Straika wa Singida Big Stars, Amissi Tambwe anapenda kujitathimini baada ya kazi, kama anavyosimulia alikuwa na msimu mbaya (2022/23), akifunga mabao machache mawili, jambo linalomfanya atumie likizo yake kujifua zaidi ili kuongeza makali yake.
Chini ya kocha Hans Pluijm, hakuwa na nafasi mbele ya mastaa waliokuwa wanaanza kikosini kama Meddie Kagere na Bruno Gomes raia wa Brazil, anafafanua hilo jinsi alivyokuwa anatumia dakika tano wakati mwingine 10 za mwisho kulinda uhai wa kipaji chake.
"Kwanza nakiri kikosi chetu kilikuwa na ushindani mkali kila namba, pia kuna wakati mchezaji anapitia upepo mbaya kama ilivyonitokea mimi huo ndio msimu wangu wa kwanza kufunga mabao machache tangu nianze kucheza timu za Ligi Kuu katika mataifa mbalimbali.
"Japokuwa kwangu sikufurahia nilichokivuna, ila kwa timu tulikuwa na msimu mzuri, kupanda daraja na kumaliza nafasi ya nne inayotupa fursa ya kucheza Kombe la Shirikisho Afrika ni jambo la kujivunia siyo dogo, kila mchezaji anapenda kucheza michuano hiyo inayotazamwa na watu mbalimbali."
SBS ilipopanda Tambwe alikuwa mfungaji namba mbili kwa mabao baada ya kufunga 14 nyuma ya kinara wa mabao 15 Edward Songo wa JKT Tanzania. "Tangu nianze kucheza Tanzania 2013/14, Simba nilimaliza kinara wa mabao 19, 2014/15 Yanga kwa mara ya kwanza 14, msimu uliofuata nilikuwa kinara wa mabao 21, ndio maana nilijisikia vibaya kumaliza msimu ulioisha na mabao mawili."
Anasisitiza hakuna straika anaweza akawa na maajabu ya kumiliki mabao mengi akiwa benchi, anaamini angepewa nafasi angefunga zaidi ya mabao 10, kwani anaona ana uwezo wa kucheka na nyavu.
"Kadri unavyocheza ndivyo unavyokuwa na hamu ya kucheka na nyavu, lakini ukikaa benchi na ikatokea ukapata nafasi unaweza ukakuta unakamia mechi hadi unakosea, kwa sababu unakuwa na presha ya kutaka kumuonyesha kocha uwezo wako, changamoto hiyo sio mimi pekee uliza mchezaji yoyote atakwambia," anasema.
LIGI YA TZ Anasema kwa sasa Tanzania imegeuka Ulaya ndogo kwa nchi jirani, akitoa sababu ya Ligi Kuu Bara imekuwa maarufu na mastaa wengi wanatamani kuja kucheza, wakiamini vipaji vyao vitaonekana kwa ukubwa. "Nina marafiki Ulaya ambao wanaifuatilia Ligi ya Tanzania, hilo limetokana na namna ambavyo imetangazwa na ni mchezo pendwa kwa mashabiki, hivyo hakuna mchezaji ataacha kutamani kuja.
"Ukitaka kuamini hilo wachezaji wanaweza wakaja kucheza wakiwa hawana majina, kwa namna mashabiki wanavyopenda soka akiwafurahisha thamani ya mchezaji inakuwa juu na kufanya nchi nyingine kuona huduma yake." Tambwe ambaye bado ana mkataba wa mwaka mmoja na SBS, anasema kwa jinsi ushindani unavyongezekana anajipanga kuhakikisha anabalisha upepo kutoka kutozungumzwa na hadi habari ya mjini.
"Ukiona straika anatajwa kila kona ujue anafanya yake uwanjani, ndio maana unaona alikuwa anatajwa Fiston Mayele wa Yanga, Moses Phiri kabla ya kuumia, akaja Said Ntibanzokiza 'Saido' ni kwa sababu ya kazi yao," anasema.
Alipoulizwa ana hat-trick ngapi tangu aanze kucheza Ligi Kuu anajibu "Nina nyingi sana siwezi kuzikumbuka, kule Burundi ndio usiseme kuna wakati nilikuwa nafunga mabao 30, ndio maana nasema msimu ulioisha kwangu hakuwa wa afya kwenye karia yangu."
MASTAA SBS Anasema maisha ya mastaa wa SBS yalikuwa mazuri, kwani walikutana wenye mtazamo wa mbali, hivyo kila mmoja alikuwa anajua nini kimempeleka kwenye timu hiyo. "Tuliishi maisha mazuri kwa maana ya mchezaji kupata mahitaji yake ya msingi kwa wakati, ilikuwa timu yenye malengo makubwa, kwa sehemu yametimia kwani timu imepata nafasi ya kushiriki michuano ya CAF,"anasema.
Tambwe ambaye amezichezea Simba na Yanga kwa nyakati tofauti, anaeleza utofauti wa maisha ya klabu hizo na SBS kwamba ni kwenye upande wa mashabiki, ila mengine yapo sawa.
"Simba na Yanga zina mashabiki wa kutosha ambao wanapenda timu zao, unapofanya vizuri utapata zawadi mbalimbali, ila maisha mengine ya kawaida kwa msimu ulioisha sikuona tofauti nyingine,"anasema.
PLUIJM KOCHA WA AINA GANI Tambwe amefundishwa na kocha Hans Pluijm tangu wakiwa Yanga, anamuelezea ni kocha anayefundisha kucheza mpira zaidi kwa kutumia akili kubwa na nidhamu ya juu.
"Chini ya Pluijm unaujua mpira zaidi, kwani anakufundisha namna unavyotakiwa kuchezwa, kwangu ni kocha mzuri anayekupa faida nyingi za kujua ufanye nini ndani ya uwanja, hata wakati wa mazoezi ujiandaaje,"anasema.