Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Takwimu mabao ya Mayele

Mayele Pic Mabao Takwimu mabao ya Mayele

Sun, 10 Apr 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Mashabiki wa Yanga ukiwagusa tu watakwambia tulia hatujafungwa na yeyote katika Ligi Kuu msimu huu na wala haijulikani tutafungwa lini na kwa timu gani?

Ukiendelea kuwasumbua ndio watakukera zaidi wakikutajia jina la straika wao, fundi wa kutupia kambani Fiston Mayele, huku wakikumalizia na ile shangilia yake.

Straika huyo aliyesajiliwa msimu huu kutoka AS Vita ya DR Congo, amekuwa tishio kwa mabeki na makipa wa timu pinzani kwa namna anavyofunga mabao yake wakati mwingine katika mazingira magumu.

Pia ni mchezaji anayeonekana anaijua vyema kazi yake ya kufunga kwa takwimu zinazoonyesha kwa sasa katika Ligi Kuu Bara ikiwa imesaliwa na raundi 11 tu za mechi kabla ya ligi kufikia tamati.

Mayele amekuwa katika moto mkali kwenye ligi akifunga mabao 11 na kuongoza orodha ya wafungaji, akiasisti mabao tatu, ikiwa na maana amehusika na mabao 14 kati ya 33 iliyonayo Yanga inayoongoza msimamo kwa pointi 51 baada ya mechi 19.

Kasi ya mshambuliaji huyo ni kama ameshindikana kwani amekuwa tishio kwelikweli, huku takwimu zikionyesha hana bao hata moja la kubahatisha la pigo la penalti.

Mwanaspoti limekutengenezea orodha ya mabao ya mkali huyo na kuonyesha namna alivyo balaa kwa mabeki na makipa wa timu pinzani kwani kila anapokabwa kibabe ndipo anapowatoa nishai kwa kutupia kambani kisha anatetema.

SABA YA MGUU WA KULIA

Kwenye mechi 19 ambazo Yanga imeshacheza mpaka sasa, Mayele amefunga mabao 7 kwa mguu wa kulia, kati ya mabao yake 11, ukiwa ndio mguu alioutumia kufunga mabao mengi zaidi.

Mayele, mabao hayo ya mguu wa kulia amezifunga Mtibwa Sugar, Dodoma jiji, Biashara United, Mbeya Kwanza, Azam na KMC.

KUSHOTO BAO MOJA

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 27, ameutumia mguu wake wa kushoto kufunga bao moja tu, ambalo aliwafunga Geita Gold ugenini, Yanga ikishinda kwa bao hilo.

KICHWA MATATU

Upande mwingine Mayele amekitumia kichwa chake kufunga mabao 3 na mawili kati ya hayo, ameyafunga katika mchezo mmoja dhidi ya Kagera Sugar, Yanga ikiwa nyumbani ikishinda kwa mabao 3-0 huku lingine akiwafunga Coastal Union.

SAIDO, DJUMA WAPISHI

Wapishi wakubwa wa mabao ya Mayele ni beki Mkongomani mwenzake Djuma Shaban na Mrundi mkongwe Said Ntibazonkiza ‘Saido’, ambao kila mmoja amemtengenezea mshambuliaji huyo mabao 3.

Wengine waliompa pasi za mabao Mayele ni beki Yassin Mustapha, kiungo Feisal Salum ‘Fei toto, ambao kila mmoja amempa pasi mbili za mabao, huku Kibwana Shomari akimpikia bao moja.

DJUMA NA MABAO MAKALI

Hata hivyo, Djuma amejitofautisha na Saido akimpa pasi mbili ambazo Mayele amezitumia kufunga mabao ya kideoni kwa mtindo wa kubinuka sarakasi (acrobatic), akizifunga Biashara United na lile dhidi ya Azam alilofunga wiki hii.

MECHI SITA ZA KIBABE

Upande mwingine ni kwamba Mayele kuna mabao ambayo ameyafunga, yakiihakikishia ushindi timu yake katika mbio zao za kuusaka ubingwa msimu huu.

Yanga, ikiwa ugenini dhidi ya Azam ikishinda kwa mabao 2-1, bao la Mayele liliihakikishia timu yake ushindi huku wakivuna Sh50 milioni za posho ya ushindi huo muhimu.

Mshambuliaji huyo, aliwafunga tena bao pekee Geita Gold ugenini likiipa Yanga ushindi muhimu wa kuendelea kusalia juu katika msimamo wa ligi.

Yanga iliichapa Kagera Sugar nyumbani kwa mabao 3-0 na Mayele alifunga mabao mawili ya kwanza, ambayo yaliihakikishia ushindi timu yake.

Mayele tena, aliwahihikishia ushindi Yanga, ilipokuwa ugenini dhidi ya Mtibwa Sugar, ambapo katika ushindi wa mabao 2-0, alifanikiwa kufunga la pili ambalo liliwazima wenyeji wao akitanguliwa na Saido.

Yanga ikiwa nyumbani ikiwakaribisha Dodoma Jiji, ikishinda kwa mabao 4-0, mshambuliaji huyo alifunga bao la kwanza kwa timu yake kisha wengine kufuatia wakiwemo Jesus Moloko, Fei Toto, na Khalid Aucho.

KMC ikiwa nyumbani ilipokea kipigo cha mabao 0-2 na Mayele akatangulia kufunga bao la kwanza na mchezo mwingine ni dhidi ya Azam nyumbani, Yanga ikishinda kwa idadi kama hiyo akitangulia kufunga bao la kwanza.

HANA PENALTI

Akiwa anaongoza kwa ufungaji, akifunga mabao hayo 11 lakini Mayele hajafunga bao lolote kwa njia ya penalti mpaka sasa, akifunga kwa kutumia krosi na pasi za kawaida.

ASISTI TATU

Ukiacha kufunga, sura nyingine ya ubora kwa Mayele ni kuwatengenezea wenzake, ambapo pia ametoa asisti tatu za mabao, akiwatengenezea Fei toto dhidi ya KMC ugenini, Dickson Ambundo Yanga ilipocheza dhidi ya Polisi Tanzania na Saido dhidi ya Kagera Sugar.

TANO ZILIZOMBANA

Kwenye mechi 19 ambazo Yanga imeshacheza mpaka sasa, Mayele amefanikiwa kuzifunga timu 9 na kuna timu 6 bado hajafanikiwa kuzifunga na zote zimebakiza mchezo mmoja dhidi ya timu yake ya Yanga, ambazo ni Ruvu Shooting, Prisons, Namungo, Mbeya City, Polisi na Simba ambao aliifunga katika mchezo wa Ngao ya Jamii pekee.

MSIKIE MWENYEWE

Licha ya kuwa kinara wa mabao, Mayele alikaririwa hivi karibuni akisema vita ya kubeba tuzo bado mbichi, lakini anachoshukuru ni kuona anaendelea kutumia kila nafasi anayoipata kwa faida ya timu yake.

“Ligi ni ngumu na nawaheshimu wachezaji wote tunaofukuzana kwani nafasi ipo wazi kwa kila mmoja, lakini nafurahi nikifunga kwani ndio kazi yangu.”

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz