Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Takwimu Hizi! Hapo Brazil unamtoa nani?

Brazil Pic Alisson Becker na Ederson

Fri, 11 Nov 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Mapema wiki hii kikosi cha Timu ya Taifa ya Brazil kilitajwa huku mjadala mkubwa ukiwa ni kuachwa kwa staa timu huyo Roberto Firmino.

Staa huyo ameachwa kwenye kikosi hicho cha wachezaji 26 ambacho kitaanza kujindaa hivi karibuni kwenye fainali za Kombe la Dunia.

Eneo la ushambuliaji la Brazil limesheni mafundi kama Antony, Gabriel Jesus, Gabriel Martinelli, Neymar, Pedro, Raphinha, Richarlison, Rodrygo na Vinicius Jr ambao ndio wamechaguliwa badala ya Firmino.

Watu wengi wamekuwa wakilaumu kwanini staa huyo kaachwa licha ya ubora wake mkubwa ambao amewahi kuuonyesha kwenye taifa hilo.

Makala hii inakuletea uchambuzi wa kina juu ya takwimu na viwango vilivyosababisha mastaa kuchaguliwa kwenye timu hiyo na kwanini wengine ikiwa pamona na Firmino hawakupata nafasi.

Richarlson, Kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Ghana alifunga mabao mawili, jamaa ni miongoni mwa mastraika wenye uwezo mkubwa wa kufunga ikiwa watapewa pasi nzuri za mwisho, akiwa na Tottenham msimu huu amefunga mabao mawili na kutoa asisti tatu.

Staa wa Arsenal, Gabriel Jesus amejumuishwa baada ya kuachwa hapo awali, kwa sasa yeye ndiye staa wa eneo la ushambuliaji pale Arsenal.

Rekodi zinaonyesha tangu aanze kuitumikia Timu ya Taifa ya Brazil mwaka 2016 amefunga jumla ya mabao 16 kwenye mechi 56.

Msimu huu yupo kwenye kiwango bora, amecheza mechi 18 za michuano yote na kufunga mabao matano sambamba na asisti saba na kuisaidia Arsenal iendelee kusalia kwenye kilele cha msimamo wa Ligi Kuu England.

Jamaa amechaguliwa kutokana na kiwango chake cha sasa sambamba na historia ya Ligi Kuu England msimu huu.

Ilikuwa kawaida kumuona Neymar akijumuishwa kwenye kikosi kutokana sababu, moja, ni miongoni mwa wachezaji wachache ambao wapo kwenye timu hiyo ya taifa kwa zaidi ya miaka 10, hivyo pia anaongeza uzoefu kwenye kikosi.

Vilevile amekuwa na msimu bora sana akiwa na PSG amecheza mechi 19 amefunga mabao 15 na kutoa asisti 12. Akiitumikia Brazil tangu alipoanza mwaka 2010, Neymar katika michezo 121 na kufunga mabao 75.

Vinicius Jr na Rodrygo hawa wote ni wachezaji wa kutumainiwa wa Real Madrid, wanaonekana kuwa ndio kizazi kijacho cha Brazil kutokana na ubora ambao wamekuwa wakiuonyesha.

Lakini mbali ya kuchaguliwa kama mpango wa muda mrefu wa taifa hilo mastaa hawa pia wameonyesha viwango bora pale Madrid.

Ukianzia kwa Vinicius amefunga mabao 10 na kutoa asisti tano kwenye mechi 20 za michuano yote alizocheza tangu mwanzo wa msimu huu na Rodrygo amefunga mabao saba na kutoa asisti tano kwenye mechi 18 za michuano yote.

Antony ambaye amejiunga na Manchester United msimu huu ameanza vizuri hali iliyochangia sana yeye kujumuishwa kwenye kikosi hicho kwani amefunga mabao matano na kutoa asisti mbili kwenye mechi 14 za michuano yote.

Kiwango kama hiki pia amekionyesha Gabriel Martinelli akiwa na Arsenal, mbali ya ubora wa Jesus jamaa amekuwa na faida nyingi kwenye kikosi.

Kwanza anaweza kucheza kama winga vilevile mshambuliaji wa kati, jambo hili limechangia sana kumpa nafasi na kuwanyima nafasi wengine kwa sababu kocha anaamini anaweza akamtumia kwenye maeneo mengine ikiwa kutakuwa na majeraha. Msimu huu amefunga mabao matano na kutoa asisti mbili kwenye mechi 18 za michuano yote.

Raphinja ambaye pia ametua Barcelona katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi yumo kwenye kikosi cha Brazil na kilichombeba zaidi ni kiwango bora alichoonyesha akiwa kwenye timu hiyo.

Kwanza amecheza mechi 11 na kufunga mabao matano tangu aanze kuitumikia Brazil mwaka jana, vilevile msimu huu akiwa na Barcelona amecheza mechi 18 akifunga mabao mawili na kutoa asisti nne.

MAKIPA

Alisson Becker vs Ederson Moraes

Makipa wote hawa wanacheza Ligi Kuu England na wanapata nafasi kwenye vikosi vya kwanza vya timu zao, Becker amekuwa kipa wa kudumu wa Liverpool kama ilivyo kwa Ederson na Manchester City.

Yeyote atakayeanza kwenye kikosi hiki anaweza kufanya vizuri katika eneo hilo kutokana na ubora ambao waliouonyesha kwenye timu zao za taifa.

MABEKI

Dani Alves vs Danilo

Kwa upande wa Dani Alves ni mmoja kati ya wachezaji wazoefu akiwa amecheza jumla ya mechi 125 za Timu ya Taifa ya Brazil akiwa amecheza jumla ya fainali nne za Kombe la Dunia kuanzia mwaka 2006 hadi sasa.

