Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tajiri wa timu yako Ligi Kuu England unamjua?

Sheikh Mansour Mmiliki wa Klabu ya Man City, Sheikh Mansour

Thu, 19 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Bilionea, Sir Jim Ratcliffe amejawa hamu ya kumiliki asilimia 25 za hisa za klabu ya Manchester United.

Na kama hilo litatimia, basi atakuwa kwenye orodha ya moja ya wamiliki matajiri wa klabu za Ligi Kuu England.

Ratcliffe na Sheikh Jassim walikuwa kwenye vita kali ya kujaribu kuinunua Man United kutoka kwenye mikono ya umiliki wa familia ya Glazer.

Lakini, tajiri wa Qatar, Sheikh Jassim alitaka kuinunua Man United jumla kwa ofa ya Pauni 5 bilioni, ambayo iligomewa na familia ya Glazer waliotaka Pauni 6 bilioni.

Hilo lilimfanya Ratcliffe aje kivingine na ofa ya Pauni 1.4 bilioni ili kumiliki asilimia 25 ya hisa za klabu hiyo ya Old Trafford. Je, dili hilo litakapokamilika, bilionea huyo wa Uingereza atashika namba ngapi kwenye orodha ya wamiliki matajiri wa Ligi Kuu England?

1. Newcastle United - Mohammed bin Salman, Pauni 538 bilioni

Kwa mbali sana kwenye namba moja ipo Saudi Arabia Public Investment Fund. Kampuni hiyo, PIF imewekeza kwa niamba ya serikali ya Saudi Arabia, huku utajiri wa kampuni hiyo ni Pauni 538 bilioni.

Mwanamfalme wa Saudia, Prince Mohammed bin Salman ndiye msimamizi wa kampuni hiyo ya Public Investment Fund, ambao ni ndiyo inayomiliki klabu ya Newcastle United.

Wamiliki wengine wa Newcastle United ni Reuben Brothers (David na Simon), wanaomiliki asilimia 10 ya hisa, zenye thamani ya Pauni 24 bilioni.

Mrembo aliyesaidia dili la kuuzwa Newcastle, Amanda Staveley na mumewe Mehrdad Ghodoussi nao wapo kwenye orodha ya wamiliki wa Newcastle na utajiri wao unatajwa kuwa Pauni 110 milioni.

2. Man United - Sir Jim Ratcliffe - Pauni 29.7 bilioni

Ndiyo hivyo, kama Sir Jim atafanikiwa kupata asilimia 25 za hisa za kuimiliki Manchester United, basi timu hiyo itakuwa na tajiri namba mbili kwa watu wenye pesa ya kutosha kwenye Ligi Kuu England.

Shabiki huyo wa Man United tangu enzi za utoto wake amepiga mabilioni ya pesa kupitia kampuni yake ya Ineos, anamiliki hisa za klabu ya Nice ya Ufaransa, Lausanne ya Uswisi na timu ya F1 ya Mercedes.

Kwa mujibu wa Sunday Times Rich List, utajiri wa Ratcliffe umekuwa kwa Pauni 6 bilioni kuanzia mwaka 2022 na sasa ana mkwanja unaokadiriwa kuwa Pauni 29.7 bilioni.

Awali aliwasilisha ofa ya kuinunua Chelsea mwaka 2022 kabla ya kuhamia mipango yake Man United. Familia ya Glazer itaendelea kuwa wamiliki wakuu wa Man United na wao utajiri wao unakadiriwa kuwa Pauni 3.9 bilioni.

3. Man City - Sheikh Mansour - Pauni 17 bilioni

Sheikh Mansour aliinunua Manchester City, Septemba 2008 na amefanikiwa kuibadili na kuwa timu ya mataji, ikiwamo kubeba mataji matatu makubwa kwenye msimu wa 2022-23.

Mansour ametokea kwenye familia ya kifamle huko United Arab Emirates, pia ni makamu wa rais na waziri mkuu wa nchi hiyo ya Ghuba.

Anatajwa kuwa na utajiri wa Pauni 17 bilioni kupitia kwenye kampuni zake za petroli, licha ya kwamba anaweza kuwa na pesa nyingi zaidi kama akijumlisha na urithi wake wa Pauni 560 bilioni kutoka kwenye familia ya Al Nahyan.

