Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tajiri mpya Man United kuanza na hawa

IMG 5946 United UEFA.jpeg Tajiri mpya Man United kuanza na hawa

Tue, 14 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati tajiri Sir Jim Ratcliffe anadaiwa kuwa kwenye hatua za mwisho kuinunua Manchester United kuna taarifa nyingi zinazosambaa kwamba mabadiliko makubwa yatafanyika.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka The Sun inaelezwa kwamba Ratcliffe, 71, amepanga kubadilisha baadhi ya vitu ndani na nje ya uwanja mara tu baada ya kununua asilimia 25 kwa Pauni 1.3 bilioni kama inavyoelezwa.

The Sun inaeleza kwamba mipango ya tajiri huyo itaanzia Januari ambapo mastaa watatu Antony, Jadon Sancho na Anthony Martial wanatarajiwa kuondoshwa kikosini. Mbali ya kuondoa mastaa hao, ripoti zinadai Man United itashusha vyuma vingine kwa ajili ya maboresho na kuziba mapengo.

Mashetani wekundu hao ambao tangu kuondoka kwa Sir Alex Ferguson, wametumia Pauni 1.4 bilioni kwenye masuala ya usajili na kocha wa sasa Erik Ten Hag akiwa ametumia Pauni 374 milioni kati ya pesa hizo.

Ratcliffe amewahi kueleza kwamba ikiwa atapewa Man United hatohitaji kumwaga pesa bila ya mpangilio bali kwa utaratibu maalumu.

Moja kati ya maeneo ambayo yanaonekana kuwa changamoto kwenye kikosi cha Man United kwa msimu huu ni eneo la beki wa kati ambalo limechangiwa sana na kuumia kwa Lisandro Martinez anayetarajiwa kurudi mwisho wa mwezi ujao.

Katika dirisha lililopita Ten Hag alihitaji kusajili beki mmoja wa kati na staa aliyekuwa anatajwa zaidi alikuwa ni fundi kutoka Korea Kusini Kim Min-jae kabla hajajiunga na Bayern Munich.

Pia akataka kuipata huduma ya beki wa kati wa Nice, Jean-Clair Todibo lakini mwisho akampata Jonny Evans pekee.

Kwa mujibu wa tovuti ya Manchester Evening kuna uwezekano kwanza Todibo akatua kwani Ratcliffe ndio mmiliki wa Nice hivyo hakutokuwa na mambo mengi kwenye mazungumzo kwani ni kama kutoa pesa mfuko wa kulia kupeleka wa kushoto. Eneo jingine pia ni lile la kiungo na winga ambapo watahitajika mastaa watakaokuwa mbadala wa Antony na Sancho, hapo kwenye kiungo kuna jina la staa wa Monaco Youssouf Fofana.

Man United imekuwa ikihangaika kutaka kusajili mchezaji atakayekuwa na uwezo wa kuunganisha eneo la ulinzi na ushambuliaji wakati huo huo aifanye timu kutokuwa rahisi kuruhusu mashambulizi.

Fofana anatajwa kuwa mmoja kati ya wachezaji wenye wastani mzuri wa uzuiaji na kushambulia sambamba na kufikisha mipira kwenye eneo la mwisho.

Ikiwa atatua huenda ikaongeza ufanisi pia wa Sofyan Amrabat ambaye hadi sasa bado hajaonyesha makali yaliyotarajiwa na vigogo wa timu hiyo.

Fofana alisajiliwa na Paul Mitchell ambaye kwa sasa anadaiwa kuwa huenda akawa mkurugenzi wa ufundi wa Man United baada ya Ratcliffe kuchukua timu.

Vilevile tajiri huyu huenda akaidhinisha usajili wa beki wa pembeni ambaye kwa sasa anadaiwa kuwa ni beki wa Bayer Leverkusen, Jeremie Frimpong ambaye hivi karibuni ameongeza mkataba mpya wa kusalia Leverkusen hadi mwaka 2028.

Kwenye eneo la ushambuliaji tajiri huenda akaanza na Federico Chiesa ambaye huenda akauzwa kwa zaidi ya Pauni 52 milioni. Majina mengine ni Evan Ferguson na Pedro Neto.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: