Katika ulimwengu wa sasa miongoni mwa mambo yaliyotawala maisha na hata michezo ni hesabu za kidigitali na takwimu.
Mchezo wa kandanda nao siku hizi umejaa matakwimu – mabao, kuotea, umiliki wa mpira, mipira ya adhabu ndogo na penalti, kadi nyekundu na nyeupe (pia zipo za kijani na nyeupe), mpira kutoka nje na kadhalika.
Hizi takwimu wakati mwingine hutawala mijadala ya mchezo, kama vile matokeo ya mchezo baada ya kupulizwa filimbi ya mwisho sio muhimu sana.
Nakumbuka katika patashika nguo chanika moja ya mwaka 2018, wakati wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara pale Simba iliposhinda 1-0 dhidi ya Yanga, moja ya matukio ambayo mashabiki wengi wa vijiweni wa timu hizi walilolizungumzia ni Wanajangwani kutopata hata kona moja katika mchezo huu.
Baadhi ya mashabiki waliliona tukio hili kama sio la kawaida, lakini katika mchezo wa kandanda yapo matokeo mengi kama haya.
Katika baadhi ya michezo mara chache mpira ulitoka nje na kurushwa kutoka pembezoni ili uendelee na wakati mwingine mchezo ulikuwa maridadi na kusikika mwamuzi mara hache akipuliza filimbi.
Lakini kubwa zaidi ni kwamba katika dakika zote 90 za mchezo hapana hata timu moja iliyoweza sio tu kupata kona, lakni hata kutikisa wavu wa mwenzake kwa kufunga bao hata la kuotea wala la mkono.
Vile vile ipo michezo ambayo timu iliyomiliki mpira zaidi, badala ya kushinda ndiyo hatimaye iliyofungwa.
Kati ya michezo ya aina hii unaokumbukwa sana ni wa tarehe 13 Novemba, 1965 pale Leicester City ilipocheza na Manchester United.
Leicester ilishambulia sana na ilimiliki zaidi mpira kuliko wapinzani wao na kupata kona 34 wakati wenzao walipata sita.
Lakini filimbi ya mwisho ya mchezo ilipopulizwa Manchester United ilitoka uwanjani na furaha kubwa ikiwa na ushindi wa mabao 5-0.
Katika mchezo wa ligi daraja ya daraja la kwanza ya England uliofanyika
miaka 13 iliyopita klabu ya Everton ilipiga kona 16 wakati wapinzani wao Sunderland wlipata kona mbili tu.
Kilichowashangaza wengi ni kuiona Sunderland ambayo ilisakamwa sana katika mchezo huu iliibuka kuwa mshindi wa bao 1-0.
Mchezo mwingine unaotolewa mfano kama mmoja wa ile iliyomalizika kwa hata timu moja kufanikiwa kupata kona katika dakika zote 90 za mchezo na 3 za nyongeza ni wa Ligi Kuu ya England wa Agosti 21, 2010 kati ya Wigan Athletic na Chelsea.
Lakini filimbi ya mwisho ilipopulizwa Chelsea iliibuka na ushindi wa mabao 6-0 na kutangazwa mabingwa wa msimu ule.
Uzoefu umeonyesha michezo mingi ya kandanda katika miaka ya hivi karibuni huwa na jumla ya wastani wa kati ya kona 10 na 12 kwa timu zote mbili zilizoteremka uwanjani.
Hapo zamani ambapo mara nyingi mashambulizi yalifanyika pembezoni mwa uwanja wastani wa idadi ya kona katika kila mchezo ulikuwa kati ya 14 na 16.
Hata hivyo, zipo timu ambazo hutokea zikapata kona nyingi kupita kiasi, lakini zikashindwa kuitumia hata moja kwa kujipatia bao.
Kwa hakika kuchambua uzuri wa timu ya kandanda kwa asilimia ya kumiliki mpira, kona ilizopata, chenga ilizopiga, mipira ya adhabu ndogo au penalti ambazo timu ilipiga kama kuisifu kachumbari ya pilau iliyooza au kukisifia kile kinachoelezwa katika soka kama “twafungwa, lakini chenga twawala”.
Matokeo ya mchezo wowote ule wa kandanda siku zote huamuliwa kwa magoli yaliyofungwa na sio kwa mtindo wa chenga twawala, mipira ya kurusha, mipira ya adhabu au kona zilizopigwa au kadi za njano au nyekundu zilizotolewa na mwamuzi.
Kwa hapa Tanzania hatuweki kumbukumbu za michezo ya aina hii, lakini wenzetu katika nchi za Ulaya na Amerika ya Kusini wanazo za michezo ya zaidi ya karne moja iliyopita.
Tanzania tumeanza kujaribu, lakini bado tunasuasua na nadhani panahitajika juhudi zaidi za kuweka kumbukumbu.
Leo hii ukienda Shirikisho la Kandanda la Tanzania (TFF) ukauliza nani alikuwa nahodha wa timu ya Tanganyika ya miaka ya 1950 jawabu linaweza kuwa ni “hatujui”.
Mambo ni mabaya zaidi katika klabu zetu kwani ukitembelea zlabu zetu utaona picha chache tu za matukio ya karibuni, lakini siyo za wachezaji na viongozi wa zamani au maelezo mafupi ya historia ya klabu hizo.
Tubadilike na twende na wakati huku tukijua tuliyoyaona, tulipo na tunakoelekea.