Mabao mawili yaliyofungwa na staa, Dany Mrwanda yametosha kuihakikishia Ken Gold pointi tatu dhidi ya Transit Camp.
Katika mechi hiyo iliyopigwa leo Jumamosi katika uwanja wa Sokoine jijini hapa, ilishuhudiwa soka safi kwa timu zote lakini wenyeji waliweza kutakata nyumbani kwa mabao 2-1.
Ken Gold ndio walitangulia kupata bao dakika ya 35 kupitia kwa Mrwanda kwa mkwaju wa penalti baada ya beki wa Transit Camp, Hamis Hajji kuushika mpira eneo la hatari.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kwa huku Transit Camp wakilazimisha mashambulizi na kufanikiwa kupata bao dakika ya 60 kupitia kwa Valentino Mashaka aliyetoka benchi.
Timu zote ziliendelea kushambuliana na dakika ya 85, Mrwanda tena aliweza kuwainua tena bao la pili na la tano kwake hadi sasa akiunganisha vyema krosi ya Ajibu Mohamed.
Wakati Ken Gold ikitakata, huko Mbarali Ihefu FC wamejikuta wakifa mbele ya DTB kwa mabao 2-1 yakifungwa na Amis Twambe dakika ya 26 na 38,huku la kujifariji kwa wenyeji likiwekwa wavuni na Joseph Mahundi dakika ya 56.
Kwa matokeo hayo, DTB inaendelea kubaki kileleni kwa pointi 11, huku Ken Gold wakifikisha alama 10 katika nafasi ya pili na kuweka vita kali kwenye kusaka nafasi ya kupanda Ligi Kuu msimu ujao.