Sheikh Mansour amekuwa na klabu nyingine kadhaa kupitia kampuni yake ya City Football Group na amewekeza pia kwenye kampuni mbalimbali za habari na maeneo mengine.

4. Arsenal - Stan Kroenke - Pauni 12 bilioni

Kwenye nafasi ya nne yupo tajiri wa Arsenal, bilioni Stan Kroenke na mkwanja wake wa Pauni 12 bilioni. Tajiri huyo ametengeneza pesa nyingi kupitia biashara ya nyumba, hasa maduka na makazi ya watu. Na amekuwa akijihusisha na michezo na burudani kwa muda mrefu, akimiliki pia klabu za LA Rams, Denver Nuggets na Colorado Rapids - na anamiliki enkari 535,000 za mifugo, ikiwa ni kubwa zaidi huko Marekani.

5. Fulham - Shahid Khan - Pauni 9.7 bilioni

Kama ilivyo kwa Kroenke, Shahid Khan naye pia amekuwa na uwekezaji kwenye michezo ya Marekani, akimiliki timu ya NFL, Jacksonville Jaguars. Ni mmiliki mwenza pia wa All Elite Wrestling kwa kushirikiana na mwanaye Tony. Pesa nyingi za Khan amezitengeneza kupitia biashara ya kuuza vipuri kupitia kampuni ya Flex-N-Gate na anatajwa ni mtu tajiri zaidi mwenye asili ya Pakistani.

6. Aston Villa - Nassef Sawiris - Pauni 5.8 bilioni

Nassef Sawiris aliwekeza Aston Villa mwaka 2018 baada ya mechi ya mchujo dhidi ya Fulham. Ni bilionea kijana zaidi wa Misri, akitokea kwenye familia ya watoto watatu ya Onsi Sawiris na baba yake alianzisha kampuni ya uhandishi na ujenzi ya Orascom.

Sawiris Jr amekuwa akishirikisha katika biashara za familia na anamiliki hisa kwenye kampuni ya adidas. Wes Edens naye pia anamiliki Aston Villa, sambamba na timu ya mpira wa kikapu ya NBA, Milwaukee Bucks - anaripotiwa ana utajiri wa Pauni 3.4 bilioni.

7. Crystal Palace - Josh Harris - Pauni 5.7 bilioni

Harris anamiliki asilimia 18 tu ya hisa za Crystal Palace, lakini ndiye mtendaji mkuu wa mambo yote yanayoendeshwa kwenye kikosi hicho cha Selhurst Park, ndiye mmiliki wa kampuni Apollo Global Management.

Mmarekani huyo anatimu kadhaa za NBA, NHL na NFL na amekuwa akijihusisha pia na masuala ya mbio za pikipiki. Steve Parish, David Blitzer na John Textor nao ni wamiliki pia wa hisa kwenye klabu hiyo ya Selhurst Park.

Kampuni ya Textor ya Eagle Football Holdings Limited inamiliki pia timu za Botafogo de Futebol e Regatas, Olympique Lyonnais, OL Reign na RWD Molenbeek.

8. Joe Lewis - Tottenham - Pauni 5 bilioni

Joe Lewis mara ya kwanza kuingia kwenye biashara ilikuwa kipindi alipokuwa akimsaidia baba yake kwenye kampuni yake ya masuala ya mapishi na mapambo kabla ya kuingia kwenye biashara ya pesa. Kwa sasa ana utajiri wa Pauni 5 bilioni na ndiye mhusika mkuu wa Tavistock Group iliyowekeza kwenye zaidi ya kampuni 200 katika nchi 15 duniani.

Baadhi ya kampuni hizo ikiwamo ya ENIC Group, anayomiliki kwa kushirikiana na Daniel Levy, mwenye utajiri wa Pauni 500 milioni na ndiyo inayomiliki Tottenham Hotspur.

9. Chelsea - Todd Boehly - Pauni 5 bilioni

Boehly anatambana na hali yake kwenye kikosi cha Chelsea baada ya kuinunua klabu hiyo yenye maskani yake Stamford Bridge kwa mkwanja kiasi cha Pauni 4.25 bilioni, Mei 2022.

