwa moja ni pale ambapo mtu ambaye si mmoja wa wahusika waliolezwa hapo juu akishiriki kwenye kamari kwa pesa ya mhusika kati ya hao waliokatazwa na FIFA na kisha kugawana faida na pia muhusika akivujisha taarifa nyeti inayoweza kutumika katika michezo hii ya kubashiri.

Kutokana na sheria za maadili za FIFA, mtuhumiwa akigundulika wazi kushiriki katika michezo ya kamari anaweza kukumbana na adhabu ya kupigwa faini na kuzuiwa kushiriki katika shughuli zozote za mpira wa miguu kwa kipindi kirefu. Hukumu inaweza kutofautiana ukubwa kutokana na maelezo ya upande wa utetezi.

Wanasoka mbalimbali wamekumbana na sheria hii akiwamo aliyekuwa mshambuliaji wa klabu ya Liverpool, na timu ya taifa ya England, Daniel Sturridge, beki wa Newcastle na timu ya taifa ya England, Kieran Trippier, na hivi karibuni kabisa mshambuliaji wa klabu ya Brentford, Ivan Toney ambaye bado anatumikia adhabu yake ya kifungo cha miezi minane kujishughulisha na mpira wa miguu.

Kabla ya hapo pia wanamichezo kadhaa wamewahi kukumbana na kadhia kwa tuhuma za kujihusisha na magenge ya kamari katika kupanga matokeo. Golikipa wa Liverpool na timu ya taifa ya Zimbabwe, Bruce Grobbelaar aliripotiwa na gazeti la The Sun kunaswa akifanya mazungumzo na magenge ya wacheza kamari wa kule Asia. Kashfa hii ilimuhusisha yeye na wachezaji wa klabu nyingine pia. Bruce katika utetezi wake alidai kuongea na watu hao kwa lengo la kupata ushahidi ili akatoe taarifa polisi.

Kesi hii ilichukua muda mrefu na hata baada ya kusafishwa, mahakama ya juu ya rufaa (House of Lords) ilikataa Bruce kulipwa fidia kubwa na gazeti la The Sun na hivyo kuishia kulipwa paundi moja ya Uingereza kwa kilichodaiwa kuwa Bruce alishinda kesi lakini mazingira na mwenendo wake vilionyesha kukosekana kwa uadilifu.

Pamoja na kuharibu mwenendo na matokeo ya michezo, kushiriki kulikopindukia kwa wanamichezo katika michezo ya kubashiri kunaweza kuathiri utendaji wao viwanjani. Baadhi ya athari za kucheza kamari kwa wanamichezo ni pamoja na kupata msongo, uraibu na hasara za kifedha ikiwemo madeni na hata kufilisika.

Hapa kwetu, michezo ya kubahatisha imetamalaki kama ilivyo kwingine duniani na labda niseme kuliko ilivyo katika nchi nyingi za bara la Afrika. Kampuni za michezo hii zinazidi kuongezeka kila uchao na matangazo ya biashara ya kampuni hizi yako hewani katika kila radio, televisheni, magazeti na mabango barabarani. Katika nchi ambayo wengi wa wanamichezo wanaweza kuchukuliwa kama watu wasio na ajira kutokana na kupata ujira mdogo au uchezaji wao kuwa wa ridhaa hali hii inaweza kuwa hatari kwa wachezaji binafsi na maendeleo ya michezo kwa ujumla.

Nionavyo mimi, elimu, tahadhari na hata adhabu kwa wanamichezo na taasisi za michezo kuhusiana na suala zima la michezo ya kubashiri haijatolewa kwa kiasi cha kutosha. Wakati mwafaka wa kuelimisha wanamichezo kuhusu madhara ya michezo ya kubashiri ni sasa vinginevyo juhudi zote za kusukuma mbele michezo zinaweza kuishia kuwa bure kufumba na kufumbua.

Mwandishi wa makala hii ni katibu mkuu wa zamani wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania.Unaweza kumtumia maoni yako kupitia namba yake ya simu iliyoko hapo juu.

Kamari, upatu, michezo ya kubahatisha, bahati nasibu, kubeti na majina mengine mengi ambayo mwisho wa siku yanarudi kwenye maana moja kuwa ni michezo ya kubahatisha kwa njia ya kubashiri matokeo na matukio.

