Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tamu, chungu Ligi ya vijana U20

Under 20 Tamu, chungu Ligi ya vijana U20

Thu, 6 Jul 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Msimu wa 13 wa Ligi Kuu ya vijana chini ya miaka 20 ulimalizika mwishoni mwa wiki na kushuhudia Mtibwa Sugar ikiitwa tena ubingwa. Ukurasa huu ambao ulikita kambi pale Azam Complex tangu kuanza kwa mashindano hayo Juni 22, iunakuletea mambo kadhaa uliyoona kuanzia siku ya kwanza hadi ya mwisho.

1. MTIBWA SUGAR NI REAL MADRID

Mtibwa Sugar wameshinda ubingwa wao wa tano wa ligi ya vijana baada ya kuifunga Geita Gold bao 1-0 kwenye fainali.

Vijana hao kutoka katikati ya mashamba ya miwa pale Madizini, Turiani Morogoro, wamefanya kama Real Madrid ya Hispania inavyofanya kwenye ligi ya mabingwa Ulaya, wakati huo ikiitwa Klabu Bingwa Ulaya.

Mtibwa Sugar ambao miaka ya mwanzoni ya mashindano haya haikuwa timu tishio, ilibadilika kuanzia mwaka 2018 pale Dodoma walipoifunga Stand United kwenye fainali, na kuanzia hapo wamekuwa hawashikiki.

Real Madrid ambao wanaongoza kutwaa ubingwa wa vilabu barani Ulaya, walishinda mara tano mfululizo kuanzia 1956 hadi 1960, na hadi sasa hawashikiki.

2. AZAM FC HAIPENDWI CHAMAZI

Mechi ya nusu fainali kati ya Mtibwa Sugar na Azam FC ilikuwa mwendelezo wa kinachoikuta Azam FC kila mechi dimbani pale, kwani uwanja mzima ulikuwa upande wa Mtibwa Sugar utadhani wao ndiyo wako kwenye uwanja wao wa nyumbani.

Sapoti ambayo Mtibwa Sugar waliipata ni kubwa kiasi kwamba hata wakiwa kwao pale Manungu hawaipati. Siyo kwamba watu wa Chamazi wanaipenda sana Mtibwa Sugar, hapana. Wanahamishia tu mapenzi yao kwa muda kwa sababu hawaipendi Azam FC.

Na hii hutokea hata kwa timu kubwa. Azam FC ikiwa Chamazi inapata wakati mgumu kutoka majukwaani kwa sababu watu wote wanakuwa upande wa mpinzani. Na kwa sababu kiingilio ni bure, basi wanaitana wengi kuja kuizomea timu yao ya nyumbani.

Hii ni bahati mbaya sana. Chamazi inapaswa kubadilika na kuiunga mkono timu yao ya nyumbani. Hata kama watu wa huko Wana timu zao wanazozipenda, lakini inapocheza Azam FC na timu ambazo siyo zao basi wawe nayo. Ni timu iliyolipa heshima kubwa eneo. Leo hii Afrika nzima inaijua Chamazi kuliko Masaki wanakoishi matajiri.

Chamazi inatajwa na kuandikwa mara nyingi zaidi kuliko Oysterbay au Mikocheni. Zaidi tu ya hiyo, Azam FC imefanya makubwa mengi kwa ajili ya maendeleo ya watu wa eneo lile. Imejenga madarasa mawili shule ya msingi Chamazi. Imejenga ofisi ya serikali ya mtaa Bamia. Imejenga visima vya maji, Sekondari ya Mbande, maji ambayo hutumiwa hata na wananchi wa kawaida siyo tu wanafunzi.

Palepale Azam Complex, Azam FC imefunga mitambo ya kuchuja maji inayotumiwa kuchuja maji ya Uhai yanayouzwa madukani, lakini pale siyo kwa ajili ya maji ya kuuza bali kwa matumizi ya kawaida.

Mabomba ya maji hayo yamefungwa kuuzunguka ukuta wa uzio wa uwanja ili wananchi wakinge bure. Yaani watu wanaozunguka ukuta wa Azam Complex wanatumia maji sawa na ya kiwandani kasoro wao wanaweka kwenye ndoo zao. Inasikitisha sana kuona watu wanaofaidika na Azam FC kiasi hiki wanaongoza kuichukia timu hii.

