Aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga, Amisi Tambwe ameanza vyema Championship baada ya kuifungia timu yake ya DTB mabao manne dhidi African Lyon kwenye mchezo wa ufunguzi wa ligi hiyo.
Kipindi cha kwanza Tambwe aliipeleka timu yake mapumziko ikiwa inaongoza mabao mawili aliyofunga baada ya kumalizia krosi nzuri iliyotokea upande wa kushoto.
Nahodha huyo alionekana kuwa tishio wakati wote ambapo pia machachali yake yalitosha kusababisha African Lyon kwenda mapumziko wakiwa pungufu baada ya mchezaji wao kuonyeshwa kadi nyekundu kwa kumfanyia Tambwe madhambi.
Safu ya kiungo ya timu yake iliweza kutawala eneo la katikati na kuweza kumchezesha na kummegea mapande huku safu hiyo ikiongozwa na aliyekua mchezaji wa Simba Nicholaus Gyani.
Kipindi cha pili Tambwe aliendelea kua tishio kwa mabeki wa African Lyon ambapo haikumchukua muda akaweza kuumkwamisha mpira wavuni baada ya kumalizia pasi nzuri aliyopewa na Gyan na kumfanya apate 'Hat trik'
Muda mchache baada ya kufunga bao lake la tatu Tabwe aliweka tena mpira kimiani na kutimiza bao la nne la mchezo na kumfanya awe kinara wa mabao wa Championship.
Baada ya mchezo kumalizika Tambwe alizungumza na Mwanaspoti na kusema kuwa sababu ni kuwa alijianda vyema.
"Niliweza kupata muda mzuri wa kujiaanda mimi pamoja na timu yangu hivyo ikawa rahisi kupata mabao hayo" aliendelea kusema
"Hii ni salamu kwa mashabiki wangu na nitaarifa kuwa nimerejea sasa na hichi nilichokifanya leo ni kitu cha kawaida kwangu" amesema Tabwe.
Kocha wa DTB alisema hajashangaa sana kutokana na ubora wa Tambwe.
"Ni moja kati ya wachezaji ambao wana uzoefu mkubwa wa kuzivumania nyavu na pia alifanya maandalizi ya kutosha kuelekea kwenye mchezo huu pongezi kwake" alisema