Wachezaji wa Yanga furaha tupu kambini, ni baada ya kupewa ahadi ya kuongezewa bonasi kutoka kwa mdhamini wa timu hiyo, Bilionea Gharib Salim Mohammed (GSM).
Bonasi iliyoongezwa kwa ajili ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo Yanga wapo katika hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo mikubwa Afrika ambayo wanashiriki.
Jumatano iliyopita akaunti za wachezaji wote zilisoma mara baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Marumo Gallants ya Afrika Kusini, katika mchezo wa kwanza wa hatua ya nusu fainali ya kombe hilo uliochezwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar.
Mastaa hao wanatakiwa kwenda kupambana tena katika mchezo wa marudiano dhidi ya Marumo utakaopigwa Jumatano ijayo kwenye Uwanja wa Royal Bafokeng huko Afrika Kusini.
Taarifa ambazo tumezipata, bonasi hiyo waliyoongezewa ni kiasi cha 350Mil kutoka 250Mil waliyokuwa wakipewa katika kila mchezo nyumbani na ugenini.
Mtoa taarifa huyo alisema kuwa furaha na hamasa ya wachezaji imeongezeka kambini kutokana na ahadi hizo wanazoahidiwa kupewa kwa wakati mara baada ya ushindi wa mchezo husika.
“Kila mchezaji hivi sasa ana furaha kambini, kila mmoja akiwa na morali na hamasa ya kuipambania timu ili ipate matokeo mazuri kwa lengo la kupata bonasi hiyo inayotolewa kwa wakati.
“Hiyo ndio sababu ya morali ya wachezaji kuongezeka hivi sasa, viongozi wanajaribu kutumia pesa nyingi ili kuwaongezea hali ya kuipambania nembo ya klabu yake.
“Wachezaji hawataki kuona wakipoteza bonasi hizo, hivyo wameweka mikakati thabiti ya kupambana kwa kuanzia mchezo wa marudiano dhidi ya Marumo Gallants tutakapokuwepo ugenini Afrika Kusini tukiweka historia ya kufuzu fainali,” alisema mtoa taarifa huyo.
Rais wa Yanga, Injinia Hersi hivi karibuni alizungumzia hilo la bonasi kusema: “Bonasi ipo katika mikataba ya wachezaji wetu ambayo ni siri kati ya mchezaji na uongozi.
“Tumeweka utaratibu wa kuwapa bonasi wachezaji wetu kwa lengo la kuongeza morali na hali ya kuipambania timu, hivyo tutaendelea na utaratibu huo,” alisema Hersi.