Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Taifa Stars mwanzo wa ndoto Morocco

Taifa Starsssss Taifa Stars mwanzo wa ndoto Morocco

Sat, 18 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Safari ya kutimiza ndoto ya kufuzu kwa mara ya kwanza katika fainali za Kombe la Dunia kwa timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' inaanza leo katika mchezo wake wa kwanza wa kundi E ugenini dhidi ya Niger kwenye Uwanja wa Marrakech, Morocco kuanzia saa 1:00 usiku.

Matokeo ya ushindi katika mchezo huo utakaoanza saa 1:00 kwa muda wa Tanzania, yataifa Taifa Stars iongoze kundi E ambalo linajumuisha pia timu za Congo, Zambia na Morocco.

Taifa Stars inaingia katika mchezo wa leo ikiwa na historia nzuri ya utemi dhidi ya Niger ambapo katika mara mbili ambazo timu hizo zilikutana, imeshinda mara moja na nyingine ikitoka sare.

Mechi hizo zote mbili ambazo timu hizo zimekutana zilikuwa ni za kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 ambapo katika mchezo wa kwanza ambao Niger ilikuwa mwenyeji, matokeo yalikuwa ni sare ya bao 1-1 na katika mchezo wa marudiano hapa Dar es Salaam, Taifa Stars iliibuka na usnindi wa bao 1-0.

Niger wamekuwa hawana mwenendo mzuri katika mechi za kimashindano walizocheza katika miaka ya hivi karibuni na kuthibitisha hilo, timu hiyo haijapata ushindi katika mechi zake saba mfululizo zilizopita za mashindano tofauti, ikipoteza sita na kutoka sare moja.

Wageni Taifa Stars angalau wamekuwa na afadhali ambapo katika mechi saba zilizopita za mashindano tofauti, imeibuka na ushindi mara tatu, sare moja na imepoteza michezo mitatu.

Ikiwa na kundi kubwa la nyota wanaocheza soka la kulipwa nje ya Tanzania pengine kuliko nyakati zote ambazo ilishiriki mashindano hayo ya kufuzu, Taifa Stars inaonekana kuimarika zaidi safari hii ikiongezewa nguvu pia na uwepo wa wachezaji wa Simba na Yanga ambao hivi karibuni wametoka kuziongoza timu zao kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Lakini pia vijana hao wa Adel Amrouche wanaingia na hali nzuri ya kujiamini inayotokana na kuwa miongoni mwa timu 24 zilizofanikiwa kutinga Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) ambazo zitafanyika mwakani huko Morocco.

Kocha wa Taifa Stars, Adel Amrouche alisema kuwa licha ya ugumu ulio mbele yao wa kucheza mechi mbili ndani ya muda mfupi, mkakati wao ni kuhakikisha wanapata ushindi kwanza dhidi ya Niger.

"Namshukuru Mungu tumefika hapa na tuko salama kwa sababu hicho ndicho cha msingi na tunamshukuru Rais, Mama Samia (Suluhu Hassan) kwa kutupatia ndege maana hapa Afrika suala la usafiri kutoka Mashariki kwenda Magharibi sio jambo rahisi.

"Tutajitahidi kufanya kila kilicho ndani ya uwezo wetu kuwafanya watu wawe na furaha kwa sababu kwangu mimi, mpira wa miguu ni kwa ajili ya kuwafanya watu wapate furaha," alisema Amrouche.

Mshambuliaji Saimon Msuva alisema kuwa wamejiandaa vizuri na wamepanga kushinda mchezo wa leo ili uwaweke katika nafasi nzuri kwenye mashindano hayo.

"Kikubwa Watanzania watuombee. Tumecheza michezo kadhaa huko nyuma na matokeo wameyaona. Lakini pia kwa michezo ambayo iko mbele yetu, tunahitaji kushinda. Tupo hapa kuwakilisha nchi yetu. Kuna watu wengi wanatuangalia sisi na hatuhitaji kuwaangusha na ukiangalia Rais wetu anatuunga mkono na anaunga mkono michezo hivyo hatutaki kumuangusha," alisema Msuva.

Kikosi kinachoweza kuanza leo ingawa kunaweza kutokea mabadiliko kulingana na sababu mbalimbali kinategemewa kuwa na wachezaji Beno Kakolanya, Dickson Job, Novatus Dismas, Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Bacca, Himid Mao, Haji Mnoga, Sospeter Bajana, Mbwana Samatta, Saimon Msuva na Kibu Denis.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live