Kumbukumbu za maandishi zinaonyesha kamari ikichezwa katika China ya zamani karibu miaka 4,000 iliyopita. Kutokana na utandawazi uliochagizwa na kubadilika kwa teknolojia, kamari inachezwa kisasa ikiwa pia imefanikiwa kuvuka mipaka ya ardhi, anga na bahari. Sasa kamari yaweza kuchezwa na mtu bila kwenda kwenye majumba ya kamari maarufu kama Cassino ambazo waitaliana walizianzisha miaka 400 iliyopita.Wanaocheza hawahitaji kufahamiana tena. Kila mtu anacheza kwa wakati wake kutoka kwenye kompyuta yake au kwenye simu kiganjani mwake.

Kamari ya asili ilitabiri mambo mengi ya kiroho na asili mfano matendo ya miungu kama kunyesha kwa mvua, kuchomoza kwa jua, magonjwa, vifo, kuandama kwa mwezi, kuonekana kwa nyota na mengine mengi, ubashiri wa matokeo na matukio ya michezo umechukua umaarufu kuliko ubashiri wa matukio mengine kwa sasa. Kampuni kubwa na watu binafsi wamewekeza pesa nyingi katika kutangaza masoko na kuibua teknolojia mpya za kuendesha biashara za ubashiri hasa kuhusu matokeo na matukio katika michezo.

Kama ilivyo kamari kwa ujumla wake, ubashiri katika michezo umeanza miaka mingi iliyopita,mfano katika dola ya kirumi huko Roma ambako inasemekana ubashiri ulifanyika katika mashindano ya farasi. Inasemekana ubashiri kwenye michezo ulifanyika pia kwenye michezo ya asili ya Olimpiki ya wayunani au wagiriki.

Ni vigumu kwa miaka hii kwenda kwenye tukio la michezo usikutane na bango la kampuni ya michezo ya kubahatishalikiwa limebandikwa mahali au kifuani kwa mwanamichezo. Mchezo pendwa wa mpira wa miguu naweza kusema ndio umevamiwa zaidi.Pesa za makampuni ya michezo ya kubashiri ndizo zinaendesha mpira wa miguu kwa sasa. KAMPUNI za kamari zimekuwa wadhamini wakubwa sana wa klabu, mashindano na hata kumiliki haki za majina ya viwanja vya mpira. Kwa ujumla katika Ligi Kuu ya England, hakuna klabu inayoweza kudai kutofaidika na fedha za kampuni za michezo ya kubahatisha.

Shirika la IMARC linalojihusisha na utafiti wa masoko na biashara linaeleza kuwa thamani halisi ya uwekezaji katika sekta hii kwenye mpira wa miguu duniani ni takribani dola za Kimarekani 3.2 bilioni na inategemewa kufikia hadi dola 4 bilioni ifikapo mwaka 2028. Katika michezo, bado kamari imekuwa ni rafiki wa mashaka kwa wanamichezo na michezo.

Pamoja na uwekezaji mkubwa unaofanywa na kampuni hizi za kubeti, kamari haijawahi kuwa rafiki wa kuaminika wa michezo na wanamichezo. Tangu nyuma ambako michezo ya farasi ilikuwa maarufu zaidi katika kamari, tulisikia kashfa za waendesha farasi au wamiliki wa farasi kushiriki katika kupanga matokeo kutokana na ushawishi wa wacheza kamari.

Matokeo ya michezo huwa hatarini kuvurugwa pale wahusika wa michezo kama wachezaji, waamuzi, makocha na wadau wengine wakijihusisha katika michezo ya kubashiri bila kufuata maadili.

Michezo hii ya kubashiri ina taswira tofauti kwa wanamichezo. Vyama mbalimbali vya michezo ikiwemo Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) linapinga vikali wanamichezo wakiwamo makocha, waamuzi na benchi la ufundi kujihusisha katika michezo hiyo. Hii inatokana na uwezo wa wahusika hao kuamua dira ya mchezo au matokeo ya mwisho ya mchezo. Hivyo basi, FIFA imeunda sheria kali endapo itachunguzwa na kubainika kwamba mhusika kati ya hao waliotajwa amejihusisha na michezo ya kamari moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja.