Mfanyabiashara huyo na mwekezaji anaziendesha pia Eldridge Industries na Hollywood Foreign Press Association. Kuonyesha matumizi ya pesa kwake haijawahi kuwa tatizo, bosi huyo alitumia Pauni 1 bilioni kwenye usajili ndani ya madirisha matatu tu tangu alipoinunua klabu hiyo.

Hata hivyo, si Boehly pekee anayeonyesha jeuri ya pesa peke yake, kwa sababu Chelsea anaimiliki kwa ushirika na washirika wenzake Behdad Eghbali (Pauni 3.1 bilioni), Hansjoerg Wyss (Pauni 3.9 bilioni) na Mark Walter (Pauni 4.7 bilioni).

10. Liverpool - John Henry - Pauni 4.2 bilioni

John W Henry ndiye kiongozi wa kampuni ya Fenway Sports Group ambayo inayomiliki Liverpool na Boston Red Sox.

Henry alikuwa akiwa ni mtoto wa mkulima wa maharagwe ya soya na ametumia kampuni ndogondogo kufikia kwenye ubilionea.

Biashara zake nyingine ikiwamo gazeti la Boston Globe, wakati patna wake kwenye masuala ya kibiashara, Tom Werner anaripotiwa kuwa na utajiri wa Pauni 1.4 bilioni. Werner ambaye ameibukia kwenye kampuni ya ABC ametengeneza pesa nyingi kupitia vipindi vya televisheni ikiwamo The Cosby Show.

11. West Ham - Daniel Kretinsky - Pauni 4 bilioni

Daniel Kretinsky alinunua hisa zake za kuimiliki West Ham, Novemba 2021, alipochukua asilimia 27 ya hisa za klabu hiyo sambamba na mshirika wake Pavel Horsky.

Mfanyabiashara huyo wa Czech ndiye mwanyekiti wa kampuni kubwa ya nishati huko Ulaya Kati, EPH na ndiye mwenyekezaji mkuu wa Royal Mail.

Anamiliki pia Sparta Prague huku pesa za nyingi akiwekeza kwenye nishati, mawasiliano, vyombo vya habari na soka. David Sullivan ndiye mmiliki mkuu wa West Ham United baada ya kifo cha David Gold. Utajiri wa Sullivan kwa sasa ni Pauni 1.1 bilioni.

12. Nottingham Forest - Evangelos Marinakis - Pauni 2.5 bilioni

Tajiri huyo milioni wa kampuni ya vyombo vya habari huko Ugiriki, Alter Ego Media, Evangelos Marinakis ndiye anayemiliki klabu ya mpira wa miguu ya Nottingham Forest. Alitengeneza pesa nyingi kwenye shughuli zake za kampuni za usafirishaji majini Capital Maritime & Trading Corp - ambayo inamiliki zaidi ya meli 100. Sasa bosi huyo ndiye mmiliki na mwenyekiti wa klabu ya Forest pamoja na Olympiacos ya Ugiriki.

13. Wolves - Guo Guangchang - Pauni 2.4 bilioni

Guangchang ni mkurugenzi mtendaji mkuu wa Fosun, kampuni za Kichina. Kampuni hiyo iliinunua Wolves kutoka kwa Steve Morgan kwa Pauni 45 milioni mwaka 2016 na hapo aliisaidia timu hiyo kupanda kwenye Ligi Kuu England, ikifika nusu fainali ya Kombe la FA na Europa League.

Guangchang anaiongoza Wolves sambamba na mabosi wenzake wa Fosun, ambao ni mabilionea Wang Qunbin na Liang Xinjun.

14. Everton - Farhad Moshiri - Pauni 1.6 bilioni

Alitajwa namba 112 kwenye orodha ya matajiri iliyotangazwa na Sunday Times Rich List, kipato cha Moshiri kwa sasa kinatajwa ni Pauni 1.6 bilioni.

Ni mwenye hisa na mwenyekiti wa USM, kampuni ya Russia inayojihusisha na masuala ya madini na mawasiliano. Moshiri alikuwa na hisa pia Arsenal, lakini aliziuza Februari 2016 ili kupata pesa za kuongezea kwenye manunuzi yake ya Everton.

