Baada ya kujihakikishia nafasi ya kushiriki mashindano ya kimataifa uongozi wa Singida Big Stars umeanza kupunguza wachezaji wanaoonekana kutokuwa na msaada ndani ya timu na kuingiza maingizo mapya.
Singida BS ina mpango wa kuachana na washambuliaji wao wawili wa kigeni Amis Tambwe (Burundi) na Dario Frederico (Brazil) ambaye tayari yupo nchini kwao kwa ajili ya matibabu.
Dario alijiunga Singida BS mwanzoni mwa msimu huu akiwa kwenye kiwango bora na kuwa kivutio kwa mashabiki nchini lakini akaandamwa na majeraha na Januari 27 mwaka huu mabosi wake walimpa ruhusa ya kwenda kwao kupata matibabu.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Singida BS kililiambia Mwanaspoti wachezaji hao wawili hawatakuwa miongoni mwa wachezaji watakaoitumikia timu hiyo msimu ujao.
"Frederico alifanyiwa vipimo na kutambulika kuwa fiti lakini viongozi walimwamuru aendelee kubaki nchini kwao ataungana na timu msimu ujao, hilo halitawezekana tena kwa sababu benchi la ufundi limependekeza kumwacha na kutafuta mchezaji mwingine;
"Tambwe pia hataweza kucheza msimu ujao, alitakiwa kuondoka tangu dirisha dogo lakini makubaliano hayakwenda vizuri kama tulivyokuwa tunatarajia." kilisema chanzo hicho ambacho hakikutaka jina lake litajwe
Chanzo hicho kilisema wapo kwenye mchakato wa kutafuta mshambuliaji na beki mmoja wa kati kwa ajili ya kukisuka kikosi imara na cha ushindani msimu ujao ambao wataiwakilisha nchi kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.
"Kocha ameutaka uongozi kumsajili msambuliaji mwenye uzoefu ambaye ana jicho la kuona goli ili kuongeza nguvu eneo hilo ambalo amekiri linachangamoto."