Mbali ya uzoefu wake, eneo hilo la beki ya kulia, linaongezewa nguvu pia na Danilo beki kisiki wa Juventus ambaye tangu msimu huu uanze ameitumikia mechi zote za michuano hiyo ambayo timu hiyo imecheza.

Ikiwa Alves atapata shida anaweza kuanza fundi huyu ambaye pia ana uzoefu. Lakini kimsingi eneo hili la beki wa kulia pia lina wachezaji hatari ambao mmoja akitoka anayeingia pia hutoa kiwango sawa au zaidi ya aliyetoka.

Alex Sandro vs Alex Telles

Baada ya Marcello, mastaa hawa ndio wanaonekana kuchukua mikoba yake. Telles amekuwa akipata sana nafasi kwenye mechi za kirafiki za hivi karibuni.

Lakini ikiwa yeye atakosekana kuna beki mwingine kisiki na bora Alex Sandro ambaye anaweza kucheza eneo hilo na kuonyesha kiwango bora.

Thiago Silva vs Gabriel Magalhaes

Silva hadi sasa amecheza jumla ya mechi 107, pia ndiye kapteni wa Timu ya Taifa ya Brazil, ameshinda karibu kila taji kubwa akiwa na klabu tofauti na ana uzoefu wa kutosha na fainali za Kombe la Dunia kwani amecheza mara tatu tofauti.

Kuna asilimia kubwa akawa anaanza kwenye eneo la beki namba nne ama akachezeshwa bwana mdogo Magalhaes ambaye ni tegemeo pale Arsenal kwa msimu huu ambapo ameiwezesha timu hiyo kukaa kileleni hadi sasa.

Marquinhos vs Eder Militao

Hapa kuna beki kisiki wa PSG, Marquinhos ambaye amecheza fainali hizi mara mbili, tangu aanze kuitwa rasmi timu ya taifa mwaka 2013.

Miltao naye japokuwa hapati nafasi ya kutosha kwenye kikosi cha kwanza cha Real Madrid, bado haiondoi ukweli kwamba ni miongoni mwa mabeki bora ambao pia wanaweza kucheza eneo hili ikiwa Eder Militao ataumia au kupata majanga yoyote.

Kwa sasa chaguo la kwanza la kocha ni Marquinho na ndiye anayeonekana kupata nafasi kubwa ya kucheza hata kwenye mechi za kirafiki.

KIUNGO

Casemeiro na Fabinho hayaitajiki maelezo mengi kuelezea ubora ambao wamekuwa nao kwenye kipindi cha miaka minne au mitano hadi sasa.

Viungo hawa wamefanya kazi kubwa kwenye timu zao, Casemeiro aliiwezesha Real Madrid kuchukua mataji manne mfululizo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya sawa na Fabinho ambaye ni kiungo tegemeo pale Anfield.

Wamekuwa na uzoefu wa kutosha kwenye michuano mbalimbali hali iliyosababisha Tete avutiwe na kuwajumuisha kwenye kikosi, vilevile viwango vyao wakiwa na timu zao msimu huu pia vimewabeba.

Ubora wa Guimares akiwa na Newcastle United umesababisha timu nyingi za England kutamani kumsajili dirisha lililopita la majira ya kiangazi, amefunga mabao matatu na kutoa asisti mbili katika mechi 12 , lakini uwezo wake wa kukaba kama kiungo mkabaji ni mkubwa sana.

Kwa upande wa Fred, kocha anaonekana kumkubali sana licha ya kutofanya vizuri akiwa na Man United. Fred ni miongoni mwa mastaa wanaofanya vizuri wanapokuwa na timu yao ya taifa.

Hivyo mbali ya panda shuka zake pale Man United kocha ndiye anayemwamini zaidi kwenye eneo la kiungo.

Paqueta ana uwezo wa kucheza zaidi ya nafasi moja kwani hucheza pia kama kiungo wa pembeni lakini eneo lake la asili zaidi hucheza kama mshambuliaji namba 10, kwenye mechi kadhaa za kirafiki kocha amekuwa akimtumia Paqueta kama kiungo wa pembeni na muda mwingine namba 10 na amekuwa akionyesha kiwango bora.

Moja ya sababu zilizochangia sana sana kuitwa kwake ni hii.

MAENEO MENGINE

Hakukuwa na upinzani mkali eneo la golikipa, makipa wote bora kutoka Brazil wanacheza Ligi Kuu England.

Ederon amecheza mechi sita za Ligi Kuu England msimu huu bila ya kuruhusu bao na Allison amecheza mechi nne bila ya kuruhusu bao, Weverton anaingia kama kipa namba tatu ameitwa kwa sababu ya uzoefu wake na utamaduni wa Brazil ambao huwa ni lazima wawe na wachezaji kutoka ligi yao ya ndani wakiwamini huongeza baraka na kusababishwa wafanye vizuri kwenye mashindano kama ilivyokuwa kwa Everton Ribeiro kwenye eneo la kiungo.

Eneo la ulinzi ambalo lina Dani Alves, Danilo, Alex Sandro, Alex Telles, Bremer, Eder Militao, Marquinhos na Thiago Silva, halikuwa na changamoto sana.

KIKOSI KAMILI

Makipa: Alisson, Ederson, Weverton. Mabeki: Dani Alves, Danilo, Alex Sandro, Alex Telles, Bremer, Eder Militao, Marquinhos, Thiago Silva. Viungo: Bruno Guimaraes, Casemiro, Everton Ribeiro, Fabinho, Fred, Lucas Paqueta.

Washambuliaji: Antony, Gabriel Jesus, Gabriel Martinelli, Neymar, Pedro, Raphinha, Richarlison, Rodrygo, Vinicius Jr.

Chanzo: Mwanaspoti