3. UDANGANYIFU WA UMRI

Kama ambavyo imekuwa ikitokea kila mwaka, mashindano ya mwaka huu pia yakitawaliwa na udanganyifu wa umri kwa wachezaji. Kuna sura za wachezaji ukiziangalia utabaini kwamba wamezidi mbali sana umri halali wa mashindano haya. Kuna wachezaji wameshiriki mashindano haya kwa misimu minne, tangu 2018. Unajiuliza, wakati ule walikuwa na miaka chini ya 15?

Mechi ya robo fainali kati ya Azam FC na TZ Prisons ilichelewa kuanza kwa takribani dakika tano baada ya maofisa wa TFF kubaini udanganyifu upande wa Tanzania Prisons. Kipa aliyetakiwa kucheza siku hiyo, Haji Salum Haji alizuiwa kucheza kwa sababu ya kuzidi umri.

Kabla ya kuanza kwa mashindano haya, TFF hukagua wachezaji na wanaobainika kuzidi umri huondolewa. Kipa wa Prisons alinaswa katika mtego huu hivyo hakutakiwa kushiriki. Lakini Tanzania Prisons wakafanya udanganyifu, wakambadili jina na kumleta kwenye mashindano akitumia jina jipya la Haji Salum Haji, na kuacha jina lake la halisi ambalo lilibainika kwenye vipimo.

Kwa hiyo maofisa wa TFF walipomuona kwa sura wakamkumbuka na kuzuia mchezo kuanza ili wakajiridhishe kwenye mtandao. Wakabaini ni kweli. Ikatoka amri kwamba wambadilishe kipa ndipo akaingia Ibrahim Mussa Kapona, na mchezo ukaanza.

4. MFUMO MBAYA WA MASHINDANO

Mashindano haya ni ligi kuu ya vijana ikiwa na maana kwamba huu ndiyo msimu wao rasmi, Lakini kwa namna yanavyoendeshwa huwezi amini kwamba huu ndiyo msimu rasmi wa ligi ya vijana. Timu iliyocheza mechi nyingi zaidi ni sita, na hizi ni zile zilizofika nusu fainali.

Kwa zile zilizoishia hatua ya makundi zitakuwa zimecheza mechi tatu tu, yaani msimu mzima timu inacheza mechi tatu rasmi...hadi msimu ujao. Hii siyo sawa kwa maendeleo ya vijana. TFF waache ujanjaujanja huu wa kukwepa gharama. Kazi yao ni kusimamia maendeleo ya kiufundi ya mpira ikiwemo watoto kucheza sana.

Na kuna fungu wanapata kutoka FIFA kwa ajili ya maendeleo ya soka la vijana, zinaenda wapi? Mfumo huu ulikuwa unatumika zamani kutokana na ukata uliokuwa unalikabili Shirikisho...lakini sasa hali ni tofauti. TFF ina hela nyingi, iache kufanya mashindano ya kijanja janja.

5. FAINALI ILIYOTANGULIA

Nusu fainali ya Mtibwa Sugar na Azam FC ilikuwa na ushindani mkubwa sana kuliko mechi zote za msimu huu kwenye mashindano hayo. Timu hizi zilicheza kwa mipango, uwezo wa mchezaji mmoja mmoja na hata kitimu. Kasi ya mchezo ilikuwa kubwa kuanzia mwanzo hadi mwisho. Mpira unatoka nyuma unapitia sehemu zote za msingi kabla haujafika mbele.

Kwa walioshuhudia mchezo huu watakubaliana nami kwamba walifaidi zaidi kuliko kwenye fainali. Mechi hii ilionesha kwamba Mtibwa Sugar na Azam FC wako mbali sana na wengine wote waliobaki.

6. VIGOGO CHALI

Yanga na Simba, miamba wa soka la Tanzania wamefanya vibaya sana msimu huu. Wote wametoka hatua ya makundi bila kushinda hata mchezo mmoja. Katika michezo waliyocheza, wote wamefungwa miwili na kupata sare moja pekee. Simba wametoka bila kufunga hata bao moja, wakiwa wamefungwa mabao matatu.

Angalau Yanga waliambulia mabao mawili ya kufunga, lakini hata hivyo walikuwa dhaifu katika ulinzi wakiruhusu mabao matano. Yanga hawajawahi kutwaa ubingwa wa ligi ya vijana, huku Simba ikiwa imeshinda mara mbili; 2011 na 2017. Mara zote waliifunga Azam FC kwa changamoto ya mikwaju ya penati.

7. DAKTARI MTIBWA AGOMA KUTOKA

Daktari wa Mtibwa Sugar alioneshwa kadi nyekundu dakika ya 75 kwa kosa la kuwasumbua waamuzi wakiwa kwenye majukumu yao. Hii ilikuwa kwenye mechi wa nusu fainali dhidi ya Azam FC.

