Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Taifa Stars mbona leo inawezekana tu

Taifa Stars Players Wachezaji wa Taifa Stars

Thu, 7 Sep 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Taifa Stars leo Alhamisi ni kufa au kupona tu wakati itakapokuwa kwenye kibarua kizito ugenini dhidi ya Algeria. Hakuna namna zaidi ya Stars kupata sare au kushinda mchezo huo wa mwisho wa Kundi F wa michuano ya kuwania ushiriki wa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023.

Ni kibarua kigumu lakini hakuna namna kinahitajika kupatiwa jibu na Taifa Stars leo itakapokutana na Algeria ugenini huko Annaba, Algeria kuanzia saa 4:00 usiku.

Historia ya kufanya vizuri nyumbani ambayo wenyeji Algeria wamekuwa nayo pamoja na ubora wa kundi kubwa la mastaa wanaounda kikosi chake, hapana shaka ni jambo linalowapa hofu Watanzania juu ya uwezekano wa timu yao ya taifa kupata matokeo inayoyahitaji katika mchezo wa leo ili iweze kufuzu Afcon lakini mwisho wa siku, nyota wa Taifa Stars wanapaswa kupambana kwa machozi, jasho na damu kuhakikisha hilo linatimia.

Ikiwa inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Kundi F na pointi zake saba, Taifa Stars inahitaji ushindi au sare ya aina yoyote ili iweze kutinga fainali za Afcon ambazo zitafanyika mwakani huko Ivory Coast, ingawa hata ikipoteza, inaweza kufuzu ikiwa Uganda itashindwa kupata ushindi dhidi ya Niger.

Kikosi kamili

Msafara wa Taifa Stars uliwasili juzi jijini Annaba ukitokea Tunisia ambako uliweka kambi ya maandalizi katika Mji wa Tabarka uliopo Kaskazini Magharibi mwa nchi hiyo ambao upo umbali wa kilomita 116 kufika Annaba, Algeria ambako mechi hiyo itachezwa.

Stars imefika Algeria ikiwa na kikosi kilichotimia baada ya kuongezewa nguvu na ongezeko la nyota wanaocheza soka la kulipwa nje wakiongozwa na nahodha Mbwana Samatta anayechezea PAOK ya Ugiriki na Novatus Dismas ambaye hivi karibuni amejiunga na Shakhtar Donetsk ya Ukraine.

Kikosi cha Stars jana kilifanya mazoezi ya mwisho katika Uwanja wa Mei 19, 1956 ambao utachezewa mechi hiyo.

Timu hiyo leo inaweza kuundwa na Beno Kakolanya, Dickson Job, Novatus Dismas, Ibrahim Bacca, Bakari Mwamnyeto, Himid Mao, Mzamiru Yassin, Mudathir Yahaya, Mbwana Samatta, Saimon Msuva na Morice Abraham.

Refa presha tupu

Mchezo huo wa leo utachezeshwa na refa wa kati Djindo Louis Houngnandande kutoka Benin huku Eric Ulric kutoka Benin akiwa msaidizi namba moja na msaidizi namba mbili amepangwa kuwa Jonathan Koffi wa Togo na refa wa akiba anatoka Benin ambaye ni Issa Mouhamed.

Houngnandande (38) amekuwa ni refa mwenye mkosi na timu zinazotoka katika ukanda wetu unaounda Baraza la Vyama va Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) na ikiwa Taifa Stars itaibuka na ushindi leo pengine itakuwa imemaliza nuksi za refa huyo.

Kumbukumbu zinaonyesha hakuna timu kutoka Ukanda wa Cecafa ambayo imewahi kupata ushindi katika mechi iliyochezeshwa na refa huyo ambapo amechezesha mechi sita (6) za timu kutoka ukanda huu na katika hizo, nne zilifungwa na mbili zilimalizika kwa matokeo ya sare tasa.

Timu ya Tanzania ambayo Houngnandande amewahi kuichezesha ni Yanga katika mchezo wake wa kwanza wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita ugenini dhidi ya Monastir ya Tunisia ambao wawakilishi hao wa Tanzania walipoteza kwa mabao 2-0.

Kuonyesha kwamba timu za ukanda huu zimekuwa na bahati mbaya pindi zikichezeshwa na Houngnandande, zimefunga bao moja tu katika mechi sita ambazo amechezesha huku zenyewe zikiruhusu nyavu zao kutikiswa mara kumi.

Historia yasakwa

Taifa Stars inasaka kufuzu Afcon kwa mara ya tatu baada ya kushiriki mara mbili fainali hizo, mara ya kwanza ikiwa ni 1980 zilipofanyika Nigeria na ikaja kufuzu tena mwaka 2019 zilipofanyika Misri.

Ikiwa hilo litatimia, Mbwana Samatta ataandika rekodi ya kuwa nahodha wa kwanza kuiongoza Taifa Stars kufuzu Afcon mara mbili.

Noti nje nje

Ikiwa Taifa Stars itafuzu Afcon, itajihakikishia kitita cha Dola 534,000 (Sh 1.3 bilioni) kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf), lakini pia wachezaji watapata bonasi ya Sh 500 milioni kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Algeria malalamiko kibao

Kocha wa Algeria, Djamel Belmadi ameonekana kutofurahishwa na uamuzi wa Chama cha soka nchini humo kupeleka mechi Annaba akidai ni uwanja ambao hauna ubora akihofia unaweza kuathiri ufanisi wa timu yake.

“Uwanja hauko tayari kuandaa mechi ya timu ya taifa, hivyo tunatakiwa kutafuta suluhisho lingine. Uwanja haupo kama ulivyokuwa mwezi Juni. haupo katika ubora ambao tunautaka kwa mechi ya kimataifa,” alisema Belmadi.

Stars matumaini kibao

Kocha wa Taifa Stars, Adel Amrouche alisema timu yake imejiandaa vizuri kupata matokeo mazuri dhidi ya Algeria leo Alhamisi.

“Tunachohitaji ni kufuzu Afcon. Tumekuwa na kambi na maandalizi mazuri kwa ajili ya mchezo huu na wachezaji wako tayari kutimiza lengo hilo,” alisema Amrouche. Watanzania wote dua kwa timu yao huku wakiiombea mabaya Uganda.

Chanzo: Mwanaspoti