Mshambuliaji wa Singida Big Stars, Amissi Tambwe si miongoni mwa mastaa waliokuja Zanzibar kwenye mashindani ya Mapinduzi Cup, lakini cha ajabu jezi yake ipo na imeonekana uwanjani.
Hivi karibuni taarifa kutoka ndani ya Singida ilisema kuwa timu hiyo inataka kuachana na mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba na Yanga na hilo limedhihirika baada ya jezi yake kuvaliwa na mchezaji mwingine.
Iko hivi; SBS juzi wameibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya KMKM, mshambuliaji aliyeipandisha timu hiyo na kumaliza msimu akiwa kinara wa upachikaji wa mabao kwa kukwamisha mpira nyavuni mara 14, Tambwe sio sehemu ya kikosi cha timu hiyo kilichopo Zanzibar lakini kuna staa ameonekana akivaa jezi namba 17 mgongoni.
Mshambuliaji wa zamani wa Al Masry ya Misri, raia wa DR Congo, ndiye aliyekabidhiwa jezi hiyo na juzi alipewa nafasi ya kuanza kwenye kikosi cha kwanza akitumika dakika 73.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya timu hiyo kimeliambia Mwanaspoti kuwa staa huyo wapo kwenye mazungumzo naye ya kutaka kumvunjia mkataba kutokana na yeye mwenyewe kugoma kutolewa kwa mkopo.
“Ni kweli hayupo lakini sio yeye pekee ambaye hajaonekana hapa kwani kuna Meddie Kagere, Pascal Wawa na wengine hawapo kwanini Tambwe,” kilihoji chanzo hicho.
“Ni kweli jezi yake imeonekana amevaa mtu lakini bado ni mchezaji wetu kwasababu anamkataba na timu japo kuna mazungumzo yanafanyika kwa lengo la kuvunja mkataba,” kilisema chanzo hicho.