Bilionea, Sir Jam Ratcliffe ametoa masharti ambayo yanaweza kuiweka Manchester United kwenye wakati mgumu wa kupata kocha mpya endapo itachukua uamuzi wa kumpiga chini Erik ten Hag.
Tajiri huyo mmiliki mpya wa Man United bado hajamfuta kazi Ten Hag, akitaka kwanza afikie makubaliano ya masharti yake na kocha mpya atakayekuwa tayari kwenda kufanya kazi huko Old Trafford.
Kieran McKenna, Mauricio Pochettino, Thomas Tuchel, Gareth Southgate, Thomas Frank na Graham Potter ni makocha waliopo kwenye rada za Man United wakiwindwa wakafanye kazi huko Old Trafford.
Lakini, tajiri ameambiwa na mashabiki asimfute kazi Ten Hag baada ya ubingwa wa Kombe la FA.
Na sasa, kocha yeyote atakayekuwa kwenye benchi la kuinoa timu hiyo itamlazimu kukubaliana na masharti ya bilionea Ratcliffe, ambayo anaamini yataipeleka mbele klabu hiyo.
1. Umri wa juu wa wachezaji watakaosajiliwa ni miaka 25.
2. Hakuna kusajili mastaa wenye majina makubwa.
3. Staili ya uchezaji itaamuliwa na mkurugenzi wa ufundi, Jason Wilcox.
4. Kocha ataomba nafasi gani ya mchezaji anayetaka asajiliwe na si kutaka mchezaji fulani.
5. Kocha atapewa majina matatu ya kila nafasi anayotaka mchezaji asajiliwe, atachagua mmoja.
Bilionea Ratcliffe anaamini kusajili wachezaji wenye umri wa miaka 25 kushuka chini watafanya kikosi kuwa fiti, chenye nguvu na kasi kubwa uwanjani. Bosi huyo hataki tena kusajili mastaa wenye majina makubwa kwa sababu hakuna ambacho wamefanya kwenye timu zaidi ya kuipa timu gharama kubwa kwenye matumizi ya pesa.
Man United imetumia Pauni 1.5 bilioni kwenye usajili wa mastaa wapya tangu Sir Alex Ferguson alipong'atuka 2013.
*MAKINDA AMBAO MAN UNITED
INAWEZA KUWASAJILI
-Michael Olise, miaka 22
-Jarrad Branthwaite, miaka 21
-Marc Guehi, miaka 23
-Jeremie Frimpong, miaka 23
-Joao Neves, miaka 19
-Benjamin Sesko, miaka 20
-Joshua Zirkzee, miaka 23