Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Taifa Stars ya Lunyamila na nidhamu ya Tshabalala

Tshabalala Simba Mohammed Hussein 'Tshabalala'

Mon, 3 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Wiki moja tu iliyopita chupa zilikuwa mezani stori zikiwa mdomoni. Nilikuwa na Edibily Jonas Lunyamila baa fulani Mbezi Beach tukipiga stori za zamani. Bahati iliyoje. Huyu ndiye wale kina Diego Maradona wa soka letu. Unamkumbuka Edibily? Alikuwa zaidi ya hatari ya kawaida.

Winga aliyekuwa mbele ya muda. Mpira aliokuwa anacheza wakati huo kama winga tumekuja kuuona miaka mingi baadaye. Winga wa kisasa. Hakai katika kibendera kupiga krosi, hapana. Anaingia katikati na kuzurura. Anapika mabao na anafunga. Leo tunaona kina Mo Salah wakicheza mpira ambao Eddy aliucheza miaka 25 iliyopita.

Tuliongea mambo mengi. Tulikumbuka matukio mengi. Tuliwakumbuka wachezaji wengi wa zamani na ubora wao. Wengine wametangulia mbele za haki na wengine wapo hai. Tulikumbuka mpira wetu ulikotoka, ulipo na unapokwenda. Nyakati zimekwenda wapi? Hatujui. Mambo mengi yamebakia kuwa historia tu.

Vijana wa siku hizi wanaona kama hadithi za kutunga, lakini ukweli katika matukio ya kushangaza ya namna ya wapi tulikotoka Edibily na mimi tulikumbushana mambo mengi ya ajabu. Moja kati ya matukio hayo ni pale timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars iliposafiri kwa basi kutoka Dar es Salaam hadi Lusaka kwa ajili ya kucheza pambano moja muhimu la kufuzu michuano ya CAF.

Kitu cha kushangaza. Timu ya taifa inasafiri kwa basi kilomita 1,531. Unatazamia watakuwa katika uchovu wa namna gani? Hata hivyo, walilazimika kusafiri kulitetea taifa. Walifungwa mabao 2-0 huku kipa wa Stars, Steven Nemes akiwa nyota wa mchezo. Unaweza kufikiria ni namna gani Stars ilielemewa kwa mashambuzi.

Edibily anakumbuka unyonge mwingine wa Stars katika pambano hilo. Mavazi. Walikuwa wamefikia hoteli moja na timu ya taifa ya Zambia. Walijiona namna gani walivyokuwa wamedhalilika kwa sababu kila walipojichanganya na wachezaji wa Zambia, wao Stars walijikuta wakiwa hawaeleweki zaidi. Kila mchezaji alikuwa amevaa kivyake. Wenzao walikuwa katika sare na Sandoz za kuvutia.

Kitu kibaya zaidi kilikuwa kinawasubiri katika safari yao ya kurudi. Wakapata ajali usiku wa manane baada ya dereva wa gari lao kuliingiza gari chini ya daraja. Hakuna aliyejeruhiwa vibaya wala kufariki dunia. Ikaanza kazi ya kujitafutia usafiri binafsi ambao ungeweza kuwafikisha katika mpaka wa Zambia na Tanzania pale Tunduma.

Waliondoka kwa mafungu mafungu kwa usafiri wa Malori usiku wa manane hadi wakafanikiwa kufika Tunduma ambako walipatiwa gari mbili aina ya Coaster zilizowafikisha Dar es Salaam. Ni zaidi ya miaka 25 sasa tangu jambo hilo litokee.

Edibily akanikumbusha jambo jingine. Wakati ule wachezaji wa Taifa Stars walipokuwa wanaweka kambi katika hosteli za Jeshi la Wokovu pale Kurasini karibu na Shule ya Jitegemee. Namna ambavyo walikuwa wanaishi katika chumba ambacho mchezaji mmoja akienda kujisaidia lazima wengine mkakae nje kwa sababu ya harufu.

Akanikumbusha namna ambavyo siku moja mchana wa mechi ngumu walijikuta wakitazamana na chakula cha aina ya Pilau. Kocha Sunday Kayuni alilazimika kuingia mtaani uswahilini kusaka chakula kingine. Unawezaje kumpeleka mchezaji acheze soka akiwa ameshiba pilau? Hata hivyo, hii ndio ilikuwa hali halisi.