Daktari huyo alikuwa akiingia uwanjani kila mara wachezaji wake wakianguka, bila kuruhusiwa na mwamuzi. Alionywa mara kadhaa na safari hii akaadhibiwa. Lakini cha ajabu hakutoka kwenye benchi la ufundi, akaendelea kuhudumu hadi mwisho.

Mwamuzi wa akiba alimfuata na kumtaka kutoka lakini akagoma na kukatokea malumbano marefu hadi alipokuja daktari wa msalaba mwekundu na kuja kuweka hali sawa. Daktari huyo akabaki na akaendelea kuhudumu.

8. GEITA GOLD KAMA MANCHESTER UNITED

Moja ya fainali za kusisimua za Ligi ya Mabingwa Ulaya ni ile ya 1999 ambapo Manchester United ilibadili matokeo dakika tatu za nyongeza dhidi ya Bayern Munich. Ikiwa nyuma 1-0, Manchester United ilifunga mabao mawili ya haraka haraka dakika tatu za nyongeza na kuwa mabingwa.

Hiki ndicho kilichotokea kwa Geita Gold kwenye robo fainali dhidi ya Mbeya City. Walikuwa nyuma bao 1-0 hadi dakika tatu za nyongeza na kufunga mabao mawili ya haraka haraka na kutinga nusu fainali. Na mabao yote yalikuwa ya papatu papatu vile vile kama yale ya Manchester United 1999.

9. MGOSI ACHARUANA NA WAZEE WA SIMBA Kwenye mchezo wao wa mwisho hatua ya makundi dhidi ya Azam FC, wazee kadhaa wa Simba waliokuwa jukwaa la VIP walikuwa wakitupa maneno ya lawama kwa kocha wao Mussa Hassan Mgosi. Walilaumu kila kitu kuhusu timu, kuanzia uwezo wa wachezaji, mbinu za walimu na hata mabadiliko yaliyofanyika.

Wazee wale wakasema 'na una bahati Azam leo wamepanga kikosi B, la sivyo ingekuwa fedheha sana'.

Kwa bahati mbaya sana wazee wale walikuwa nyuma tu ya benchi la ufundi la Simba hivyo Mgosi aliyasikia maneno yale yenye kukera kwa ukaribu wa kutosha. Wakati wa mapumziko, akapanda jukwaa la VIP na kuwacharukia. Aliwawakiwa wale wazee kwa ukali ulioshiba, wote wakakaa kimya.

Mgosi alitamba pale jukwaani kama enzi za Chidi Benz alivyotawala jukwaa. Akashuka na kwenda zake kwenye vyumba vya kubadilishia nguo kuongea na wachezaji wake. Kipindi cha pili wazee wale wote walikaa kimya, somo la Mgosi lilieleweka.

10 MASIKINI CHASIMBA

Nahodha wa sasa wa timu ya vijana ya Mtibwa Sugar, Ladaki Chasabi, alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mashindano hayo msimu uliopita. Uchaguzi wa mchezaji bora wa mashindano hufanywa na wenye mashindano yao, yaani TFF.

Lakini kwenye tuzo za TFF zilizofanyika Tanga mwezi Juni, TFF haohao walimtangaza Clement Mzinze wa Yanga kuwa mchezaji bora wa ligi ya vijana ya msimu uliopita. Unajiuliza, ligi ipi? Ligi ambayo Mzinze alicheza hakuwa mchezaji bora wa mashindano, bali Chasabi.

Ikawaje Mzinze akapewa tuzo ambayo haikuwa yake. Nini kimebadilika? TFF wamepewa na nani hili? Huo ni mwendelezo wa sintofahamu ya tuzo za TFF ambazo kila msimu lazima ziwe na kasoro kuliko msimu uliopita.

Tuzo ya mchezaji bora chipukizi ilitambulishwa na utawala wa Jamal Malinzi kumuenzi Ismail Mrisho, mchezaji wa Mbao FC ya Mwanza aliyefariki dunia uwanjani mjini Bukoba, Desemba 2016 kwenye mashindano ya 2016/17.

Na jina la tuzo liliitwa hivyohivyo, Tuzo ya Ismail Mrisho na mshindi wa kwanza alikuwa Shaaban Chilunda wa Azam FC, lakini tangu utawala wa Wallace Karia tangu uingie, jina la tuzo hiyo halikuwahi kutumika. Wameliweka pembeni na kinachofanyika ndicho hiki.

Chanzo: Mwanaspoti