15. Bournemouth - Bill Foley - Pauni 1.3 bilioni

Foley anamiliki kampuni ya Fidelity National Financial. Mfanyabiashara huyo mashuhuri ni bosi pia wa Black Knight Sports & Entertainment inayomiliki timu ya mchezo wa NHL, Vegas Golden Knights na aliinunua Bournemouth kutoka kwa Maxim Demin mwaka 2022.

Foley aliungana na washirika wake Nullah Sarker na mwigizaji wa Hollywood, Michael B Jordan katika kampuni ya Turquoise Bidco Limited, ambayo ndiyo mmiliki wa klabu hiyo maarufu kama Cherries.

16. Brighton - Tony Bloom - Pauni 500 milioni

Bloom amepata utajiri wake kwenye kampuni za kamari na kubeti na mchezaji maarufu wa poka. Amejitengenezea pesa zaidi na kufikia utajiri huo wa Pauni 500 milioni kupitia biashara nyingi tofauti na mmiliki pia wa mbio za farasi.

Shabiki huyo wa siku nyingi wa Brighton, Bloom aliinunua klabu ya mapenzi yake mwaka 2009 na tangu kipindi hicho imekuwa ikifanya vyema ndani ya uwanja na sasa ikitamba kwenye Ligi Kuu England na hata kwenye soka la Ulaya.

17. Brentford - Matthew Benham - Pauni 252 milioni

Kama Bloom, Benham ni shabiki mkubwa wa klabu anayoimiliki. Amepata utajiri wake na kupiga pesa nyingi kupitia michezo ya kamari na ni mmiliki wa Smartodds na Matchbook, ambazo ni kampuni za kubeti.

Mhitimu huyo wa elimu ya fizikia kwenye chuo cha Oxford anafanya kazi kwenye taasis za kifedha huko London na aliinunua Brentford mwaka 2012 na kuihamishia klabu hiyo kwenye uwanja mpya.

Benham pia alikuwa mmiliki wa hisa nyingi wa FC Midtjylland ya Denmark, lakini aliuza hisa zake Agosti 2023.

18. Sheffield United - Abdullah bin Musa’ed - Pauni 164 milioni

Prince Abdullah kutoka Saudi Arabia ametajwa ni mmoja wa wajukuu 1,000 wa mfamle wa kwanza wa Saudi Arabia, Ibn Saud. Musa’ed amejitengenezea utajiri mwenyewe kupigia kampuni yake ya karatasi inayotengeneza karatasi chooni, jikoni na tishu na amewekeza zaidi Afrika Kaskazini na Mashariki ya Kati. Kampuni yake ina thamani ya Pauni 225 milioni- lakini alilipa Pauni 1 tu katika uwekezaji wake wa kwanza wa asilimia 50 za hisa kwenye klabu ya Sheffield United mwaka 2013.

19. Burnley - Alan Pace - Pauni 156 milioni

Alan Pace kupitia kampuni yake ya ALK Capital alinunua asilimia 84 za hisa za kuwa mmiliki wa klabu ya Burnley yenye maskani yake Turf Moor, Desemba 2020. Jambo hilo limemfanya mfanyabiashara huyo wa Marekani kuweka mwenyekiti mpya kwenye klabu. Pace amekuwa na kampuni ndogo nyingi huko Wall Street ikiwamo benki na taasisi za fedha, ikiwamo ile ya Citi yenye maskani yake New York.

20. Luton Town - Inamilikiwa na mashabiki

Mwisho kabisa ni timu ya Luton Town, ambayo inamilikiwa na kundi la mashabiki, ambalo limeamua kuitambulisha timu yao kama Luton Town Football Club 2020 Limited. Hiyo ina maana timu hiyo haina mmiliki mmoja mwenye pesa nyingi na ndiyo maana hata utajiri wake haufahamiki. Mwenyekiti wa klabu, David Wilkinson alipigiwa kura na wakurugenzi wenzake, wakati Gary Sweet ni mkurugenzi mtendaji mkuu. Utajiri wao haufahamiki.

Chanzo: Mwanaspoti