Sasa nipo katika hoteli ya Le Meridian katikati ya Jiji la Jakarta, hapa Indonesia. Nyakati zimekwenda kasi. Taifa Stars imealikwa tu kucheza pambano la kirafiki dhidi ya timu ya taifa ya Indonesia. Mechi ilikuwa jana. Nimekumbuka mengi hasa wakati huu Taifa Stars ikiwa inajiandaa kucheza pambano la kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya wale wale Zambia Juni 11.

Unaweza kuamini Stars inaweza kupanda basi kwenda Lusaka? Nyakati hizi ambazo wachezaji wanadeka kiasi kwamba wachezaji wa Simba, Yanga na Azam hawawezi hata kwenda hapo Dodoma kwa basi. Wanakwenda kwa ndege. Na kudeka huku pia kumesababisha nikumbuke safari ya kina Edibily kule Lusaka.

Kibu Denis amedai amechoka na anataka kupumzika. Nadhani ana mamilioni mengi kutoka kwa klabu yake ya Simba baada ya kusaini mkataba mpya. Kuna wachezaji wengine pia ambao nimethibitishiwa wameichomolea safari kwa madai ya uchovu baada ya ligi mbalimbali kumalizika.

Wachezaji ambao sababu ya msingi inaeleweka na imeeleweka ni wale wa Yanga na Azam ambao jana walitarajiwa kucheza pambano la fainali michuano ya FA pale Unguja. Mastaa wengi wamechomoa. Staa mkubwa zaidi ambaye tuliwasili naye hapa ni Mohammed Hussein ‘Tshabalala’. Mwingine mkubwa aliyekuja baadae ni Himid Mao ‘Ninja’.

Wakati tukiwa Doha pale katika safari hii ya saa 14 hewani nilikuwa nikimwangalia kwa makini Tshabalala. Alikuwa ametulia katika kundi kubwa la vijana wengi ambao majina yao yameanza kuchomoza kwa sasa. Katika mazoezi yeye alikuwa miongoni mwa wachezaji ambao waliongoza kundi la kubeba goli moja kulihamishia katikati ya uwanjani.

Katika maelekezo ya makocha wake, Juma Mgunda na Hemed Morocco, huwezi kuamini Tshabalala ndiye alikuwa akisikiliza kwa makini zaidi. Ni kama vile alikuwa ameitwa katika kikosi cha Stars kwa mara ya kwanza. Kumbe ndiye alikuwa mchezaji mwenye mechi nyingi zaidi katika timu hiyo na kwa mechi za kimataifa kwa jumla. Fikiria idadi ya mechi za kimataifa ambazo ameichezea Simba.

Achilia mbali kwa nilichokiona, lakini watu wengi walio katika msafara pia waliniambia Tshabalala nidhamu imetulia. Kwa mfano, angesema anajisikia kifundo cha mguu kinamuuma na asingeweza kujiunga na timu ya taifa, nani angejali? Na hilo lingekuwa limetokea katika mechi ambayo haikuwa na maana kubwa sana kwa taifa.

Huyu ndiye Tshabalala. Haishangazi kuona kwa muda mrefu amekuwa akiichezea Simba kwa kiwango cha juu. Ana nidhamu ya hali ya juu ambao imejificha kimya kimya. Nidhamu ambayo wachezaji hawa wadekaji hawana. Nidhamu ambayo imemfikisha mbali na kumfanya kuwa mmoja kati ya mabeki bora wanaocheza soka la ndani Afrika kwa sasa.

Kumbe Tshabalala alikuwa tayari hata kuucheza mpira ule wa kina Lunyamila. Mpira wa kusafiri kutoka Dar es Salaam hadi Lusaka Zambia kwa basi. Wachezaji wa leo wanaona safari ya kwenda Jakarta kwa ndege ni mbali wangewezaje kusafiri saa 20 za basi kwenda Lusaka?

Lakini hii ndiyo dunia ya kisasa ambayo imekuwa ikilalamikiwa. Kila mahala wachezaji wamekuwa laini. Kwa jumla kila miaka inavyoyoyoma ndivyo mwanadamu anavyokuwa laini. Hata kesho nalazimika kuandika hapa kumjadili Kevin John ‘Mbappe’. Kwa nini amefeli Genk katika dunia hii ya leo? Inashangaza sana.

Chanzo: Mwanaspoti