Njia ya moja kwa moja inahusisha mchezaji au muamuzi kuweka pesa mwenyewe kwenye mchezo wa ubashiri. Njia isiyo ya moja kwa moja ni pale ambapo mtu ambaye si mmoja wa wahusika waliolezwa hapo juu akishiriki kwenye kamari kwa pesa ya mhusika kati ya hao waliokatazwa na FIFA na kisha kugawana faida na pia muhusika akivujisha taarifa nyeti inayoweza kutumika katika michezo hii ya kubashiri.

Kutokana na sheria za maadili za FIFA, mtuhumiwa akigundulika wazi kushiriki katika michezo ya kamari anaweza kukumbana na adhabu ya kupigwa faini na kuzuiwa kushiriki katika shughuli zozote za mpira wa miguu kwa kipindi kirefu. Hukumu inaweza kutofautiana ukubwa kutokana na maelezo ya upande wa utetezi.

Wanasoka mbalimbali wamekumbana na sheria hii akiwamo aliyekuwa mshambuliaji wa klabu ya Liverpool, na timu ya taifa ya England, Daniel Sturridge, beki wa Newcastle na timu ya taifa ya England, Kieran Trippier, na hivi karibuni kabisa mshambuliaji wa klabu ya Brentford, Ivan Toney ambaye bado anatumikia adhabu yake ya kifungo cha miezi minane kujishughulisha na mpira wa miguu.

Kabla ya hapo pia wanamichezo kadhaa wamewahi kukumbana na kadhia kwa tuhuma za kujihusisha na magenge ya kamari katika kupanga matokeo. Golikipa wa Liverpool na timu ya taifa ya Zimbabwe, Bruce Grobbelaar aliripotiwa na gazeti la The Sun kunaswa akifanya mazungumzo na magenge ya wacheza kamari wa kule Asia. Kashfa hii ilimuhusisha yeye na wachezaji wa klabu nyingine pia. Bruce katika utetezi wake alidai kuongea na watu hao kwa lengo la kupata ushahidi ili akatoe taarifa polisi. Kesi hii ilichukua muda mrefu na hata baada ya kusafishwa, mahakama ya juu ya rufaa (House of Lords) ilikataa Bruce kulipwa fidia kubwa na gazeti la The Sun na hivyo kuishia kulipwa paundi moja ya Uingereza kwa kilichodaiwa kuwa Bruce alishinda kesi lakini mazingira na mwenendo wake vilionyesha kukosekana kwa uadilifu.

Pamoja na kuharibu mwenendo na matokeo ya michezo, kushiriki kulikopindukia kwa wanamichezo katika michezo ya kubashiri kunaweza kuathiri utendaji wao viwanjani. Baadhi ya athari za kucheza kamari kwa wanamichezo ni pamoja na kupata msongo, uraibu na hasara za kifedha ikiwemo madeni na hata kufilisika.

Hapa kwetu, michezo ya kubahatisha imetamalaki kama ilivyo kwingine duniani na labda niseme kuliko ilivyo katika nchi nyingi za bara la Afrika. Kampuni za michezo hii zinazidi kuongezeka kila uchao na matangazo ya biashara ya kampuni hizi yako hewani katika kila radio, televisheni, magazeti na mabango barabarani. Katika nchi ambayo wengi wa wanamichezo wanaweza kuchukuliwa kama watu wasio na ajira kutokana na kupata ujira mdogo au uchezaji wao kuwa wa ridhaa hali hii inaweza kuwa hatari kwa wachezaji binafsi na maendeleo ya michezo kwa ujumla.

Nionavyo mimi, elimu, tahadhari na hata adhabu kwa wanamichezo na taasisi za michezo kuhusiana na suala zima la michezo ya kubashiri haijatolewa kwa kiasi cha kutosha. Wakati mwafaka wa kuelimisha wanamichezo kuhusu madhara ya michezo ya kubashiri ni sasa vinginevyo juhudi zote za kusukuma mbele michezo zinaweza kuishia kuwa bure kufumba na kufumbua.

Mwandishi wa makala hii ni katibu mkuu wa zamani wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania.Unaweza kumtumia maoni yako kupitia namba yake ya simu iliyoko hapo juu.

Chanzo: Mwanaspoti