Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tambwe awapa Yanga Krismasi

33402 Pic+tambwe Tambwe

Wed, 26 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mabao matatu ‘Hat trick’ aliyofunga Amiss Tambwe katika mchezo wa Kombe la Azam Sports Federation Cup dhidi ya Tukuyu Stars jana yamemfanya afikishe idadi ya mechi saba kufunga kwa namna hiyo huku Yanga ikifuzu hatua inayofuata.

Kabla ya mabao hayo, Tambwe tayari alishafunga mabao matatu kwenye mchezo mmoja mara sita tangu alipoanza kucheza hapa nchini akitokea Burundi ambapo alifanya hivyo kwenye Ligi Kuu dhidi ya timu za Polisi Moro, JKT Oljoro, Coastal Union, Majimaji, Mgambo Shooting na Stand United.

Nyota ya Tambwe kwenye mchezo wa jana ilianza kung’aa mapema dakika ya 13 baada ya kufunga bao la kuongoza akimalizia mpira uliotemwa na kipa wa Tukuyu Stars, uliotokana na kichwa cha Feisal Salum ‘Fei Toto’.

Kuingia kwa bao hilo, Tukuyu Stars walionyesha nia ya kupambana na Yanga ili kusaka bao la kusawazisha lakini kukosa kwao uzoefu kuliwagharimu na kuwafanya wapoteze nafasi chache walizozipata ikiwemo ile ya dakika ya 21 ambayo Malule Omary kushindwa kufumania nyavu akiwa ana kwa ana na kipa wa Yanga, Klaus Kindoki.

Nafasi hiyo waliyokosa Tukuyu Stars ni kama iliwaponza kwani walianza kushambuliwa mfululizo na Yanga iliyoonyesha njaa ya kufunga idadi kubwa ya mabao katika mchezo huo uliokuwa wa upande mmoja.

Tambwe tena aliwanyanyua vitini mashabiki wa Yanga baada ya kufunga bao la pili akimalizia mpira wa kichwa uliopigwa na Deus Kaseke ambaye alitumia vyema udhaifu wa mabeki wa Tukuyu Stars waliojichanganya na kumpasia wakati walipokuwa kwenye harakati za kuokoa.

Katika kipindi hicho cha kwanza, nyota aliyesajiliwa na Yanga kwenye dirisha dogo, Haruna Moshi ‘Boban’ alikuwa kivutio kutokana na pasi alizokuwa akipiga kwenda kwa washambuliaji wa timu hiyo ingawa alilazimika kutolewa dakika ya 26 akiwa anachechemea.

Matokeo hayo yalidumu hadi wakati wa mapumziko na dakika kumi tu baada ya kipindi cha pili kuanza, Tambwe alifunga hesabu ya mabao kwa upande wake baada ya kuipatia Yanga bao la tatu.

Mshambuliaji aliye kwenye kiwango bora hivi sasa, Heritier Makambo, alipigilia msumari kwenye jeneza la Tukuyu Stars dakika ya 80 baada ya kuifungia Yanga bao la nne akimalizia vyema pasi ya Paul Godfrey.

Yanga ambayo ilifanya mabadiliko machache kwenye mchezo wa jana, itapaswa kujilaumu yenyewe kwani ilipoteza nafasi nyingi ambazo zingeweza kuwafanya waondoke na ushindi mnono.



Chanzo: mwananchi.co.tz